Na Joseph Ngilisho ARUSHA
Viongozi wa dini ya Kiislamu kutoka taasisi ya Twariqa Mkoani Arusha, wamepinga maandamano yaliyoitishwa na chama Cha Siasa cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA,na kumwomba Rais Samia Suluhu Hassan kukutana na chama hicho kwa lengo la kutafuta njia iliyobora itakayosaidia kuepusha athari zinazoweza kujitokeza.
Kauli hiyo imetolewa na msemaji Mkuu wa Taasisi hiyo Sheikh Haruna Husein wakati akiongea na waandishi wa habari kueleza msimamo wa Taasisi hiyo baada ya CHADEMA kutangaza dhamira yao ya kuandamana Septemba 23 kushinikiza kupatikana kwa wafuasi wa chama hicho waliotekwa na kupotea.
Msemaji huyo alilaani vikali matukio ya utekaji na mauaji yanayoendelea hapa nchini hususani tukio la kiongozi wa ngazi za juu wa chadema Ally Kibao aliyeuawa baada ya kutekwa kwa kushushwa kwenye basi Septemba 8 Mwaka huu na watu wasiojulikana.
"Kwanza tuna laani vikali tukio la utekaji na kuuawa kwa Ally Kibao mfuasi wa chadema na wengine waliotekwa na kupotea hii hali tusikubali iendelee ,tunamwomba Rais Samia akemee na akomeshe mauaji hayo kupitia mamlaka yake "
Sheikh Husen aliwaomba viongozi wa dini hapa nchini kutokaa kimya bali waungane kulaani matukio ya aina hiyo yanayoichafua nchi yetu ambayo uchumi wake unategemea sekta ya utalii.
"Tunajua nchi yetu inajali demokrasia na kuruhusu maandamano ya amani ila sisi kama viongozi wa dini tunaomba tuliachie kwanza jeshi la polisi kukamilisha uchunguzi wake na tumwombe rais Samia akutane na vyama vya upinzani ili kujadili jambo hilo kwa njia ya amani na sio ya maandamano "
Shekh Haruna aliliomba jeshi la polisi kuharakisha uchunguzi ili wahusika wabainike na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
"Jeshi la polisi wafanye uchunguzi wa kina na wawe 'serious' na jambo hili wasiache nchi yetu ichafuliwe na watu wachache ,nawaomba vyama vya siasa waingie kwenye maridhiano wasilete taharuki kwenye nchi yetu"
Naye Mwenyekiti wa Mkoa wa Arushawa taaisisi hiyo ya Twariqa Ustadhi Shabaan Maulidi alishauri viongozi wa serikali na vyama vya siasa kukaa chini ili kujadili matukio ambayo yanaleta hofu kwa wanachi hususani matukio ya utekeji na mauaji.
Alisema watekaji ni genge la watu wachache wenye nia ovu ya kuharibu sifa ya Tanzania yenye amani ,hivyo sisi kama viongozi wa dini tunashauri uchunguzi wa kina ufanyike ili kudhibiti na kuwashughulikia wahalifu .
"Yanapotokea matukio ya watu kutekwa, kuuawa na kutolewa viungo haya ni matukio ambayo hayajazoeleka hapa nchini lazima tuungane viongozi wote wa dini kuyakemea bila kufumbia macho"
Naye Sheikh Iddy Ngella alimwomba Rais Samia kutoka hadharani na kukemea matukio ya utekeji na mauaji yanayoendelea hapa nchini .
Aidha alilitaka jeshi la polisi kukaa kitako na Chadema kwa njia ya amani kuliko mvutano unaoendelea kwa sasa kwani viongozi wa dini hawapo tayari kuona damu ikimwagika kwenye nchi iliyojengwa kwa misingi ya amani.
"Tunamwomba Rais Samia atoke hadharani na kutoa tamko la kukemea matukio ya uhalifu yanayoendelea nchini ,hali hii inachafua taswira ya nchi yetu na hivyo inaweza kuleta athari katika sekta ya utalii "
Aidha viongozi hao wa dini waliwataka viongozi wenzao kutoogopa kusemwa kuwa wanatumika, wakati wa kuongelea masuala ya msingi kama hayo bali watumie mamlaka yao kama wajibu wao katika kukemea kupinga na kuonya pale kunapojitokeza hali ya uvunjifu wa amani.
Ends...
0 Comments