MAANDALIZI JMAT DAY YAPAMBA MOTO BAJETI NZITO YAPITA,DC AKEMEA MAOVU, ASKOFU ASEMA BAADHI YA VIONGOZI WA DINI WAMEGEUZA DINI KICHAKA CHA KUPIGA PESA

 Na Joseph Ngilisho ARUSHA 


Mkuu wa wilaya ya Arusha,Felisician Mtahengerwa ameitaka jumuiya ya maridhiano na amani Tanzania (JMAT) ,kutumia umoja wao kukemea matendo maovu yanayomea kila kukicha katika jamii kutokana na mmomonyoko wa maadili na kusababisha mauaji,ubakaji ,ulawiti na mapenzi ya jinsia moja.

Akiongea katika kikao cha pili cha kamati ya maandalizi ya siku ya kuzaliwa kwa JMAT itakayofanyika Machi 5,2025 jijini Arusha,Mtahengerwa aliipongeza kamati hiyo  inayoongozwa na Askofu Eliud Isangya pamoja na Askofu dkt Israeli Maasa katibu wa JMAT Taifa kwa hatua nzuri iliyofikia ya maandalizi hayo.

Mkuu huyo wa wilaya alisema jumuiya ya maridhiano na amani inayoundwa na viongozi wa dini na mila ni msingi wa amani hapa nchini ,na ina wajibu wa  kuwakumbusha wazazi na walezi juu ya misingi bora ya malezi.

"Niwaombe sana viongozi wa dini bado tunashida ya malezi ulawiti,ushoga vinazidi kutamalaki kwa kasi kubwa, tusaidieni kuwakumbusha wazazi wajibu wao  katika misingi ya malezi,wazazi tumesahau malezi tumekuwa watu wa mitandao ,vitu vya kuiga vinatupoteza"alisema.


Mwenyekiti wa JMAT Mkoa wa Dodoma, Prof.Emmanuel Shija alisema kuwa suala la maadili linapaswa kuzingatiwa na pande zote wakiwemo viongozi wa dini na jamii kwa ujumla kwa kila mtu kutimiza wajibu wake.

Alisema kuanzishwa kwa JMAT kumesaidia kupunguza mmomonyoko wa Maadili ,aliwataka viongozi wa dini kujitolea zaidi katika kuielimisha jamii ili kuondokana na matukio maovu.

Naye mmoja ya viongozi  wa dini Sheikh Shabaan Juma ,Sheikh wa mkoa wa Arusha, alipongeza chombo hicho cha JMAT kwa utendaji wake kuhusu kudumisha amani hapa nchini .

Sheikh aliwaomba viongozi wa dini kuwa watu wa mfano kwa matendo yao ili yaendane na kile wanacho kihubiri  kwa waumini wao na kwa jamii yote hapa nchini.


Askofu mkuu wa kanisa la Furaha Taifa (KLFT),Jonnes Molla alisema suala la mmomonyoko wa maadili linatokana na baadhi ya viongozi wa dini kusahau majukumu yao na kujikita katika utafutaji wa fedha.

Askofu Molla ambaye pia ni Mwenyekiti wa JMAT mkoa wa Kilimanjaro  alisema viongozi wa dini wameweka pembeni wajibu wao na kuelekeza nguvu zao katika utafutaji wa pesa kiasi kwamba wanaiona pesa kama mungu,wanaipenda pesa kuliko hata mungu ,ndio maana matukio ya dhambi yameongezeka

"Makundi maovu  yamezidi kuongezeka baadhi ya viongozi wa dini wanaitumia dini kama kichaka cha kujificha na maovu yao, mtu anauza udongo ,maji chumvi kutafuta pesa uliona wapi "Alihoji askofu


Baadhi ya wajumbe wa JMAT ,Mwanaidi Kimu na Justine Laizer walisema JMAT imekuwa  msaada mkubwa kwa jamii katika kudumisha amani hapa nchini kutokana na hamasa wanayoifanya kuanzia ngazi ya mitaa ,vitongoji na vijiji.

Aidha walisema maandalizi ya siku ya maridhiano yanaenda vizuri na wao kama viongozi wa ngazi ya kata wanaimani kila kitu kitakuwa sawa.












Kwa upande wake Kaimu kamanda wa polisi Mkoa wa Arusha,ACP Peter Lusesa, aliipongeza JMAT kwa kuwa mdau mkubwa wa amani hapa nchini na kusema  kuwa  jeshi la polisi linawajibu  wa kushirikiana  na JMAT katika kudumisha amani kupitia maridhiano .

Awali akifungua kikao hicho Mwenyekiti wa kamati ya Maandalizi, Askofu Eliud Isangya aliwaeleza wajumbe namna maandalizi hayo yanavyoendelea vizuri huku mhasibu wa kamati hiyo Sadati Cosmas akisoma bajeti ya sh, milioni 545 inayotarajiwa kutumika katika maadhimisho  ya siku ya  maridhiano yatakayohudhuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha AICC.




Ends....




Post a Comment

0 Comments