By Ngilisho Tv -MOSHI
Mamlaka ya udhibiti wa huduma za nishati na maji (Ewura) Kanda ya kaskazini, imewaonya wafanyabiashara wa gesi ya kupiki kuacha tabia ya uchakachuaji na kuhakikisha wanakuwa na mizani, ili kuweza kuhakiki uzito wa gesi kabla ya kuuza.
Rai hiyo imetolewa na meneja wa Ewura Kanda ya Kaskazini, Lorivii Long’idu wakati wa kikao na wadau wa gesi ya kupikia katika Mkoa wa Kilimanjaro, iliyofanyika mjini Moshi na kuwakutanisha wadau mbalimbali ikiwemo wafanyabiashara wa bidhaa hiyo.
Amesema kumekuwepo na changamoto ya uchakachuaji wa gesi za kupikia ambao unafanywa na wafanyabiashara wasio waaminifu na kusema watakaobainika kuuza gesi zenye uzito pungufu, watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Amesema matumizi ya gesi ya kupikia yameendelea kuongezeka nchini mwaka hadi mwaka ambapo mwaka 2010 nchi ilikuwa inaagiza tani 10,000 kwa mwaka mzima lakini mpaka kufikia mwaka jana 2023, imeagizwa tani 250,000, hivyo ni vyema wafanyabiashara wakatumia fursa hiyo kupanua biashara zao na kuepuka wizi na uchakachuaji.
“Uchakachuaji kwenye gesi ya kupikia majumbani umekuwa kwenye namna tofauti na ule uchakachuaji ambao upo kwenye mafuta ambapo tunasema mafuta yale yanawekwa na kimiminika kingine ambacho ni cha gharama nafuu ili kupata faida isiyo halali” amesema Long’idu
Ameongeza kuwa “Lakini uchakachuaji ambao tunauona sana kwenye gesi ya kupikia ni wananchi kuuziwa mitungi ambayo uzito ni pungufu, baadhi ya wafanyabiashara sio waaminifu, wengine wanatumia kupikia ikishapungua wanarudi kuiuza, niwaonye wafanyabiashara, kuacha tabia hiyo kwani kufanya hivyo ni kinyume cha taratibu na sheria, tunaendelea na ufuatiliaji, watakaobainika hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao “
Aidha amewataka pia wananchi wanapokwenda kununua gesi, kuhakikisha muuzaji ana mizani na anaipima ili kuhakikisha hakuna uchakachuaji.
Amesema mbali na hilo, wameendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhamasisha matumizi sahihi ya gesi, ili kuepuka majanga ya moto yatokanayo na gesi majumbani.
Afisa vipimo kutoka ofisi ya wakala wa vipimo (WMA) Mkoa wa Kilimanjaro, Yudatade Peter amesema moja ya majukumu yao ni kusimamia usahihi wa vipimo katika mitungi ya gesi.
“Kama mtu ananunua mtungi wa gesi wa kilo sita, ahakikishiwe pale kwenye mzani kwamba imesoma kilo sita ili kupata thamani ya Ile fedha yake na wale ambao tunawakuta wamekiuka sheria wakati wa ukaguzi wetu, sheria inafuata mkondo wake”
Jackline Shayo mkazi wa Soweto Manispaa ya Moshi, mtumiaji wa gesi ya kupikia amesema elimu zaidi inahitajika katika jamii ili kuhamasisha matumizi ya gesi ya kupikia kama nishati safi ikiwa ni pamoja na kujenga uelewa wa matumizi ya mizani kwa wafanyabiashara.
0 Comments