Na Joseph Ngilisho ARUSHA
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA),imekuja na mpango wezeshi kwa wafanyabiashara kuwekeza vituo vya mafuta kwa gharama nafuu katika maeneo ya pembazoni na vijijini ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo na kuondoa hatari ya kuuza mafuta kiholela.
Akiongea na vyombo vya Habari katika viwanja vya maonesho ya nanenane Njiro, Arusha, Meneja wa EWURA kanda ya Kaskazini, Lorivii Long'idu alisema EWURA imewataka wafanyabiashara kujenga vituo vya mafuta kwa gharama nafuu na kwa njia salama ili kuwarahisishia wamiliki wa vyombo vya moto wakiwemo bodaboda kupata huduma hiyo kwa njia salama isiyo hatarishi.
"Tupo hapa katika maonesho ya Nanenane kutoa elimu kwa umma juu ya utaratibu wetu mpya wa kuwezesha wafanyabiashara kutoa huduma ya mafuta kwa njia salama kwa kurahisisha utoaji wa vibali vya ujenzi katika maeneo ya pembezoni na vijijini "
Alisema kumekuwepo na utaratibu wa uuzaji wa mafuta kwa njia ya chupa na madumu unaotokana na ongezezo la uhitaji wa vyombo vya moto zikiwemo bodaboda ambazo zimekuwa zikitoa huduma ya usafiri maeneo ya pembezoni na vijijjni ambako vituo vya mafuta havijajengwa.
"Serikali ya awamu ya sita kupitia wakala wa nishati vijijini imekuja na utaratibu kukopesha ama kuwezesha ujenzi wa vituo vya mafuta kwa gharama nafuu vijijini na maeneo ya pembezoni"Alisema.
"Sisi kama Ewura baada ya kuliona hilo tumejaribu kurahisisha taratibu za upatikanaji wa leseni za ujenzi wa gharama nafuu.Niwaombe wananchi na wafanyabiashara watakayoina fursa hii ya kuwekeza vituo vya mafuta vya gharama nafuu wafike Ewura kupatiwa elimu hiyo"
Alisisitiza kuwa ujenzi wa vituo vya mafuta wa gharama nafuu ni kuanzia kiasi cha sh,milioni 55 hadi 70 na kiasi hicho cha fedha unaweza kukipata kwa mkopo kupitia Wakala wa nishati vijijini REA kwa njia ya Mkopo.
Meneja alisema kuwa ujenzi wa vituo vya mjini ni mgumu kidogo kwa kuwa utakulazimu uwe na hati ya umiliki wa Ardhi lakini kijijini unachohitaji kuwa nacho ni muhtasari wa kijiji unaoonesha umeruhusiwa ujenzi wa kituo cha mafuta na kibali cha mazingira wa eneo husika .
"Kwa kuona umuhimu wa watu kuwekeza vituo vya mafuta vijijini tumeamua kupunguza gharama za maombi ya ujenzi wa vituo cha mafuta vya gharama nafuu, ambapo vijijini utalipia sh, 50, 000 tu tofauti na mijini gharama za kupata kibali ni sh, 500,000"
Alitoa rai kwa wafanyabiashara kuchangamkia fursa hiyo inayolenga kuondoa uuzwaji wa mafuta kiholela na kuhatarisha maisha ya watu kutokana na tabia ya kulaza madumu ya mafuta ndani ya nyumba zao za kuishi.
Ends..
0 Comments