RAIS SAMIA: MAUAJI HAYAJAANZA TANZANIA YAPO KILA MAHALA MABALOZI MSITUELEKEZE NINI CHA KUFANYA

 By Ngilisho Tv-MOSHI


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amesema matukio ya mauaji yanatokea katika kila nchi na Tanzania haijawahi kuagiza Balozi wake aseme jambo kwa nchi nyingine.


"Utasikia mtoto kabeba bunduki kaenda kushambulia shule, kadhaa wamekufa, kufa kupo tu. Kwa njia yoyote matukio haya yanatokea katika kila nchi."


Ametoa kauli hiyo leo katika hafla ya kufunga Mkutano wa Maafisa waandamizi wa Jeshi la Polisi, na maadhimisho ya miaka 60 ya jeshi hilo, yaliyofanyika Moshi mkoani Kilimanjaro.





Rais Samia amesema matukio haya yanapotokea katika nchi nyingine, “sisi hatujawahi kuziambia nchi kupitia balozi wetu, ‘hebu waambie hao.’ Sasa wengine wasiwe mafundi wa kutuelekeza nini cha kufanya."


Kauli ya Rais Samia imekuja wiki moja tu tangu Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania, kutoa wito wa uchunguzi huru kuhusu matukio ya utekaji na mauaji nchini Tanzania.


Rais Samia ameweka wazi kuwa serikali yake haikubaliani na yanayotokea, na kifo chochote kile kinaumiza na wale wanaotaka kuonesha huruma zao wafanye hivyo kwa kufuata makubaliano ya mahusiano ya kidiplomasia ya kimataifa.


“Tunapotekeleza falsafa ya 4R sio kwamba tumetupilia mbali sheria za Nchi yetu au tumeruhusu utovu wa nidhamu utokee ndani ya Nchi yetu lahasha, sheria ziko palepale , mila desturi zetu ziko palepale, miongozo ya kufanya mikutano na mengine yote yapo palepale, 4R ni falsafa iliyokuja kuunganisha Taifa na sio inayoruhusu utovu wa nidhamu kwa baadhi ya Watu”


“Hatutovumilia vitendo vyovyote vya kuleta machafuko na mifarakano Nchini hatutovumilia, ni vizuri tusisahau au wale wanaojiandaa na machafuko wasishangae mapito waliyopita, ni falsafa hiihii ndio imewapa ruhusa ya kurudi hapa Nchini, tukafumbia macho mengine yote njooni tujenge Taifa letu, sasa kama wameshaota mikia sasa sheria zilezile bado zipo”


“Kule kwetu kuna Watu wanaitwa Makhulukutabu ni Watu wenye hulka za kuishi kwenye tabu tu, kwenye utulivu kwenye raha aah kwao sio mahali kwao, Mungu kaumba Watu wa aina hii na Tanzania tunao, sasa sheria za Makhulutabu pia zipo tutashughulika nao, wasisahau mapito waliyopita”


“Watu walewale wanaposahau yote haya na kutoa kauli za kuturudisha nyuma sisi hatutokuwa tayari, amani na utulivu wa Nchi yetu tutalinda kwa gharama yoyote kama Nchi nyingine zinavyolinda Nchi zao nasi Watanzania tutalinda Nchi yetu kwa gharama yoyote” —— Rais wa Tanzania, Dkt. Samia kwenye maadhimisho ya miaka 60 ya Jeshi la Polisi Mkoani Kilimanjaro leo September 17,2024


Ends..

Post a Comment

0 Comments