Na Joseph Ngilisho ARUSHA
KITUO cha Demokrasia Tanzania (TCD) kupitia mradi wa kusaidia wanawake kushiriki mchakato wa uchaguzi nchini ,kimeanza kuwawezesha wanawake kielimu, kuzitambua sheria za uchaguzi ili washiriki kikamilifu uchaguzi ujao wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani 2025
Hayo yamebainishwa na Afisa Programu wa TCD, Likele Shungu wakati wa semina ya kuwanoa wanawake kutoka vyama vitano vya siasa iliyofanyika jijini Arusha na kushirikisha vyama vya CCM, CHADEMA, ACT-WAZALENDO, NCCR-MAGEUZI na CUF kutoka wilayani ARUMERU .
Shungu alisema ,hatua hiyo imekuja kufuatia idadi ndogo ya wanawake kujitokeza na kushiriki chaguzi mbalimbali na hivyo TCD kupitia Programu yao inayofadhiliwa na ubalozi wa Ayalend nchini Tanzania wameona umuhimu wa kuwawezesha wanawake kuzijua sheria na kanuni za uchaguzi ikiwa ni njia mojawapo ya kuwawezesha kushiriki chaguzi zijazo.
"Tumewakutanisha wanawake viongozi kutoka vyama vya siasa wilaya ya Arumeru ili kuwapatia ufahamu juu ya sheria za uchaguzi zilizopitisha na tume huru ya uchaguzi mwaka huu 2024 ,pamoja na kanuni za uchaguzi wa serikali za mtaa ili wazijue na kuweza kuhamasisha na wenzao kushiriki uchaguzi ujao"
Alisema takwimu zinaonesha ushiriki mdogo wa wanawake katika chaguzi mbalimbali kiasi cha kuwa chini ya asilimia 9 na wengi wa wanawake waliopo madarakani kupitia vyama vya siasa wametokana na mgongo wa uteuzi wa viti maalum .
Alisema tangia wameanza semina hizo nchini kumekuwa na mwitikio mkubwa kwa wanawake wengi kuhamasika kushiriki uchaguzi ujao na walishukuru kituo hicho cha Demokrasia Tanzania kwa kuwafumbua macho kwani wengi wao walikuwa gizani hawajui hata mabadiliko ya sheria za uchaguzi zikoje.
Naye Mwl.Deus Kibamba mchambuzi wa masuala ya kisiasa ,ambaye alikuwa mtoa mada katika semina hiyo,alisema kumekuwepo na changamoto za uteuzi nafasi za wanawake katika vyama vya siasa ndio maana vifungu vya sheria vilivyopitishwa kwa sasa vinataka vyama vya siasa lazima viwe na sera ya jinsia na ujumuishi.
"Katika mjadala unaoendelea hivi sasa kumekuwepo na shida katika uteuzi wa wanawake ndani ya vyama vya siasa , ndio maana vifungu vya sheria vilivyopitishwa mwaka huu 2024, vinapigania wanawake wawe na haki sawa ya kuteuliwa ndani ya vyama vya siasa na katika nafasi za kitaifa"
Alisema katika mjadala huo wanawake wamehamasika sana kutokana na mabadiliko ya sheria hiyo ambayo imeleta fursa katika ushiriki wao katika kugombea nafasi mbalimbali pamoja na uteuzi.
Mmoja ya washiriki wa semina hiyo Gladness Laizer kutoka chama Cha NCCR-MAGEUZI alipongeza mabadiliko hayo ya vifungu vya sheria na kuongeza kuwa, mabadiliko hayo yatavuta idadi kubwa ya wanawake kushiriki fursa za chaguzi mbalimbali.
"Kwakweli sisi wanawake hususani vijana tumefurahia mabadiliko ya sheria ambayo yameleta hamasa kubwa tofauti na hapo awali ambapo wengi wetu tuliongopa kugombea kutokana na mfumo dume uliokuwepo wa kuona mwanamke hastahili kugombea nafasi yoyote ya uongozi"
Ends....
0 Comments