Na Joseph Ngilisho ARUSHA
ZAIDI ya washiriki 600 na mashirika 500 yasiyokuwa ya kiserikali kutoka ndani na nje ya nchi, watashiriki katika wiki ya Azaki itakayofanyika jijini Arusha, kuanzia kesho Septemba 9 hadi 13 mwaka huu 2024
Akiongea na vyombo vya habari Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Wiki ya Azaki mwaka 2024, Nesia Mahenge,alisema mkutano huo utafunguliwa kesho na Waziri wa mipango na uwekezaji
Alisema kuwa jumla ya washiriki zaidi ya 600 kutoka hapa nchini na nje ya nchi mashirika 500 yatashiriki kwenye mkutano huo wa Azaki.
Hata hivyo,alisema mgeni rasmi atakuwa ni Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo,pia kutakuwapo na viongozi wengine kutoka nje ya Tanzania akiwamo Balozi wa Umoja wa Ulaya(EU) na Balozi wa Canada.
Alisema lengo la mkutano huo, kwa mashirika hayo yasiyokuwa ya kiserikali ni kukutana na kujifunza,kubadilishana uzoefu kutoka kwenye mashirika hayo.
Alisema pia watakwenda kwenye jamii kuangalia mambo yaliyofanywa na Serikali katika jitihada za kuwaletea maendeleo wananchi na Watanzania kwa ujumla.
"Kama mashirika yasiyokuwa ya kiserikali tutaangalia namna ya kuwawezesha wananchi katika jitihada zilizofanywa na Serikali katika kuwaletea maendeleo wananchi wetu,"alisema.
Naye John Kalaghe, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la HakiElimu, alisema katika wiki hiyo ya Azaki,watakuwa na kipindi cha ushiri wa vijana hasa katika michakato ya kidemokrasia ndani na nje ya mifumo ya shule.
"Tumeandaa sesheni ya vijana ambayo watazungumza juu ya ushirika wao katika suala la michakato ya kidemokrasia,"alisema.
Licha ya kuzungumza hayo,alisema tofauti ya mijadala mingine,watawakutanisha vijana na watapata fursa ya kujadiliana kuhusu ushirika wao katika michakato hiyo.
"Lengo la kuandaa sesheni hii kwa vijana ni kuwahamasisha kushiriki katika michakato ya kidemokrasia kwa kuwa ukiangalia tafiti mbalimbali zilizofanyika ushirika wa vijana katika michakato hiyo ni hafifu.
"Tunataka kuangalia na kujadiliana umuhimu wa vijana kushiriki kwenye michakato hiyo, kwa kuwa mwaka huu na mwakana kuna fursa kwa kundi hili kuchukua fomu za kugombea katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu mwaka 2025.alisema"
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Foundation for Civil Society(FCS),Justine Rutenge,alisema katika wiki hiyo ya Azaki kutakuwepo na mada mbalimbali ikiwamo ya suti,dira na thamani.
"Tuko katika kipindi ambacho kina michakato ya kidemokrasia kwa kuwa tunaelekea kwenye uchaguzi wa serikali mitaa, uchaguzi Mkuu wa mwakani na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, hivyo vijana watapata fursa ya kupaza sauti zao kwa kuwa ni muhimu kwao.
Mkurugenzi wa Mtandao wa jinsia Tanzania Tanzania (TGNP),Lilian Liundi amesema kuwa,zaidi ya waandaaji 20 kutoka asasi za kiraia wakishirikiana katika kuandaa wiki hiyo ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni sauti,dira na dhamani.
Liundi amesema kuwa,mwaka huu wanataka sauti ya mwananchi iweze kusikika kwani kuna umuhimu wa kuweka sauti za wadau wote na upana wao kuhusu kuzungumza maswala mbalimbali.
“Tunataka kuona sauti za watu mbalimbali zinasikilizwa huku wanawake tukitaka watoe sauti zao na kusikilizwa na kuangalia dira ya 2050 kuhusu maswala ya wanawake na uwekezaji katika dira kwani tunataka swala la uwekezaji liwe kipaumbele.”amesema .
Kwa upande wake Mkuu wa kitengo cha sekta za umma kutoka benki ya Stanbic , Doreen Dominic amesema kuwa,wamekuwa wakifanya wiki hiyo kwa mfululizo mwaka wa sita sasa huku lengo kubwa likiwa ni kupaza sauti ya pamoja katika maswala mbalimbali .
Ameongeza kuwa,kupitia wiki hiyo wanaungana na taasisi mbalimbali katika kufanya maboresho mbalimbali na kujadili sauti ya pamoja na kuhakikisha wanapigania haki za watanzania wote waliopo katika maeneo mbalimbali ili waweze kupata haki zao za msingi .
Ends...
0 Comments