WAUMINI WA DINI YA KIISLAMU NA BAKWATA ARUSHA KUTOANA ROHO NI MGOGORO WA KUGOMBEA ENEO LILILOPO MSIKITI WA BONDENI

 Na Joseph Ngilisho ARUSHA 


Waumini wa msikiti Mkuu wa Ijumaa maarufu kama 'Msikiti wa Bongeni' ulioko Mkoani Arusha  wameingia katika Mgogoro mkubwa na Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata baada ya kutofautiana katika uendelezaji wa eneo la msikiti huo.


Waumini hao wa Umoja wa Waislamu Mkoani Arusha (AMU) wameingia katika Mgogoro na Bakwata baada ya kutaka eneo la wazi lililosalia pembezoni mwa msikiti huo kujengwe Msikiti mwingine mkubwa wa kisasa itakayokuwa alama kubwa ya dini yao Afrika Mashariki lakini Bakwata wao wakihitaji kujenga vibanda vya biashara kibabe.


Eneo hilo la Msikiti wa bondeni uliopo ndani ya kiwanja namba 478, Kitalu H na I, linalomilikiwa AMU tangu mwaka 1964, mbali na Jengo la Msikiti lakini pia lina jengo la ghorofa nne la shule ya Sekondari ya Bondeni, pamoja na maduka kwa upande wa chini.


Aidha Msikiti huo pia ndio unatumika kwa ibada na viongozi wakuu wa kiserikali wakiwemo Marais na wageni wa Kimataifa wanaofika mkoani Arusha.


Hadi sasa AMU walishapendekeza ramani ya jengo la msikiti huo mkubwa na wanachosubiri ni majibu ya vipimo vya udongo lakini hivi karibuni kumeshuhudiwa kipande cha eneo hilo kikimegwa na kuzungushiwa uzio wa mabati na kuanzwa kuchimbwa msingi wa ujenzi wa vibanda vya biashara.


Hata hivyo swala hilo limeonekana kuwakera waumini wa msikiti huo na kuamua kuzungumza kwa vyombo vya habari wakimuomba Rais Samia aingilie kati swala hilo kabla ya kuamua kuiburuza Bakwata Mahakamani.


Wakizungumza Leo jumapili Julai 21,2024  Waumini hao wamesema kuwa eneo hilo tiyari walishapata wafadhili wa kusaidia ujenzi huo, na mchoro umeshafanyika, wanachosubiri ni majibu ya vipimo vya udongo pekee ili kuanza ujenzi hivyo maamuzi ya Bakwata kujimegea ardhi kutaka kujenga vibanda katika eneo hilo  hawakubaliani nalo.


Akizungumza kwa niaba ya AMU, Sheikh Aziz Bashir, amesema kuwa eneo hilo walishaliweka wakfu ya utakatifu kwa ajili ya kufanyia ibada hivyo kuwataka uongozi wa Bakwata kuheshimu Kanuni na Taratibu hizo walizozikuta tangu kunajengwa msikiti wa awali mwaka 1967.


‘Huu msikiti ulikuwa ndio mkubwa Tanzania na Afrika mashariki enzi hizo ndio maana hata hadi leo viongozi wakuu wa nchi wanasali hapa, na kwa sasa limekuwa dogo ndio maana tunataka kujenga mwingine, tunashangaa viongozi wa Bakwata kuja kuharibu mazingira yetu na kukata miti hovyo na kuweka uzio hapa bila hata kutushirikisha wakati wanajua malengo yetu” alisema na kungeza;


“Kwa sasa tumewazuia mafundi hakuna kuendelea na ujenzi, hivyo kwa sababu Rais wetu huwa pia anasali hapa tunamuomba aingilie kati swala hili la sivyo tutaiburuza Bakwata mahakamani wakiendelea na ujenzi lakini pia tutadai mali zetu zote sambamba na mapato na matumizi hata ya miradi iliyopo ya shule na maduka kwani haitunufaishi kwa chochote” alisema Bashiri.


Mmoja wa waumini wa Msikiti huo wa Bondeni, Zuberi Ally amesema, Msikiti ni taasisi mbayo inapaswa kughughulikia maendeleo ya imani na elimu na sio miradi ya kuvuruga mahali patakatifu hivyo wako tiyari kulipeleka suala hilo mahakamani kwa ajili ya kupigania eneo hilo muhimu la ibada.


“Lakini pia, msikiti huu Mkuu wa Ijumaa, ndio unaotumika na viongozi wakuu wa nchi, wakiwemo Marais, Mawaziri na Makatibu Wakuu, na viongozi wa mataifa mbalimbali hivyo kiusalama sio sahihi kuujengea vibanda,” alifafanua Ally.


“Msikiti ni eneo nyeti ambalo linatakiwa hasa kuwa na majengo ya kufanyia ibada na pengine sehemu za kutoa elimu kama Madrasa au shule za elimu dunia na Mbinguni ili kuwajenga vijana kiakili na sio vinginevyo sio vurugu,” aliongeza mkazi mwingine wa jijini Arusha, Mama Aisha Jumanne.

 

Akizungumzia sakata hilo kwa njia ya simu, Katibu wa Bakwata Arusha Seif Banka amesema kuwa Ujenzi unaofanyika katika eneo hilo ni kwa ajili ya maduka kwa lengo la kuongeza mapato ya msikiti huo.


Amesema kwa sasa hawezi kuzungumzia zaidi swala hilo zaidi kutokana na kuna sintofahamu ya kufanikisha mradi huo, bila kuutaja.


“Ilikuwa mradi kama miradi mingine ya kuongeza mapato, lakini kwa sasa kuna mambo yameingilia kati ambayo siwezi kuyasema kwa sasa naomba nitafute baada ya siku mbili tatu tutazungumzia undani wake” alisema Seif.


Sheikh wa Mkoa, Shaaban Bin Juma amesema kuwa waliazimia kuwekeza vitega uchumi katika eneo hilo, ila kwa sasa wamesitisha kwa muda.


“Kwa sasa kuna vikao vya ndani vinavyoendelea kujadili suala hili, tutakapokuwa tayari tutawajulisha,” alisema Sheikh Juma.


Mwandishi wa habari alipotembelea eneo la msikiti huo Mkuu wa Ijumaa alishuhudia uzio wa mabati pamoja na kibao cha kibali cha ujenzi wa Maduka chenye Namba 163/2023 huku msingi wa ujenzi ukiwa umeanza.

Picha ya waumini ni kwa hisani ya mitandao

Ends..

Post a Comment

0 Comments