OPERESHENI YA EWURA YAPUNGUZA UCHAKACHUAJI WA GESI ZA MAJUMBANI,WENGI WAKAMATWA


Na Joseph Ngilisho ARUSHA 


MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA)Kanda ya Kaskazini, imesema kuwa ukaguzi wa mara kwa mara kwa wauzaji wa mitungi ya gesi ya majumbani LPG imepunguza uchakachuaji wa kuwaibia wateja unaofanywa na baadhi ya mawakala wasiowaaminifu wenye  lengo la kujiongezea kipato kwa njia haramu.


Akiongea katika semina ya mawakala wa gesi za majumbani LPG Mkoani Arusha iliyoandaliwa na kampuni ya ORYX Gesi Tanzania, Meneja wa EWURA kanda ya Kaskazini ,Lorivii Long'idu alisema EWURA imekuwa ikiwakumbusha wauzaji na wasambazaji wa gesi za Majumbani namna ya kuzingatia ubora wa utunzaji na usafirishani wa mitungi katika njia salama.



Alisema kuwa EWURA imepata mafanikio makubwa kupunguza suala la uchakachuaji wa mitungi mikubwa na midogo ya gesi kwa kuwakamata wafanyabiashara wasio waaminifu wanaoendesha vitendo hivyo na kuwachukulia hatua kali .


Alisema katika Mikoa ya Tanga ,Kilimanjaro na Arusha wafanyabiashara kadhaa wamechukulia hatua kutokana na tabia hiyo ya uchakachuaji ili kujinufaisha na faida kubwa kwa  kuwaibia walaji.


"Tumeendelea kuwakamata baadhi ya wafanyabiashara wanaojihusisha na ukiukwaji wa uuzaji wa gesi kwa kujihusisha na uchakachuaji katika mikoa ya Tanga,Kilimanjaro  na Arusha na kuwachukulia hatua za kisheria na hali hii imefanikiwa kupunguza malalamiko kwa wateja"


"Tumekutana hapa kuwakumbusha wafanyabiashara wasambazaji wakubwa na wadogo wa gesi ya LPG ya ORYX  taratibu na sheria za ufanyaji wa biashara hiyo na kuwasisitiza namna ya uuzaji bora wa bidhaa hiyo na kuwakumbusha namna ya kupata leseni za uuzaji wa bidhaa hiyo zinazopatikana katika ofisi ya EWURA "


Aliwataka wafanyabiashara wa gesi kuwa na mikataba na makampuni inayowasambazia  gesi za majumbani ,suala ambalo litasaidia kuibana kampuni husika iwapo mitungi yao itabainika kwenda kinyume na takwa la kisheria.


 Awali afisa Mauzo wa Kampuni ya ORYX kanda ya kaskazini, Gamu Kimolo alisema lengo la kuwakutanisha mawakala wa gesi ni kuwakumbusha wajibu wao kwa kuwapati elimu ili wawe mabalozi mazuri katika matumizi ya gesi za Majumbani LPG.


Alisema tangia wameanzisha  utaratibu wa kutoa elimu kwa mawakala wao ,imesaidia kuongeza usalama majumbaji juu ya matumizi ya gesi ya LPG na  kupunguza majanga yanayotokana na mitungi ya gesi isiyosalama.


Kimolo alisema kuwa kampuni yake imekuwa ikiwafungia baadhi ya mawakala wanaokiuka taratibu za uuzaji wa gesi kwa kuchakachua kwa kutoa gesi mtungi wa kampuni moja na kuweka mtungi  wa kampuni nyingine pia kuuza bei kinyume na bei elekezi ya kampuni .





Ends...











Post a Comment

0 Comments