MKURUGENZI MPYA JIJI LA ARUSHA AJA NA KAZI YA 5G+,ASIMAMISHA WATUMISHI WAZITO WAZEMBE

 Joseph Ngilisho ARUSHA

                                  

Mkurugenzi Mpya wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, John Kayombo amewasimamisha kazi watumishi wanne wa kituo cha afya Kaloleni ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili za uzembe kazini kwa kushindwa kuhudumia majeruhi.


Watumishi hao ambao ni Madaktari wawili na Wauguzi wawili wamesimamishwa kazi jana kufuatia kuonekana kwa taarifa kupitia mitandao ya kijamii ikiwatuhumu kuchelewa kutoa huduma kwa majeruhi wa ajali ya bodaboda Baraka Mudadu (21) Mkazi wa Mianzini.


‘Taarifa ya awali inaonyesha majeruhi huyo alipokelewa kituoni hapo Agost 21, 2024 saa 4 asubuhi na kupatiwa huduna ya dharura ikiwemo kushonwa na kufungwa majereha ya kichwani yaliyokuwa yakitoka damu” Alisema Kayombo;


 


“Baada ya hapo inaonekana alipewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Rufaa Mount Meru kwa ajili ya matibabu zaidi” Alisema Mkurugenzi huyo.


 


Pamoja na mgonjwa kupewa rufaa hiyo, Kayombo amesema kuwa walalamikaji walionyesha kutoridhishwa kutokana na kuchelewa kupatikana gari la wagonjwa na hivyo kuamua kumpeleka mgonjwa wao Hospitali ya Rufaa kwa kutumia machela ya kituoni hapo (stretcher) kinyume na utaratibu.


“Kutokana na hilo, nimeunda timu ya ufuatiliaji wa tuhuma hizo ikiwa na wajumbe kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha na Halmashauri ya Jiji la Arusha na imeanza kazi Agosti 22, 2024 na taarifa ya uchunguzi huo itatolewa utakapokamilika” amesema Kayombo.


Pia ametumia nafasi hiyo kuwaagiza watoa huduma wote na watumishi kwa ujumla kutoa huduma kwa wananchi kwa kufuata miongozo, weledi, maadili ya kitaaluma pamoja na sheria taratibu na kanuni.



Awali ilisambaa video mitandaoni ikiwaonyesha baadhi ya wakazi wa Arusha wakiwa wanakokota machela ya Kituo cha Kaloleni yenye mgonjwa juu hadi hospitali ya Rufaa ya Mount Meru iliyoko zaidi ya mita 2000 kutoka kituo hicho cha afya.


 


Wakizungumza kwenye video hiyo walisema kuwa wamefikia hatua hiyo baada ya kuona mgonjwa wao anacheleweshewa huduma za kitabibu katika hospitali ya Rufaa Mount Meru anakotakiwa kwenda kwa madai kuwa gari la wagonjwa halina mafuta.


 


Steven Mesiaki alisema kuwa rafiki yake amepata ajali asubuhi ya Agost 21 ,2024 na kuwahishwa katika kituo hicho cha afya Kaloleni na kubainika kuwa na majeraha makubwa kichwani hivyo kupatiwa huduma ya awali na kesho yake kuandikiwa rufaa katika Hospitali ya Mout Meru.


 


“Tangu asubuhi wanajizungusha hawataki kumpeleka na tulipouliza wanasema gari halina mafuta lakini hawataki kunyoosha kuwa wanataka hela ya mafuta bali wanatuzungusha ili tutoe rushwa”;


 


“ Na sisi tumegoma kujiongeza na kutoa hela hiyo tukaamua kuchukua machela yao na kumkokota hadi hapa hospitalini na tunashukuru Mungu tumemfikisha salama na kwa wakati na tumepokelewa haraka”alisema Mesiaki.


Ends....


Post a Comment

0 Comments