USHIRIKINA UNAVYOGEUZA FURSA MTO UGALA,VIJANA WAGOMBEA MAPESA YAKITUPWA NA ABIRIA WA TRENI,


Baadhi ya abiria katika treni inayopita Kijiji cha Katambike, Kata ya Ugala, wilayani Nsimbo, mkoani Katavi wanadaiwa kurusha sarafu katika Mto Ugala kwa imani kuwa watatatuliwa matatizo yao.


Inadaiwa kuwa watu hao hutumwa kufanya hivyo na waganga wa kienyeji kwa kuwa "ndio sadaka kwa miungu iliyoko katika mto". Hutupa sarafu za Sh. 50, 100, 200 na 500. 


Nipashe imetembelea eneo hilo na kuzungumza na wasafiri na viongozi mbalimbali ambao wamelitaja ni jambo ambalo limekuwapo kwa muda mrefu kwa wenye imani hizo. 



Eneo hilo ambalo ni maarufu kwa jina la "Tutani", treni inapofika hapo, abiria wenye imani hiyo hurusha sarafu kupitia madirisha ya mabehewa ya treni kama njia ya kutimiza matakwa ya waganga wao. 


"Ni kweli hapa pana desturi ya watu kutupa fedha tutani; iwe treni inayotoka Mpanda kwenda Tabora wanatupa au inayotoka Tabora kwenda Mpanda wanatupa pia. 


"Hii desturi haijaanza leo wala jana, ni ya enzi na enzi, wanafanya hivyo kwa sababu watu wengi wanapokwenda kuchukua dawa kwa mganga wa kienyeji wanaulizwa 'unasafiri kwa njia gani?', akijibu treni anaambiwa 'hii dawa ili ikafanye kazi kule unakokwenda lazima ukifika kwenye Mto Ugala utoe sadaka ya fedha', fedha yoyote ile,”alisema Michael Jakabwe, mkazi wa Katambike. 



"Iwe Sh. 50, mia (Sh. 100), mia tano na sana fedha zinazotupwa pale zilizo nyingi sana ambazo tunazishuhudia ni 50, 100, 200 na 500, zinatupwa sana. 


"Unakuta mtu amebeba dawa ya kilimo, maana kwenye kilimo watu wanatumia dawa ili wapate mazao. Mfano, amebeba dawa ya kilimo na ili dawa ikubali kwenye mazao yake, lazima aitolee kafara ya fedha na hili jambo halijaanza leo. 


"Wengine wanabeba dawa za biashara, mganga anakwambia 'ukifika Mto Ugala sharti utupe fedha na anatoka amejiandaa kabisa na ile fedha ameiandaa kaiweka labda mfuko wa nyuma na zile fedha mara nyingi wanaambiwa zisichanganywe na fedha nyingine. 



"Wasipotoa kafara pale, wanaaminishwa kuna mzimu mkubwa unakaa kwenye mto ambao unaitwa "Silongwe", hivyo wasipotoa sadaka ya fedha ule mzimu utazuia dawa zao zisifanye kazi maana ule mzimu utachukia 'kwanini wapitishe vitu vyao bila kutoa kafara'. 


"Nikwambie tu ukweli, asikudanganye mtu zile fedha zina madhara kwa sababu wanaozitoa wanakuwa wamenuia, anayenuiza ni yule aliyeagizwa na mganga wake pale kuna watu wanakwenda kuokota zile fedha wanapata madhara. 


"Mfano, juzi tu hapa hata mwezi mmoja haujapita, kuna mtoto aliona fedha baada ya maji kupungua, akaenda kuichukua, yule mtoto alitumbukia kwenye maji na kufariki dunia," alidai. 



Hata hivyo, serikali haimini katika uchawi. Kuamini uchawi pia ni kosa la jinai kwa mujibu wa sheria za nchi. 


Salumu Katema, mkazi mwingine wa eneo hilo alisema: "Hiyo ni imani kwa kuwa wengi wanapotoka Mwanza na baadhi ya mikoa mingine ya Kanda ya Ziwa wanakuwa wamebeba dawa katika mabegi, wanaambiwa 'mkifika pale Ugala msipotupa hela, zile dawa mlizobeba zinafia palepale, zinakosa nguvu'. 


"Kwa hiyo, mtu akifika pale anachukua fedha anarusha kwenye maji au inaangukia kwenye mawe, asubuhi watu wanajipatia ridhiki.


 "Mara nyingi mimi huwa ninasafiri kutoka Mpanda kwenda Kaliua, tukifika pale Ugala watu wengi huwa tunatupa fedha, hata mimi huwa ninatupa. 



"Ni utaratibu ambao tumezoea ila inasemekana pale kuna mizimu kwa hiyo watu wanatupa vile kwa ajili ya matambiko," alisema Milimo Saidi, Mkazi wa Mpanda. 


"Unatupa hela yoyote, hata Sh. 10,000 haulazimishwi utupe sarafu tu, ni wewe mwenyewe utakayotaka, hata zaidi ya Sh. 10,000 kwa sababu ukitupa isipokwenda majini, watu wanachukua na wanatumia. 


"Sisi tumekuwa tunaokota pale hizo fedha,  tunazitumia hatujawahi kudhurika, hata watoto huwa wanakwenda pale wanajua kuna fedha," alisema Kashinde Mayanda, mkazi wa Ugala, akiibua hoja inayokinzana na mtangulizi wake aliyedai kuna madhara kuchukua fedha zinazotupwa mtoni huko. 


Mzee wa Kimila, Ibrahim Chatama alisema hicho kijiji kimeitwa Katambike kutokana na matambiko yanayofanywa hujko; kwamba ukifika pale wenyeji wanakwambia 'nenda ukatambike'. 


"Zamani elimu ilikuwa ndogo, watu walikuwa wanafuata mila zaidi kuliko elimu, mila zingine zilikuwa zinafuatwa, zilikuwa halisia, zingine zilikuwa potofu, zilikuwa haziwezi kusaidia wananchi. 


"Sehemu ile ya kijiji kilipo, kuna mto ambao ni Ugala, ni mrefu sana. Miaka ya nyuma wakati wanatengeneza reli kutoka Kaliua kuja Mpanda, sehemu ile iliwasumbua sana makandarasi, wakitengeneza tuta, asubuhi hawalikuti hata kama hakuna mvua. 


"Ilibidi waende wakawaone wazee kwenye kijiji hicho hicho, wakaambiwa 'hapa si mahala pa mchezo kuna mzimu unaitwa "Silongwe", bila kuuomba reli hii haitapita, sharti uombe kwa kutumia fedha na fedha zilizokuwa zinatumika zamani ni zile nyeupe (sarafu) zenye nembo ya Mwenge upande mmoja na upande mwingine kichwa cha Baba wa Taifa. Baada ya kufanya hivyo, reli ikakamilika. 


"Binadamu wengi tuna imani za kimila hususani wale wote wanaokuwa na dawa za kienyeji wanaambiwa 'wewe mkeo si anaumwa sana au mtoto anaumwa, basi chukua hii dawa ila ili uifikishe salama, ukifika pale Ugala sharti uombe ule mzimu ukupitishie salama'," alidai. 


Alisema kuwa zamani treni ilikuwa ikipita zile fedha zilizotupwa zilikuwa haziokotwi, lakini hivi sasa imekuwa fursa, kuna vijana wanakuwa pale treni ikipita watu wakirusha fedha, wanaokota na kuzifanyia matumizi yao na hawadhuriki, hakuna madhara yoyote. 


Kwa mujibu wa Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania, fedha ni tunu ya Taifa na kila mmoja ana wajibu wa kuilinda na kuitunza. Ni kosa la jinai kutupa au kuharibu fedha sarafu au noti. 


Kifungu cha 332A cha Sheria ya Kanuni za Adhabu, Sura 16, kinaelekeza: "Mtu yeyote, bila mamlaka, kwa kunuwia anaharibu, anachana, anakata au vinginevyo anachanachana noti yoyote ya benki au fedha ambayo inatumika kihalali, atakuwa anatenda kosa ambalo limo kwenye jedwali, na atakuhumiwa kutoa faini ya Sh. 5,000 kwa kila noti iliyoharibiwa au akishindwa adhabu ya kifungo cha mwaka moja."


Chanzo NIPASHE!

Post a Comment

0 Comments