UCHAGUZI MERERANI WAWAVURUGA WACHIMBAJI WAJUMBE WADAIWA KULAMBISHWA ASALI KWEUPE,MCHIMBAJI ALIA NA RMO 'ANATUVURUGA HAFAI'

 Na Joseph Ngilisho-MERERANI 


UCHAGUZI wa viongozi wa  kamati ya usuluhishi wa Migogoro ya wachimbaji wa Madini Mererani wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara,umeingia dosari mara baada ya  kudaiwa kugubikwa na vitendo vya rushwa kiasi cha baadhi ya wajumbe kulambishwa asali wakiwa ukumbini .


Baadhi ya washiriki wa kinyang’anyiro hicho,Elisafi Lema aliyekuwa mgombea katika uchaguzi huo alisema hakubaliani na matokeo ya uchaguzi huo kwa sababu haukuwa huru na haki na uligubikwa  na vitendo vya rushwa huku wagombea wengi wakikosa sifa za kugombea ila waliingizwa kwenye kinyang’anyiro hicho kwa maslahi ya watu wachache, akiomba uchaguzi huo urejewe upya kwa sababu umekosa sifa.


"Nimepokea matokeo ya uchaguzi kwa masikitiko makubwa  sifa moja wapo ya kugombea nafasi ya uongozi ilikuwa ni lazima mgombea awe mmiliki wa mgodi na mwanachana wa chama cha  wachimbaji wa madini Mererani (MAREMA) lakini cha ajabu waliochaguliwa wengi wao sio wamiliki wa migodi na hawakuwa na sifa ,naiomba serikali iingilie kati kwani kamati iliyochaguliwa haitakuwa na afya badala yake itakuwa chanzo  cha migogoro kutokoma"alisema


Lema ambaye ni mmiliki wa mgodi kitalu B,alienda mbali zaidi kwa kumtuhumu mchimbaji mwenzake , Japhet Lema(NYAKE) kuingia chumba cha kuhesabia kura wakati sio mhusika na kugawa asali wakati  zoezi la kujesabu likiendelea.


"Tatizo kubwa lililotokea siku ya leo katika uchaguzi kuna mmiliki mwenzetu wa mgodi anaitwa Njake alinifuata akaniambia mimi sitakuwa mjumbe wa kamati hii akamtaja na mjumbe mwingine Abdalah Ngoma akamtaja na mjumbe mwingine wa block C akasema yeye ni Njokaa wa Onee wa Franone hivyo hamtapita na kweli imetokea hivyo kupitia kauri hiyo naamini kwamba alijipanga kutuangusha"


"Wakati wa zoezi la kuhesabu kura Mwenyekiti wa Marema  Tawi ,alimchukua huyu mzee Njake na kumwingiza kwenye chumba cha kuhesabia kura kwa ushahidi na baadaye baada ya kuhesabiwa kura mimi na NICK KIKUYU imeonekana hatujashinda na Abdala Ngoma yeye jina lake halikuwepo kabisa"


Alisema katika uchaguzi huo waliochaguliwa kuanzia ngazi ya mwenyekiti na katibu ni watu wa karibu na Mzee NJAKE akiwemo aliyekuwa meneja wake wa Mgodi.


Naye Fatuma Mushi(Mama Kikuyu)mmiliki wa Mgodi ,alisema kuwa uchaguzi huo umevurugwa na ofisa mkazi wa Madini ,Mererani (RMO), Nchagwa Marwa kwa kuruhusu wafanyabiashara  'kubaka' uchaguzi kwa kulambisha watu asali.


"Rmo amekata majina ya wagombea na kuweka majina yake ya mfukoni kupitia shinikizo la Njake na Njake anataka kuunda kamati yake ili kupambana na mmoja ya wafanyabiashara wa madini aliyemtaja kwa jina moja la Saitoti"


"Pia kijana wangu anaitwa NICKY KIKUYU jina lake limeondolewa kwa sababu wanadai hatakiwi ni Nyokaa na kibaraka wa Onee"


Kwa upande wake Japhet Lema (Njake)alipohojiwa juu ya tuhuma hizo alikana kuingilia uchaguzi huo katika chumba cha kura akidai kwamba yeye aliitwa na RMO kutoa mchango wa fedha ili kufanikisha shughuli za uchaguzi huo.


"Mimi sijaingia kwenye kura na fungu la fedha kurubuni wajumbe kama inavudaiwa ila mimi niliitwa na RMO hapo nje akiomba mchango wa kulipia mahema (tents) na hakuna meneja wangu niliyemwingiza achaguliwe"


Naye  ofisa Mkazi wa Madini RMO,Marwa ambaye alikuwa msimamizi wa uchaguzi huo alisema uchaguzi huo ulifanyika kwa uhuru na haki na hakuna vitendo vya rushwa na hao wanaolalamika ni wale walioshindwa katika kinyang’anyiro hicho. 


Marwa aliwataja waliochaguliwa kuunda kamati hiyo kuwa ni,Charles Chilala Mwenyekiti wa kamati, Zephaniah  Mungaya Makamu Mwenyekiti, Abubakari Madiwa Katibu na Agripina Kasian Naibu Katibu pamoja na wajumbe.


Awali kabla ya zoezi la uchaguzi kuanza  baadhi ya wajumbe wasio na kadi za uanachama wa Marema walizuiwa kushiriki uchaguzi huo wakitakiwa kulipia sh,elfu kumi, lakini  Mwenyekiti wa Marema Mkoa wa Manyara, Justine Nyari  aliingilia kati na kuamuru mchimbaji yeyote mwenye leseni aruhusiwe kupiga kura .

NB ,Picha na Mtandao

Ends..








Post a Comment

0 Comments