Na Joseph Ngilisho- NGORONGORO
Jamii ya kifugaji ya kabila la Kimasai wilayani Ngorongoro Mkoani Arusha,imewasimika wanawake sita kuwa viongozi wa juu wa kimila(Laigwanani) ikiwa ni hatua nzuri kwa jamii hiyo kuondokana na mfumo dume.
Hatua hiyo imefikiwa ikiwa ni kampeni ya Shirika la Memutie women organization kutoa elimu kwa jamii hiyo na kuwezesha kufanyika kwa sherehe hizo katika kata ya Maalon Juni 18,2024 iliyohudhuliwa na viongozi mbalimbali wa kiserikali na wadau wa maendeleo.
Akizungumza katika tukio hilo la kihistoria mgeni rasmi, Hamza Hamza, katibu tawala wilaya ya Ngorongoro kwa niaba ya mkuu wa wilaya hiyo, alisema shirika la Memutie ni shirika la kuigwa kwa mambo wanayoyafanya na wao kama serikali wapo tayari kufanya kazi na wadau wote wa maendeleo.
Aliongeza kuwa tukio lilofanyika ni tukio la kihistoria kwani katika maisha yake hakuwahi kushuhudia viongozi wa kimila wanawake wanaaminiwa katika vyombo mbalimbali vya kimaamuzi ngazi ya juu akieleza kuwa jamii nyingi hazitambui nafasi ya mwanamke katika kufanya maamuzi ikiwepo jamii ya kimasai.
"Ndugu zangu wanaume kwa wanawake wa jamii hii ya kifugaji binadamu wote ni sawa nichukue nafasi hii kulipongeza shirika la Memutie kwa hatua hii pamoja na jamii hii kwa kutambua mchango wa mwanamke na kuwaingiza kwenye uongozi ili kutoa maamuzi ,hii ni hatua nzuri ya kumkomboa mwanamke na kulikomboa taifa"
Aliwataka wanawake waliosimikwa kwenda kutenda haki katika maamuzi yao ikiwemo kutetea wanawake kupinga mila potofu na kupambana na ukatili katika jamii hiyo ila aliwatahadhalisha kwamba wasije kujisahau na kwenda kuwadharau wanaume ,haki ya mwanaume ipo pale pale.
Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa shirika la Memutie Rose Njilo alisema tukio hilo la kuwasimika laigwanani sita wanawake ni jitihada za shirika hilo kuwaunganisha wanawake kutoka kata sita wilayani humo ambazo ni kata za Piyaya Malambo,Arach , Maroni ,Olerion na Engusero Sambu.
"Tukio lililofanyika ni tukio la kihistoria katika jamii ya kifugaji haikuwa rahisi kuwapa nafasi hii wanawake hii ni kampeni yetu Memutie kuhakikisha kwamba mwanamke anapata nafasi kuleta mabadiliko chanya katika harakati za mapambano ya ukatili dhidi ya watoto "
Alisema katika jamii hiyo jambo hilo halijazoeleka lengo lao ni kuwapa nafasi wa wanawake kushiriki katika maamuzi ya wanaume na kupaza sauti katika mapambano ya ukatili ndoa za utotoni na unyanyasaji.
"lengo kuu ni kuhakikisha wanawake wanashiriki katika vyombo vya kutoa maamuzi ngazi ya kijamii na kuleta mabadiliko chanya katika kupambana na maswala ya ukatili wa kijinsia katika jamii"Alisema Njilo
Miongoni mwa Laigwanani waliosimikwa , Naisho Saipu alisema shirika la Memutie ndilo lilowapatia elimu kuwa wanawake wanaweza kuwa viongozi katika jamii na wao kabla ya kupata hiyo elimu walikuwa wanakumbuna na vitendo vya kikatili ikiwepo ukeketaji na kukosa kupaza sauti zao.
Aliomba serikali kuwaunga mkono viongozi hao wa kimila katika mapambano ya kutokomeza mfumo dume katika jamii na kutokupokea rushwa.
Naye, Lengumo Parimiria ambaye ni laigwanan wa mila kutoka kata ya Engusero sambu amesema wapo tayari kushirikiana na Laigwanan wa kike waliosimikwa na kuwapa ushirikiano huku akisema watafanya kikao cha Malaigwan na Ingaigwanak waliosimikwa hii leo ili kupeana taratibu mbalinbali.
Ends....
0 Comments