KIGOGO WA POLISI ARUSHA MATATANI KWA KUMVUNJA MGUU MTUHUMIWA AKIMLAZIMISHA KUKIRI MAKOSA,RPC AANZA KUMCHUNGUZA KIBARUA CHAKE MIKONONI MWA IGP

 By Ngilisho Tv-ARUSHA 


Jeshi la polisi Mkoa wa Arusha limeanza uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili Askari wake Omari Mahita anayedaiwa kumpiga hadi  kumvunja mguu mtuhumiwa wakati wa mahojiano.

Mahita ambaye hivi karibuni amehamishiwa kikazi jijini Arusha kama mkuu wa upelelezi wa wilaya (OC CID ),akichukua nafasi ya Gwakisa Minga ambaye hivi karibuni aliondoshwa ghafla,anatuhumiwa kutenda unyama huo kwa kumkanyaga na miguu yake ,mtuhumiwa akiwa amelala kifudifudi.



Mahita ambaye ni mtoto wa IGP Omari Mahita (mstaafu), anatuhumiwa kumvunja mguu wa kushoto Peter Charles (21) Mkazi wa kata ya daraja II, jijini Arusha akiwa katika chumba cha mahojiano June 6, 2024 akimlazimisha kusema.ukweli wa tuhuma zinazomkabili.  


Alipohojiwa kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Arusha SACP Justine Masejo alisema polisi wanafanyia kazi tuhuma hizo na tayari wameanza uchunguzi wa tukio hilo, na endapo ikibainika kosa kutendeka wahusika watachukuliwa hatua za kisheria.

"Ni kweli hilo tukio liko ofisini kwangu na tumeanza uchunguzi nalo tangu Agost 8, 2024 nilipopata taarifa kwa kwa njia ya simu kutoka kwa ndugu wa huyo kijana akimtuhumu askari wangu kumpiga hadi kumvunja mguu” alisema Masejo na Kuongeza;

“⁸Baada ya taarifa hizo niliwaita na kuwakutanisha na mtuhumiwa kumtambua na kutoa malalamiko yake kwangu na tukaanza kwa kufungua jalada na bado upelelezi unaendelea kwa mujibu wa Sheria maana hakuna aliye juu ya Sheria” 

Alisema kuwa upelelezi ukikamilika wanatarajia kumchukulia hatua Askari huyo endapo itabainika alitenda kosa hilo la uvunjifu wa sheria kwa kujichukulia sheria mkononi hadi kujeruhi.

Akizungumzia tukio hilo, kijana Peter Charles (21) alisema kuwa siku ya Tukio Mei29,2024 majira ya saa 1.20 usiku wakiwa nyumbani kwa mmoja wa rafiki yao kata ya daraja II, wakiwa wanatizama sinema kwenye luninga, walikuja askari watatu na kugonga mlango kisha kujitambulisha na kuwataka kutoka nje na kuwapakia kwenye gari walilokuja nalo.

“Walituchukua hadi kituo cha polisi cha kati bila kutuambia kosa letu, kwa madai kuwa tutajua huko huko kituoni” 

Alisema kuwa walikaa kituoni siku tatu bila kusemeshwa kabla ya siku ya nne kuitwa katika chumba cha mahojiano na kuhojiwa kwa nini wanacheza kamari mitaani.

“Tulikataa kuwa hatuchezi kamari lakini hawakutaka kutuamini zaidi ya kutupiga kwa marungu kwenye magoti, mgongoni na kiunoni wakidai kukubali kwetu ndio msamaha wetu, hata hivyo tuliendelea kukataa na kurudishwa rumande tukiwa na maumivu makali sana”

 
Alisema kuwa siku ya saba tena waliitwa na kuanza kushushiwa kipigo kama vilevile awali na askari wawili mmoja akimtaja kwa jina la Mahita, na baadae akawaamuru kulala kwa tumbo na kumkanyanga mguu wa kushoto kwa kumpandia hadi mguu kuvunjika.


“Wakati ananikanyaga, mfupa wa mguu ndio ukavunjika kwa kutoa mlio mithili ya kuni iliyovunjwa na damu kuanza kutoka mfululizo, ndio akaamuru tunyanyuke na kuuliza hizo damu za nani na nilipojibu ni mimi na wenzangu nao walikuwa na michubuko akaturuhusu tukanawe bombani turudi mahabusu” amesema Peter.

Alisema kuwa damu ziliendeleq kuvuja usiku kucha hadi kutapakaa chumba kizima, na kwa maumivu yale alipata joto kali sana akiwa mahabusu, kabla ya mmoja wa askari asubuhi kuona hali ile na kumletea dawa za kukata damu na maumivu.

“Pamoja na hizo dawa hazikusaidia, hivyo walileta chumvi nyingi na kumwagia kwenye kidonda changu wakaondoka. Hali ilizidi kuwa mbaya ikabidi nivue shati langu kujifunga kidonda, na baadae saa nne alikuja askari Mahita tena na kuuliza unaendeleaje nikamwambia nimevunjika naomba msaada wa kwenda hospitali, lakini akasema bado hujavunjika, ntakuvunja zaidi nitenganishe na hizo nyama, akaondoka”.

 

Pater alisema kuwa jioni ya siku hiyo ya nane june 5,2024 waliletwa vijana wengine wanne mahabusu, kabla ya kesho yake siku ya tisa kuitwa kwa pamoja chumba cha mahojiano na kusomewa shtaka linalowakabili wote saba kuwa ni wizi wa kutumia silaha huku wakirudishwa  mahabusu kwa ajili ya maandalizi ya jalada letu tupelekwe mahakamani.

“Tulibaki tunashangaa sisi watatu, inakuwaje tunageuziwa shtaka, tulibaki na wenzangu kuuliza, Yule askari Mahita akaitwa tukaachwa nae, akaanza kutuambia kuwa kwa sababu tumekataa kosa la kamari basi tutakwenda jela kupambana na kesi ya Wizi wa kutumia silaha, tena akawa anasema hana msaada na kidonda changu nitapelekwa jela nikaponee huko” amesema Pater.

Amesema kuwa alikata tamaa ya kuishi na kutaka kujidhuru kutokana na maumivu aliyokuwa anapata.

“Siku baada ya siku kweli tukachukuliwa tukapelekwa mahakamani na kusomewa shtaka la kucheza kamari sisi watatu baada ya wale wanne kuja kuachiwa, na baada ya hapo tulidhaminiwa ndio nikapelekwa hospitali na kupata matibabu haya” alisema Peter.

Mjomba wa Peter, ambae hakutaka kutajwa jina lake, amesema kuwa baada ya kijana wao kukamatwa walikuja kugundua baada ya siku tatu na walipofuatilia walinyimwa dhamana na kuamua kupiga simu kwa ofisi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) na kutakiwa kutuma RB namba kabla ya kuambiwa dhamana iko wazi hivyo asubiri swala lake linashughulikiwa.

 

“Baadae alinipigia nirudi kituoni kumdhamini mtu wangu, lakini nilipokwenda ijumaa nikaambiwa nirudi jumatatu atapelekwa mahakamani kwa sababu kosa lake halidhaminiki bali ni Rb namba ilikosewa kuandikwa kosa la kamari lakini ni wizi wa kutumia silaha”;

“Nilibaki nashangaa, nikaomba hata kumuona lakini hawataki kabisa hadi jumatatu nikarudi tena lakini wakasema jalada bado hadi jumatano ndio wakamfikisha mahakamani na kufanikiwa kumdhamini” amesema Mjomba huyo.


Amesema kuwa baada ya kutoka walirudi polisi kusaka PF3 ya kijana kutibiwa wakakataa kumpa wakasema hiyo ni kesi nyingine na kumtaka kumpeleka hospitali kumtibu mwenyewe na kuahidi kurudisha gharama.

“Ilibidi nimpeleke kituo cha Afya Olorien tudanganye ameanguka akasafishwa na katika uchunguzi wa X-Ray alibainika amevunjika vibaya hivyo nikatakiwa kwenda hospitali ya Seliani nikiwa na PF3 kwa daktari aliyepigiwa na nikaelekezwa kwake tena nikapewa namba yake”

“Kutokana na daktari kusisitiza niende na Pf3, kesho yake ilibidi twende tudanyange katika kituo cha Polisi Kijenge kuwa ameumizwa na rafiki yake hivyo nipewe namba ya kumtibu kabla ya kurudi kufungua jalada ambapo walikubali na kunipatia ndio ikawa msaada wa matibabu kwa kijana wetu”

Alisema, baada ya kulazwa kwa siku tatu kwa matibabu na kuruhusiwa kurudi nyumbani akiwa na vyuma na dawa alizopewa, waliamua kulifikisha swala hilo kwa jeshi la polisi ili kuona namna wanaweza kupata msaada wa matibabu lakini pia watuhumiwa wachukuliwe hatua za kisheria kuwa fundisho kwa wengine.

 Ends....

Post a Comment

0 Comments