By Ngilisho Tv-KENYA
Kukamatwa kwa mshukiwa wa mauaji ya Kenya kumezua hisia kali kote nchini - baadhi ya watu wakihoji kuwa polisi wana maswali ya kujibu.
Polisi wanasema Collins Jumaisi Khalusha, 33, alikiri kuwaua wanawake 42 - lakini siku ya Jumanne wakili wake aliiambia mahakama kuwa aliteswa ili kukiri mauaji.
Ni taarifa ya hivi punde zaidi kuhusu tukio la kutatanisha lililofuatia ugunduzi wa mabaki ya miili tisa iliyokatwa vipande, kuwekwa kwenye mifuko, kufungwa kwa kamba na kutupwa kwenye machimbo ambayo hutumika kama jaa la taka karibu na kituo cha polisi mtaani Mukuru, jijini Nairobi.
1) Miili hiyo ilitupwa vipi mita chache kutoka kituo cha polisi
Baadhi ya watu hawaelewi ni kwa vipi polisi hawakuweza kugundua kuwa miili ilikuwa ikitupwa karibu mita 100 kutoka kituo chao kilichopo katika mtaa wa mabanda wa Mukuru Kwa Njenga.
Wakazi wamewakosoa maafisa kwa "utepetevu" katika kushughulikia masuala ya uhalifu.
Kujibu hilo, Kaimu Mkuu wa Polisi Douglas Kanja siku ya Jumapili alitangaza kwamba maafisa wa kituo cha polisi cha Kware kilichopo karibu na eneo la tukio wamehamishwa.
Haijabainika ikiwa wamehojiwa jinsi mauaji hayo yalivyofanywa bila kutambuliwa.
Lakini kutokana na sifa mbaya ya kikosi cha polisi linapokuja suala la haki za binadamu, Mamlaka inayosimamia utendakazi wao ilisema inafanya uchunguzi kubaini ikiwa polisi walihusika kwa vyovyote na mauaji hayo.
CHANZO CHA PICHA,EPA
Maelezo ya picha,Operesheni ya kuopoa miili kutoka kwenye chimbo hilo ilivutia mkusanyiko mkubwa wa watu
Kile kinachoshangaza zaidi ni jinsi wakazi walivyogundua mabaki hayo.
Familia ya Josephine Owino, ambaye alikuwa ametoweka, inasema alimjia "ndotoni" mmoja wao na kuwaelekeza kwenye jalala hilo.
Diana Keya, ndugu wa Bi Owino, aliiambia kituo cha Citizen TV kwamba familia iliwalipa vijana kupekua taka katika jalala hilo.
Hivyo ndivyo miili tisa iliyoharibika vibaya ilipatikana Ijumaa wiki iliyopita. Ilikuwa imefungwa kwenye mifuko ya plastiki kwa kutumia kamba.
Taarifa ya awali ya polisi ilisema "kisa hicho kiligunduliwa" na wakazi.
Alipoulizwa baadaye mkuu wa Kurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mohamed Amin alisema: "Sisi sio waotaji na hatuamini ndoto."
2) Miili hiyo ilikuwa hapo kwa muda gani
Polisi walisema miili iliyopatikana ilikuwa katika hatua tofauti za kuoza, na kuongeza kuwa waathiriwa walikuwa wameuawa nyakati tofauti.
Polisi pia wanasema mshukiwa Bw Khalusha alikiri kuwaua wanawake hao kwa kipindi cha miaka miwili, ushahidi ambalo sasa unatiliwa shaka.
Jambo ambalo haliko wazi ni iwapo mabaki hayo yalitupwa wakati huo au hivi karibuni.
Hussein Khalid, mkurugenzi mtendaji wa shirika la Haki Afrika, aliiambia BBC kwamba maelezo ya polisi kuhusu matukio hayo yalikuwa na "maswali mengi".
0 Comments