Na Joseph Ngilisho-MERERANI
WACHIMBAJI na wadau wa Madini ya Tanzanite,Mererani katika Mkoa wa Kimadini wilaya ya Simanjiro mkoa wa Manyara wamedai utaratibu wa kikanuni uliowekwa na serikali wa kuhamishia soko la madini ya Tanzanite eneo la Mererani , unatija na umeongeza mzunguko na thamani ya biashara hiyo.
Wakiongea katika mkutano na waziri wa Madini,Anthony Mavunde katika mji mdogo wa Mererani wamemweleza kuwa tangia kufunguliwa kwa soko hilo kumeleta amani na ongezeko la thamani ya madini hayo baada ya serikali kudhibiti uuzwaji holela uliopelekea madini hayo kutoroshwa na kutojulikana yanatoka nchi gani.
Baadhi ya wafanyabiashara wa madini hayo,Sengeyu Laizer na Jumanne Kilo ,walidai kuwa ziara ya Waziri wa madini imewapa faraja baada ya kuwahakikishia kwamba soko la madini ya Tanzanite litaendelea kubaki Mererani ikiwemo uchakataji na uongezaji wa thamani.
Sengeyu Laizer alisema kabla kudhibitiwa kwa soko hilo kuuzwa kiholela,Tanzanite iliadimika nchini badala yake ikawa na soko nchi za nje na kupelekea wafanyabiashara wakubwa pekee kunufaika ila kwa sasa wanaishukuru serikali maana hata wafanyabiashara wadogo wa madini wananufaika.
"Kuwepo kwa soko hili kumetuongezea kipato kwa sisi wafanyabiashara wadogo,pia kutafanya nchi yetu ijulikane zaidi kimataifa ,na soko hilo litakaribisha wanunuzi wakubwa kutoka masoko makubwa ya madini duniani na mji wetu wa Mererani umeanza kustawi tofauti na hapo awali"Alisema Mfanyabiashara Kilo.
Akitoa taarifa ya mwenendo wa soko hilo,Ofisa wa madini Mkazi Mererani, Nchagwà Marwaa alisema kuwa udhibiti wa madini hayo kumechangia ongezeko mzunguko wa biashara ya madini hayo na kwamba tangia kuanza kwa soko hilo madini ya bilioni 18.6 yamepatikana Mererani na kuuzwa nje ya nchi na serikali kuchuma mrabaha wa bilioni 1.
Alisema hadi sasa vibali 700 vya usafirishaji wa madini hayo nje ya nchi vimetolewa hadi kufikia mwaka huu 2024 .
Waziri wa Madini Anthony Mavunde, alisisitiza kuwa uchakataji wa kuongeza thamani madini hayo utaendelea kufanyika Katika soko la madini, Mererani wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara na kwamba suala hilo lipo kikanuni na hakuna atakayeweza kubadilisha utaratibu huo.
Mavunde amesema soko la madini ya tanzanite litabaki katika mji wa mirerani na kwamba madini hayo yataongezewa thamani ndani ya ukuta wa mirerani kama Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa walivyoagiza.
Alisema ujenzi wa jengo la Tanzanite City katika mji wa Mirerani unaogharimu zaidi ya Sh bilioni tano umefikia asilimia 80 na wiki ijayo mkandarasi anakabidhiwa fedha amalizie kazi na litakapokamilika litakuwa jengo la kimataifa
"Serikali imeamua kuwekeza kwa kujenga kitega uchumi cha jengo kubwa baada ya rais Kuachia sh,bilioni 5 ili biashara ya soko la madini hayo ifanyika katika jengo hilo na biashara ya madini ya Tanzanite itaendelea kufanyika Mererani "alisema Mavunde .
Hata hivyo baadhi ya wafanyabiashara wa Tanzanite kutoka mkoa wa Arusha, Noel Ole Varoya alipinga vikali utaratibu wa madini hayo kuuzwa katikansoko moja la madini Mererani pekee wakiitaka serikali iruhusu yaweze kuchakatwa katika masoko mingine hususani Arusha na kuuzwa .
Akiongea katika mkutano huo ,Olevaroya alimweleza waziri kuwa watu wanamdanganya rais pasipo kumwambia ukweli hasara inayotokana na uuzaji wa madini kwa mfumo huo wa soko moja Mererani.
Aliiomba serikali iruhusu madini hayo yauzwa katika masoko yote ya madini hapa nchini na yaruhusiwe pia kuongezewa thamani katika masoko mengine kwani hapa nchini hakuna wataalamu wa kutosha wa kuchakata.
"Mh waziri madini ya Tanzanite yaruhusiwe kuuzwa katika masoko yote yaliyopo mijini na yaruhusiwe kukatwa katika masoko mbalimbali mijini maana yanapokatwa Mererani pekee wanapokuja wanunuzi wakubwa wanataka yarudiwe kukatwa sasa hii ni hasara maana hadi sasa hatuna wakataji wazuri waliopo Mererani "
Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka alimshukuru Mavunde kwa kumaliza utata wa soko la madini ya tanzanite na akadai baadhi ya watu na wanasiasa walikuwa wakiyumbisha wafanyabiashara.
Ends..
0 Comments