WAHITIMU CHUO CHA AFYA CEDHA WATAKIWA KUSIMAMIA KANZI DATA HOSPITALINI, MKUU WA CHUO APONGEZA UWEKEZAJI WA SERIKALI WA TRILIONI 6.7 SEKTA YA AFYA

Na Joseph Ngilisho ARUSHA 

Wahitimu wa kada mbalimbali za Sayansi ya Afya katika kituo cha Maendeleo ya Elimu ya Afya (CEDHA),wametakiwa kusimamia vema mifumo ya kanzi data iliyopo mahospitalini ili kuwepo na takwimu sahihi zitakazosaidia kuboresha huduma za Afya nchini.


Pia wametakiwa kujitenga na suala la mmomonyoko wa maadili kwa watumishi wa umma ikiwemo vitendo vya rushwa, kutowajibika kwa wagonjwa,lugha chafu pamoja na uharibifu wa vifaa vya umma.

 

Rai hiyo imetolewa na Meya wa Jiji la Arusha Maxmilian Iranghe wakati wa Mahafali ya 37 ya chuo hicho, ambapo  jumla ya wahitimu 29 kutoka kada mbalimbali za afya walimaliza masomo yao.


"Mkatoe huduma bora  kwa wateja wote wa huduma ya afya na kusimamia mifumo ya kanzi data iliyopo hospitalini ili tuwe na takwimu sahihi zitakazotumika  na wizara ya Afya katika kuboresha huduma za afya na kwa kufanya hivyo myakuwa mnatekeleza kwa vitendo falsafa ya rais wetu ya kuboresha huduma ya afya nchini"Alisema Iranghe


Aliwasihi wahitimu  kwenda kuwa mabalozi wema wa chuo hicho katika jamii zao kwa kuzingatia maadili mema waliojifunza, kwani elimu na taaluma bila maadili si kitu chochote. 


Mstahiki Meya alikipongeza chuo cha afya cha CEDHA kwa kuwa kuwa mkombozi sekta ya afya nchini kwa kutoa wataalamu bora wa afya.


Alisema kuwa chuo hicho kinalo jukumu kubwa la kusaidia jitihada za Serikali kutekeleza mpango wa MMAM kwa kuandaa wakufunzi wa watumishi wa afya na kuandaa wataalamu wa taarifa za afya ambao ndio msingi wa kuzichakata data zote za afya na kupata taarifa sahihi za kuboresha huduma mbalimbali. 

Awali mkuu wa chuo hicho cha CEDHA ,dkt Johannes Lukumay alisema anajivunia mafanikio makubwa ya kuendelea kutoa wahitimu bora wa kozi ya sayansi ya Taarifa za afya na Ualimu wa Afya ambapo kilele cha mafanikio hayo ni wahitimu 29 katika mahafali ya 37.


Dkt. Lukumay aliipongeza serikali kupitia wizara ya Afya kwa kuratibu na kusimamia uwekezaji mkubwa wa sh, Trilioni 6.7 zilizotolewa na serikali kwa ajili ya kuboresha sekta hiyo ikiwemo ujenzi wa mindo mbinu ,ununuzi wa vifaa tiba ,kusomesha madaktari bingwa na bobezi pamoja na ajira za watumishi wa Afya.


Alisema kuwa chuo cha Afya Cha CEDHA kilianzishwa mwaka 1983 kikiwa na majukumu manne ambayo ni kufundisha  mbinu za kuwafundisha wakufunzi wa vyuo vya taaluma za Afya,kuwaendeleza kitaaluma watumishi wa Sekta ya Afya waliopo katika Nyanja Mbalimbali ,kufanya tafiti zenye kutatua changamoto za sekta ya afya na kutoa ushauri elekezi katika masuala ya Afya.


Alisema katika mwaka wa fedha 2024/25 CEDHA imepanga kuendesha mafunzo kulingana na majukumu iliyokasimishwa  na wizara ya Afya .Taasisi itatekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa majengo matatu ,utawala,Mikutano na Malazi ya watu 200.


"Pamoja na mipango mizuri inayotekelezwa CEDHA,taasisi yetu inakabiliwa na baadhi ya changamoto ikiwemo mwitikio mdogo wa wakufunzi kuhudhulia mafunzo "Alisema.







Ends...



Post a Comment

0 Comments