Na Joseph Ngilisho ARUSHA
SHULE yenye mchepuo wa Kiingereza ya Tumaini Junior iliyopo wilayani Karatu Mkoa wa Arusha, imejivunia mafanikio bora ya ufaulu kwa miaka 20 yaliyotokana na matokeo mazuri kwa wanafunzi 895 waliohitimu elimu ya msingi tangu kuanzishwa kwake mwaka 2004 na kuifanya kuwa kinara kwa ukanda huo na kitaifa.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa shule hiyo Modest Bayo katika mahafali ya 14 ya shule ya Tumaini Junior yaliyoenda sanjari na maadhimisho ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwa shule hiyo.
Aidha alisema matokeo mazuri ya ufaulu yameifanya shule hiyo kuwa miongoni mwa shule 10 bora na shule 100 bora kitaifa kati ya shule 10659 katika kipindi cha miaka 10 mfululizo.
"Tangu kuanzishwa kwa shule ya Tumaini Junior katika wilaya yetu ya Karatu tumeweza kushika nafasi ya kwanza mara 9 na nafasi ya pili mara nne na mwaka 2018 shule yetu imefanikiwa kutoa mwanafunzi wa kwanza wa kike Kitaifa aliyefaulu vizuri kwa kupata alama za juu "
Bayo alisema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mzuri kati ya walimu na wanafunzi,kuwepo kwa vitendea kazi pamoja na kuwajenga uwezo wa kifikra, kimazingira na kimaadili mema wanafunzi wote pamoja na kuwapatia elimu ya kujitegemea.
Alisema kuanzishwa kwa shule hiyo ya Tumaini Junior kumezalisha shule nyingine ya sekondari ya Tumaini Senior yenye kidato cha Nne hadi cha sita iliyopo Makuyuni wilayani Monduli na shule ya awali Tumaini TX ambazo zote zimetokana na zao la Shule hiyo.
Aidha Bayo amewahakikishia wazazi kutojutia uamuzi wa kuwaleta watoto wao katika shule hiyo kwa kuwa anauhakika wa ufaulu mzuri katika matokeo ya mtihani wa kitaifa kwa wahitimu wa darasa la saba mwaka huu.
Alisema shule yake imekuwa ikitoa mchango wa ajira kupitia wanafunzi wanaohitimu katika shule hiyo ,ambapo hadi sasa jumla ya wafanyakazi 146 wametokana na zao la shule hiyo na hivyo kuisaidia serikali kukabiliana na wimbi la ukosefu wa ajira nchini.
Awali Mwalimu mkuu wa shule hiyo ya Tumaini Junior, Gasper Silvery alisema matokeo mazuri ya ufaulu kwa wanafunzi ni pamoja na kuwa na walimu wengi wenye uwezo mzuri kufundosha ,ambapo shule hiyo inawalimu wapatao 40 wanaofundisha wastani wa wà nafunzi 800 wanaosoma katika shule hiyo.
"Tunatarajia kuwa na huduma bora zaidi ya hii kwa wanafunzi wetu ili tuhakilishe tunafanya vizuri zaidi katika matokeo ya kitaifa,tumeanzisha mashirikiano na vyuo vikuu vya nje ili kubadilishana uzoefu zaidi,ambapo walimu wetu watanufaika kupata mbinu na ujuzi wa kufundisha na kuwapa manufaa wanafunzi wetu na tunampango wa kuwaongezea teknolojia zaidi "
Katika mahafali hayo ya darasa la saba jumla ya wahitimu 98 wamemaliza masomo yao wakiwemo wasichana 50.Ambapo wametakiwa kuyaishi yale mema yote waliofundishwa huku kujiepusha kujiingiza katika matendo maovu yasiofaa katika jamii.
Ends..
0 Comments