MGANGA MKUU MATATANI KWA KUMWOMBA RUSHWA MJAMZITO

 By Ngilisho Tv 


MGANGA wa Kituo cha Afya Ndago kilichoko wilayani Iramba mkoani Singida, Dk. Japhet Nkwabi, ameingia matatani baada ya Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda, kuiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kumchukulia hatua kwa madai ya kuomba rushwa ya Sh.152,000 kwa mjamzito.


Aidha, mkuu huyo wa wilaya amemwagiza Ofisa Utumishi na Rasilimali Watu Halmashuri ya Wilaya Iramba kumchukulia hatua za kinidhamu kwa makosa ya kutomtii mkuu wake wa kazi na kutokuwapo kwenye kituo chake cha kazi kwa zaidi ya wiki tatu. 



Mwenda alitoa agizo juzi katika kikao kazi cha watumishi wa halmashauri hiyo ambacho kilikuwa na lengo la kufanya tathmini ya mafanikio na changamoto ya kila idara kwa mwaka wa fedha uliopita 2023/24. 


 "Haiwezekani serikali inatoa huduma za wajawazito bure lakini huyu mtumishi amekuwa akiwaomba kinamama rushwa ili kuwahudumia. Hivi  karibuni alikuja mama mjamzito kutoka kijiji cha Mtekente alitaka kupata huduma ya kujifungua lakini  daktari huyu alimwambia bila kumpa Sh. 152,000 hawezi kumzalisha," alisema.  


Mwenda alisema huduma za afya kwa mjamzito kwa mujibu miongozo ya Wizara ya Afya, zinatolewa bila malipo yoyote na mtumishi yeyote wa afya atakayemwomba rushwa mjamzito, atachukuliwa hatua.



 "Nimekuwa nikipokea tuhuma nyingi dhidi ya daktari huyu kwa watu mbalimbali pia amekuwa hamheshimu  mkuu wake wa kazi mganga mfawidhi wa kituo chake, Dk. Ahmad Selemani, kwa kigezo wana elimu sawa," alisema. 


Alisema daktari huyo katika kuonyesha hamtii mkuu wake wa kazi, ameondoka kituoni kwake kwenda Dar es Salaam bila ruhusa kutoka kwa mkuu wake kituoni wala ruhusa kutoka kwa mwajiri wake. 


Aidha, Mwenda alielezea kuchukizwa na kitendo cha uongozi wa Hospitali ya Wilaya ya Iramba kumhamishia daktari huyo Hospitali ya Wilaya kutoka Kituo cha Afya Ndago.  


"Kama daktari anaomba rushwa kwa wagonjwa na kuwaambia bila kutoa pesa hawezi kuwahudumia na mnaamua kumleta Hospitali ya Wilaya huku si ndiyo atawamaliza wagonjwa wengi" alihoji.

Post a Comment

0 Comments