WATAALAMU WA POSTA AFRIKA WAKUTANA ARUSHA,WATAKIWA KUONGEZA KASI MATUMIZI YA TEKNOLOJIA ILI KUFUNGUA FURSA ZA KIUCHUMI

Na Joseph Ngilisho-Arusha.

Naibu Katibu mkuu wizara ya ujenzi ,mawasiliano na uchukuzi Zanzibar ,Dk.Mzee Suleiman Mndewa amewataka Wataalamu wa masuala ya Posta Afrika   kutumia vyema maendeleo ya teknolojia katika kuwezesha sekta hiyo kufungua fursa za kiuchumi na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi katika nchi hizo .

Ameyasema  wakati akifungua mkutano wa 42 wa baraza la utawala la Umoja wa Posta Afrika unaoenda sambamba na ufunguzi wa  vikao vya wataalamu wa masuala ya Posta .


 Aidha mkutano huo umewashirikisha Wataalamu kutoka nchi zote za Afrika wanachama wa PAPU ikiwa na  lengo la kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili ili kutoa huduma bora kwa wananchi .

Dk.Mndewa amesema kuwa nchi za Afrika ili ziweze kufanikiwa zaidi katika masuala hayo ni wajibu wao kwa pamoja kama nchi hizo kuhakikisha kila mmoja anashiriki katika uchumi wa kidigitali.

“Kupitia mkutano huu ni wajibu  wetu kuhakikisha tunatafuta  ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili nchi wanachama,kwani  bado kuna changamoto katika nchi za Afrika ikiwemo miundombinu na teknolojia ambazo zinahitaji  kupatiwa ufumbuzi ili kurahisisha mawasiliano kwa haraka”amesema Dk.Mndewa.

Ameongeza kuwa ,ni vizuri  nchi za Afrika kwa umoja wao kutumia teknolojia ili kuweza kupunguza gharama na kuweza kutimiza malengo waliyojiwekea kama nchi.

Naye Posta Masta mkuu ,Maharage  Chande amesema kuwa,mchango wa posta ni kuhakikisha sheria na mambo ya kiutawala yanasaidia kufanya maboresho mbalimbali katika sekta sambamba na kusaidia biashara na uchumi katika nchi za Afrika.


“Tunataka kuzungumza kwa karibu na kuangalia namna tutaweza kufanya biashara kwa urahisi kutoka kusini kwenda kaskazini na tunataka kuhakikisha  kanuni  zinafuatwa katika kufanikisha biashara hiyo. “amesema.

Aidha amesema kuwa ,wanaangalia namna ya kufanya maboresho katika masuala ya bima ambapo amesema Posta kwa sasa wanajitahidi sana katika kuhakikisha  hawatumii  tena barua  kama zamani hivyo wanakimbizana kupokea  teknolojia ili waweze kutimiza malengo yao .

Naye Katibu Mkuu wa PAPU Afrika,Dkt Sifundo Chifu Moyo amesema kuwa , kuna  baadhi ya changamoto ambazo kwa asilimia kubwa tayari viongozi wa nchi hizo wameanza kuzitafutia Ufumbuzi ikiwemo ajenda ya kuendelea kuwasilisha michango kwa kuzingatia mapato kutoka kwa nchi wanachama shabaha kuu ikiwa ni kufikia malengo kwa kutambua umuhimu wa Umoja huo wa posta Afrika.


“Sekta ya posta bado ina mchango mkubwa katika Uchumi na maendeleo kwa kuzingatia masuala ya utawala ikiwemo ajenda ya Kupokea na kuifanyia kazi matumizi ya akili mnemba yaani (Artificial intelligence),katika Hali hiyo ipo haja kwa mataifa haya kuzidi kuimarisha shughuli za kibiashara ili kukuza uchumi wa mataifa haya pamoja na ulipaji Kodi” amesema  Posta masta Mkuu Maharage Chande.

Mkutano huo wa 42 wa baraza la Utawala Afrika umewakutanisha Wataalamu mbalimbali kutoka mataifa zaidi ya 15 sambamba na ufunguzi wa Vikao vya Wataalamu wa masuala ya posta kwa maendeleo ya mataifa hayo yanayo unda umoja wa posta barani Afrika.







Post a Comment

0 Comments