Na Joseph Ngilisho ARUSHA
VIONGOZI wa dini kutoka wilaya ya Sengerema Mkoani Mwanza ,Kilimanjaro na Arusha wametembelea hifadhi ya Taifa ya Tarangire ikiwa ni hatua mojawapo ya kuhamasisha utalii wa ndani na kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo hapa nchini.
Viongozi hao kutoka taasisi ya dini ya kiislamu ya Twarika pamoja na wakristo waliungana kwa pamoja na kuamua kutembelea hifadhi hiyo ili kuhamasisha wananchi kujenga tabia ya kutembelea hifadhi na vivutio mbalimbali nchini.
Akiongea na waandishi wa habari walioambatana katika ziara hiyo,msemaji wa Taasisi ya Twarika Sheikh Haruna Husein alisema wao kama viongozi wa dini wamepanga kutembelea hifadhi mbalimbali nchini wakianzia na hifadhi hiyo ya Tarangire ili kujionea rasilimali zilizopo na kuzitangaza .
"Tumefika hapa Tarangire ikiwa ni mwanzo wa kutembelea hifadhi mbalimbali hapa nchini,tumejionea wanyama mbalimbali kama Tembo wakubwa, Simba,Nyati ,Pundamilia , Nyumbu na wanyama wengine wengi, tumejifunza mengi na tunatarajia kwenda katika hifadhi zingine "
"Tunawajibu wa kumuunga mkono rais Samia ambaye amekuwa mstari wa mbele kuhamasisha utalii kupitia filamu ya Royal Tour hali iliyosababisha kuongezeka kwa watalii na pato la taifa kupanda kupitia sekta ya utalii.
Sheikh Husein alilipongeza shirika la hifadhi za Taifa Tanapa kupitia Kamishna Mkuu wa uhifadhi ,Juma Kuji kwa kulinda na kuzitunza hifadhi zake zipatazo 21 hapa nchi, ikiwemo kuboresha miundombinu ya barabara za ndani ya hifadhi na kufanya hata gari ndogo kuweza kupitika kirahisi.
Hata hivyo aliliomba shirika hilo kupitia hifadhi zake kudhibiti wanyama wakali wanaoingia kwenye makazi ya watu na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali pamoja na kujeruhi wananchi na kusababisha vifo.
Naye mchungaji Sosteness, makamu askofu wa jimbo la Mwanza Magharibi kutoka kanisa la TNG Sengerema, alisema yeye ni mara ya kwanza kutembelea hifadhi za taifa nchini na amefurahi kujionea vivutio mbalimbali wakiwemo wanyama
ambapo hapo awali alizoea kuwaona kwenye picha ama kwenye Luninga.
"Nawashukuru wenzetu wa dini ya kiislamu kwa kuratibu safari hii na kutushirikisha , naimani tutatumie elimu hii tulioipata kuhamashisha waumini wetu na wananchi kutembelea hifadhi zetu"
Kwa upande wake Mkuu wa hifadhi hiyo ya Tarangire,kamishna msaidizi Mwandamizi,Beatrice Kesi alisema kumekuwepo na ongezeko la watalii wa ndani na kufikia 700 wanaotembelea kila siku katika hifadhi hiyo.
Alisema ongezeko hilo limetokana na mapinduzi katika sekta hiyo yaliyoletwa na rais Samia kupitia filamu yake ya The Royal Tour .
Alisema hifadhi hiyo yenye ukubwa wa kilometa za mraba zipatazo 2850 ilianzishwa miaka ya 1970 na mwaka huu itafikisha umri wa miaka 50 ikiwa ni hifadhi ya pili kwa kuingiza watalii wengi hapa nchini.
Aliwataka watanzania kujenga tabia ya kujionea vivutio vyao vilivyopo hapa nchini kuliko kuwaachia watalii pekee wanaotoka mbali kuja hapa nchini.
Ends..
.
0 Comments