Na Joseph Ngilisho, ARUMERU
Kikongwe mwenye umri wa miaka 90 mkazi wa Kata Sokoni II wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, Penina Madero, amefariki dunia baada ya kushambuliwa na kundi la nyuki wanaodaiwa kufugwa na mwanae
Mwanaye ambaye ni mlemavu wa kusikia Obeidi Alfayo
akizungumza kwa uchungu baada ya tukio, alisema baada ya kupata taarifa kuwa mama yake anashambuliwa na nyuki alijitahidi kwenda kumuokoa lakini ilishindikana.
Alisema ilishindikana kutokana na kuwepo kwa nyuki wengi katika eneo hilo hali iliyosababisha mama yake kuanza kutapika na kuishiwa nguvu na kukimbizwa katika hosptali ya Kaloleni Jijini Arusha na muda mfupi baadaye alifariki dunia.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa kijiji cha Ngiresi, Loti Soleiyo alisema wakazi wa eneo hilo walishindwa kumuokoa bibi huyo kutokana na wingi wa nyuki hao wakihofia kushambuliwa hali iliyosababisha marehemu kukosa msaada.
Kabla ya tukio hilo inasemekana kikongwe huyo kwenye majira ya saa tisa mchana alienda kwenye shamba lake ambalo kijana wake ameweka mizinga miwili ya nyuki kwa ajili ya kuvuna magimbi.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo walisema wakati kikongwe huyo anaendelea kuchimba magimbi nyuki walianza kumshambulia kikongwe huyo hadi kumletea mahuti.
Aidha, kwa mujibu wa mashuhuda hao walisema katika eneo hilo kuna mizinga ya nyuki ya watu wengine kutokana na eneo hilo kuwa na miti mingi ya matunda.
Jana serikali ya kijiji kwa kushirikiana na idara ya misitu ya Wilaya ya Arumeru waliteketeza mizinga yote iliyoleta madhara katika eneo hilo
Inaelezwa kuwa kwa kipindi cha miaka nane iliyopita watu mbalimbali wamejeruhiwa na nyuki hao katika eneo hilo.
Ends....
0 Comments