Wananchi Kanda ya Kaskazini wamehimizwa kutumia fursa ya Maonesho ya Wakulima na Sherehe za Maonesho ya Nanenane yanayofanyika Njiro Jijini Arusha, kujifunza teknolojia za kisasa kwa ajili ya kilimo, ufugaji na uvuvi na kuzitumia ili kuendeleza dhana ya Uchumi Mahalia.
Kauli hiyo, imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu wakati akifungua Maonesho hayo ya Nanenane Kanda ya Kaskazini, yanayoendelea kwenye viwanja vya Themi - Njiro, mkoani Arusha.
Babu amewasisitiza viongozi, waandaaji na watalamu wa Kilimo na Mifugo, kuwahamasisha wananchi husuasni wakulima na wafugaji kujitokeza kwa wingi kwenye maonesho hayo, ili kujifunza mbinu za kisasa za kilimo na ufugaji bora, unaoendana na mabadiliko ya kiteknolojia sambamba na mabadiliko ya tabia nchi.
"Niwaombe viongozi mlioko hapa tumieni fursa hii kuwaleta wafugaji na wakulima kutoka maeneo yenu kwa wingi ili waweze kujifunza teknolojia mbalimbali na hatimaye kuzitumia katika maeneo yao ili kuendeleza dhana ya Uchumi Mahalia (Local Economic Development)". Alisisitiza Babu.
Aidha, aliwasisitiza wananchi kuendelea kujikita na kuwekeza kwenye kilimo ambacho ndio uti wa mgongo wa Taifa, ambapo 90% ya wananchi kanda ya Kaskazini hukishughulisha na Kilimo, kwa kuwa Serikali chini ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeweka nguvu kubwa katika kuboresha sekta ya kilimo
Alisema kwa mwaka 2023/2024, mikoa ya Kanda hiyo, imenufaika katika utoaji wa mbolea za ruzuku, uboreshwaji wa miundombinu ya umwagiliaji na kupunguza utegemezi wa mvua katika kukuza mazao, uanzishwaji wa mashamba darasa ya malisho,uendelezaji wa viwanda vya usindikaji wa mazao ya mifugo, ujenzi wa majosho na usambazaji wa madawa ya kuogesha mifugo pamoja ugawaji wavitendea kazi kama pikipiki kwa maafisa ugani.
Hata hivyo, Mkuu huyo wa mkoa aliagiza kufanyika tathmini baada ya maonesho hayo ili kupata picha halisi na kujibu baadhi ya maswali kadha wakadha ikiwemo kufahamu kwa undani mafunzo hayo, teknolojia ipi au zana zipi zimekuwa na mvuto kwa wananchi waliotembelea maonesho ili ziweze kutumika kusambazwa kwa wingi katika halmashauri.
Maonesho ya 30 ya Kilimo na Sherehe za Nane Nane Kanda ya Kaskazini yanaendelea mkoani Arusha, kwenye Viwanja vya Themi Njiro yakijumuisha mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara, Kilele kikiwa tarehe 08.08.2024, yamebeba Kauli mbiu ya "Chagua viongozi bora wa Serikali za Mitaa kwa Maendeleo endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi"
Awali Katibu Tawala mkoa wa Arusha Mussa Miseile alieleza namna mikoa ya kanda ya kaskazini ulivyoshiriki maandalizi ya maonesho hayo ikiwemo kuboresha miondo mbinu katika na kufanya yaonekane yakufana yenye ubora wa hali ya kuvutia.
Alisema maonesho ya mwaka huu katika viwanja vya Themi ni kielelezo tosha kuwa kanda ya kaskazini ulimejipanga ipasavyo kuhakikisha yanawanufaisha wakulima na wafugaji wa mikoa yote ya kanda hii na mikoa ya jirani.
Ends.....
0 Comments