Na Joseph Ngilisho ARUSHA
Waziri wa nchi Ofisi ya Rais, Tawala za mikoa na serikali za Mitaa TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa ,amewaagiza wakuu wa mikoa na wilaya hapa nchini kuwatafuta popote walipo watoto wenye ulemavu ambao wamekuwa wakifichwa majumbani na wazazi ama walezi na kuwanyima haki ya elimu.
Mchengerwa ameyasema hayo leo septemba 17,2024 wakati akifungua maadhimisho ya miaka 30 ya utekelezaji wa elimu Jumuishi , katika shule maalumu ya Sekondari Patandi wilayani Arumeru Mkoani Arusha ikiwa ni utekelezaji wa mkataba wa kimataifa wa Salamanka uliosainiwa na serikali mwaka 1994 na kuanza kutumika rasmi mwaka 1997.
Waziri Mchengerwa alisema kupitia maadhimisho hayo serikali imelenga kuelimisha jamii ya kitanzania kuona umuhimu wa kutumia mfumo wa elimu Jumuishi kumpatia mwanafunzi mwenye mahitaji maalumu fursa ya kupata elimu bora kwa kuzingatia mahitaji yake.
"Ikumbukwe kuwa Tanzania imeridhia na kusaini mikataba mbalimbali ya kimataifa na kikanda inayohusu elimu Jumuishi ,miongoni mwa mikataba hiyo ni Tamko la Salamanka la mwaka 1994 na tamko la Dakaa la mwakla 2000 ambayo yameelekeza kila nchi kutafsili kwa vitendo na kutekeleza elimu Jumuishi kwa mazingira yaliyopo katika nchi husika"
Alisema nchi yetu Tanzania elimu Jumuishi ilianza kutekelezwa muda mrefu kupitia sera ya elimu ya mwaka 1978 iliyoelekeza upatikanaji wa elimu kwa kila mtoto,utekelezaji wa sheria hiyo kwa watoto wenye mahitaji maalumu umerasimishwa mwaka 1998 kupitia mradi wa wizara ya elimu kwa kushirikiana na shirika la kimataifa la elimu , sayansi na utamaduni (UNESCO).
"Katika Taifa Letu bado tuna watu wenye kufikiri kwamba mtoto mwenye changamoto hana haki ya kupata elimu, nichukue nafasi hii kuwaagiza wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya, wekeni utaratibu wa kufuatilia jamii hiyo kuanzia ngazi ya makazi ya wananchi kama kuna mtoto mwenye changamoto amefichwa serikali ichukue hatua mara moja"
Waziri amesema kuwa idadi ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu imeendelea kuongezeka na kufika 78,429 mwaka 2024.Alisema serikali imetenga jumla ya shule 6088 zinazopokea wanafunzi hao na kuwapatia Afua stahiki na miongoni mwa shule hizo, shule 309 zina mabweni kwa ajili ya wanafunzi hao.
Kutokana na kuongezeka kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu nchini, serikali imejenga shule mbili maalumu za mfano moja wapo ni shule maalumu ya Patandi.
Alisema serikali imedhamiria kuwapatia taaluma stahiki wanafunzi wenye mahitaji maalumu kwa kuhakikisha wanapata chakula cha uhakika kwa kutoa ruzuku kwa mwanafunzi wa kutwa na bweni .
Awali Mkurugenzi wa elimu maalumu, dkt. Magreth Matonya kutoka wizara ya elimu sayansi na teknolojia ,alisema maadhimisho hayo ya miaka 30 katika shule maalumu ya patandi yametokana na kuanza utekelezaji wa elimu jumuishi nchini ambapo Tanzania ilisaini mkataba wa kimataifa mwaka 1994.
"Maadhimisho haya yana malengo manne, kutangaza fursa kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu, kutangaza mafanikio ,kutoa elimu ya uhamasishaji kwa wazazi wanaowaficha watoto na kutoa tathimini tulipo na tunapoelekea"
Dkt Matonya alisema dhana ya elimu Jumuishi ni kuwaweka pamoja wanafunzi wenye mahitaji maalumu na wasio na mahitaji maalumu waweze kusoma kwa kutegemeana na kusaidiana
Alisema tangia kuanza kwa mpango huo wa elimu jumuishi serikali imefanikiwa maeneo 36 ikiwemo kuanzisha kamusi ,kuboresha vyuo vya ualimu ambapo mwaka 2024 jumla ya walimu 768 wamehitimu pia ununuzi wa vifaa vya kujifunzia kwa wanafunzi wenye mahitaji.
Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na Maafisa Elimu wa Mikoa, Maafisa Elimu Watu Wazima Mikoa yote, Wakurugenzi wa Halmashauri, Maafisa Elimu Msingi na Sekondari, Maafisa kutoka Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Maafisa Elimu Maalum wa Halmashauri na Wadau mbalimbali wanaoihunga mkono Serikali.
Ends...
0 Comments