Na Joseph Ngilisho ARUSHA
JIJI la Arusha kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa wilaya wametumia kumbukizi ya kifo cha hayati Mwalimu Julias Kambarage Nyerere kufanya matembezi ya amani kuhamasisha wananchi kujiandikisha daftari la mpiga kura ili kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa Novemba 27,2024.
Akiongea katika viwanja vya mashujaa baada ya matembezi hayo yaliyoanzia katika ofisi za jiji hilo hadi soko la Kilombero , Mkurugenzi wa jiji la Arusha ,John Kayombo aliwataka wakazi wa jiji hilo kumuenzi baba wa Taifa kwa kujiandikisha kwa wingi ili kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa.
Kayombo ambaye pia ni msimamizi wa uchaguzi huo,amesema kuwa jiji la Arusha limetenga vituo 462 ili kuwapatia fursa wananchi kujiandikisha kwa wingi bila kukaa kwenye foleni kwa muda mrefu.
"Tumeamua kuongeza vituo vya kujiandikishia kutoka vituo 154 hadi vituo 462 ili wananchi wasipoteze muda mwingi kwenye zoezi hili la kujiandikisha"
Alisema wananchi lazima watambue kuwa uchaguzi huu wa serikali za mitaa ni tofauti na uchaguzi mkuu wa mwaka ujao 2025 hivyo wananchi wasichanganye ,kadi za uchaguzi mkuu hazikupi fursa za kwenda kumchagua Mwenyekiti wa serikali za mtaa.
Mkuu wa wilaya ya Arusha,Felisician Mtahengerwa alisema kula tarehe 14,oktoba kila mwaka taifa linaadhimisha kumbukizi ya kifo cha Rais wa Kwanz wa Tanzania Hayati Mwl.Julias Nyerere ambaye alifanikisha kuwaunganisha watanzania kupitia makabila yao na kuwa na lugha moja ya Kiswahili.
Aliwataka wananchi kuendelea kuyaenzi maono ya mwasisi wa Taifa mwl.Nyerere ambaye alifanikiwa kutujengea msingi imara ya amani.
DC Mtahengerwa aliwataka wananchi kuwakataa watu wenye nia ovu ya kutaka kutugawa kwa maslahi yao na kuendelea kudumisha amani iliyoachwa na baba wa Taifa kwa maslahi yao.
Pia alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi katika wilaya hiyo kujiandikisha kwa wingi ili kutumia haki yao ya msingi kupiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu.
Ends..
0 Comments