HISTORIA imeandikwa leo kupitia tukio la leo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kufanya uzinduzi wa Reli ya SGR.
Tukio hili ni uthibitisho kwamba Watanzania wamethubutu na wameweza. Kwa hakika nchi yetu instahili pongezi kwa kuonesha mfano kwamba inawezekana kwa nchi ya Afrika kujenga miundombinu ya Reli ya SGR pasipo kutegemea nchi nyingine.
Mara ya mwisho nchi yetu ilivyotekeleza mradi mkubwa wa Reli ya TAZARA, tulisaidiwa mkopo kutoka kwa rafiki zetu wa China. Vivyo hivyo nchi nyingi za Afrika zilizojenga reli za SGR katika miaka ya karibuni wakiwemo jirani zetu wa Kenya- walipata mkopo kutoka China.
Mradi huu wa SGR ya Tanzania ulisanifiwa na kujengwa (designed & built) kwa viwango vya a juu zaidi (kwa maana ya uwezo wa kuhimili mizigo inayopitishwa kwenye reli (Axle load of rolling stock).
Wakati reli za SGR zilizojengwa katika nchi zote za Afrika uwezo wake ni Axle load kati ya tani 21-23; SGR ya Tanzania Axle load yake ni tani 35 (yaani ina uwezo wa kubeba mizigo mizito zaidi.
SOMA: Rais Samia azindua safari za SGR
Wataalam wengi wa nje waliona uamuzi ule wa kujenga kiwango cha Axle load 35 ni wa kupoteza pesa kwasababu hatuna mizigo mingi ya kuhitaji uwekezaji mkubwa wa aina ile.
Lakini Serikali iliamua kuendelea na viwango hivyo kwasababu ya kuona mbali— uwekezaji huu utadumu kwa miaka mingi-na utaiwezesha nchi yetu kutumia nafasi yake kijiografia kuvutia mizigo kutoka nchi za jirani kutumia bandari zetu. Hivyo uamuzi wa kuwa na miundombinu ya reli yenye uwezo mkubwa ni sahihi kwa mtu anayeangalia mbali.
Ni uamuzi huo wa kujenga reli ya kiwango hicho cha juu ulioyafanya kampuni za Ujenzi wa Reli ya China yasiombe zabuni ya ujenzi wa Reli ya SGR awamu ya kwanza ya Dar-Morogoro– kwani yalifahamu – Tanzania haiwezi kupatiwa mkopo kutoka China kwa ajili ya ujenzi wa Reli ya SGR kwa sababu kiwango cha Axle load 35 tulichochagua-ni tofuati na vigezo vilivyokuwepo vya Mikopo ya China inatolewa kujenga Reli yenye kiwango cha Axle load kati ya 21-23.
Mchakato wa kutafuta fedha za ujenzi wa reli haukuwa rahisi. Serikali ilifanya mazungumzo na nchi mbalimbali na taasisi za fedha kimataifa.
Majibu yalikuwa ya kukatisha tamaa. Wengi waliona hakuna tija kujenga reli ya SGR. Na wengine walisema ni hasara kujenga Reli ya SGR kwani uchumi wa Tanzania hauwezi kuzalisha mzigo wa kutosha. Wengine walishauri Tanzania ikarabati reli ya zamani iliyojengwa kipindi cha ukoloni- inatutosha.
Pamoja na maneno mengi ya kukatishwa tamaa, sambamba baadhi ya ahadi hewa za kufikiria kutusaidia kujenga ujenzi wa reli hiyo, serikali haikukata tamaa kwani uzoefu wa nyuma ulionesha kwamba hata wakati wa kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa Reli ya TAZARA maneno ya kuvunja moyo na kukatishwa tamaa kwamba haiwezekani kujenga reli yalikuwepo.
Hivyo Serikali ilikaza moyo na kuthubutu kuanza ujenzi wa mradi wa Tanzania SGR. Ni furaha kubwa kwamba leo tunashuhudia uzinduzi wa kipande cha Dar–Dodoma. Simulizi ya Historia ya ujenzi wa SGR ya Tanzania hainabudi kuwatambua kwa uzito wa kipekee viongozi wetu wawili.
Wa kwanza ni Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli – aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Moyo wake wa ujasili na uthubutu ndio ulipelekea nchi yetu kuanza kujenga SGR (kutoka kwenye maneno na makaratasi hadi kujenga reli halisi).
Aliziba masikio ya waliokuwa wanasema “haiwezekani kujenga SGR bila ya msaada wa Taifa kubwa”. Alijiaminisha na kutuaminisha kwamba Reli itajengwa iwe jua, iwe mvua, haturudi nyuma. Na kweli alianza kuijenga.
Kiongozi wa pili ambaye mchango wake mkubwa utakumbukwa katika historia ya SGR ni Dkt Samia Suluhu Hassan. Kwanza akiwa Makamu wa Rais, yeye ndiye alikuwa kwenye “front line” ya kutafuta fedha sa ujenzi nje ya nchi.
Kipindi kile ambacho Hayati Rais Magufuli alikuwa hafanyi safari za nje ya nchi, Mama Samia ndiye aliyekuwa akienda nie kuzungumza na viongozi mbalimbali duniani kutafuta ufadhili wa kujenga SGR.
Kazi hiyo aliifanya kwa ufanisi mkubwa chini ya usaidizi wa karibu wa aliyekuwa Waziri wa Fedha kipindi hicho Mhe. Dkt. Philip Mpango na Waziri wa Mambo ya Nje Hayati Dkt. Augustine Mahiga. Fedha iliyopatikana kuanza ujenzi wa SGR- ilitokana na kazi nzuri aliyoifanya Mama Samia – nje ya nchi.
Hayati Dkt Magufuli alipotangulia mbele ya haki ujenzi wa mradi wa SGR ulikuwa bado unaendelea. kipindi hicho kilikuwa kigumu katika uchumi wa dunia kutokana na janga la UVIKO19.
Pamoja na changamoto hizo Mheshimiwa Rais Samia alipoingia madarakani Mwezi Machi 2021 alithubutu na kuweza kuendeleza ujenzi wa mradi wa SGR hadi kuukamilisha katika kipindi kigumu cha uchumi duniani. Kwa hakika msemo wake mashuhuru ya “Kazi Iendelee” unaoneka kiuhalisia kwenye mradi huu.
Rais Samia hakuishia kukamilisha vipande vya reli vilivyokuwa vimeanza kujengwa, bali alianzisha ujenzi wa vipande vipya ambavyo ujenzi wake unaendelea.
Katika makala hii ninapenda pia kutambua baadhi ya watumishi waliokuwa na mchango muhimu katika kusaidia viongozi wetu kufanikisha safari ya ujenzi wa SGR- miongoni mwao yupo Prof. Makame Mbarawa, Dkt.Leonard Chamuriho; Ndugu Masanja Kadogosa na Marehemu Patrick Mfugale. Hawa na wengine ambao sikuwataja, walifanya kazi usiku na mchana kufanikisha mradi huu.
Kwa hakika kazi kubwa imefanyika na kazi kubwa bado ipo mbele yetu. Watanzania sote tushikamane tuunge mkono jitihada zinazofanyika chini ya Uongozi wa Dkt Samia Suluhu Hassan, kutekeleza sehemu iliyobaki ya mradi wa SGR. Kwa hakika- tumeweza, tunaweza na tutaweza.
Imeandikwa na Mbelwa Kairuki, Balozi wa Tanzania nchini Uingereza
0 Comments