SERIKALI KUAJIRI WAHUDUMU WAPYA WA AFYA MIKOA 10 KUNUFAIKA ,DKT MAHERA ASISITIZA MPANGO UMEIVA WANASUBIRI KIBALI ,DKT LUKUMAY AIPONGEZA SERIKALI KWA UWEKEZAJI WA TRILIONI 6.7 SEKTA YA AFYA.

 Na Joseph Ngilisho ARUSHA 


Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI(AFYA)Dkt Wilson Mahera amesema serikali ipo mbioni kuajiri watumishi wapya wa sekta hiyo ikiwa ni mpango mahususi wa kuboresha sekta ya afya nchini ili kuondoa tatizo la upungufu wa watumishi hususani wahudumu  ngazi ya jamii .

Dkt Mahera amebainisha hayo jijini Arusha, wakati akifungua mafunzo ya siku tano yanayofanyika katika Chuo cha Afya CEDHA ,kwa Timu ya uendeshaji huduma ya Afya kutoka Mkoa wa Tanga (RHMT),waratibu wa Afya mama na Mtoto Ngazi ya Halmashauri (CHMT) na wataalamu wa TEHAMA wa Halmashauri zote mkoa huo.
 Mafunzo hayo yamefadhiliwa na shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ)yaliyolenga kuwajengea uwezo ngazi ya uongozi.
Alisema kupitia mpango huo mikoa kumi nchini,itanufaika na  nyongeza ya watumishi wapya ukiwemo mkoa huo wa Tanga lengo ni kupunguza vifo vya mama na mtoto, kupunguza magonjwa ya mlipuko,maambukizi ya magonjwa yakiwemo Malaria.

"Katika bajeti hii serikali imepanga kuajiri watumishi wapya na  sasa tunasubiri tu kibali cha kuajiri na kama mnavyofahamu serikali imekuja na mpango wa wahudumu ngazi ya jamii  watakaosambazwa katika mikoa hiyo ili kuwapunguzia changamoto ya uhaba wa watumishi"alisema Dkt Mahera

Alitoa rai kwa wataalamu hao wa afya wanaopatiwa mafunzo, kutumia ujuzi huo wanaoupata kwenda kufundisha na wengine   ili wakatoe huduma nzuri kwa wananchi huku wakizingatia   maadili ya kazi yao.

Awali mkuu wa Taasisi ya CEDHA ,Dkt Johannes Lukumay  aliipongeza serikali kupitia waziri wa Afya ,Ummy Mwalimu kwa uwekezaji mkubwa wa zaidi ya sh, Trilioni 6.7 katika sekta ya Afya,uwezeshaji iliolenga kuimarisha miundo mbinu ikiwemo vifaa tiba ,dawa na kusomesha madaktari bingwa na bobezi.

Alisema mafunzo hayo yenye washiriki 53 kutoka mkoa wa Tanga yamelenga kuboresha huduma na utoaji wa mafunzo ya msingi ya menejimenti, uongozi na utawala ili kuziwezesha timu  kusimamia,kuendesha na kuboresha huduma za afya,ustawi wa jamii na lishe katika ngazi ya Mkoa ,Halmashauri na ngazi za kutolea huduma za afya.

Dk Lukumay alisisitiza kuwa mafunzo hayo ,wataalamu hao wa afya watapata uelewabjuu ya stadi za uongozi  na utawala na pia watafanya mtihani wa kuwapima (POST TEST) na taasisi hiyo ya CEDHA itawatunuku vyeti.

Katika hatua ngingine dkt Lukumay alisema pamoja na utoaji bora wa mafunzo hayo, Taasisi ya Cedha imekuwa na changamoto ya kupata idadi ndogo ya washiriki.

Alimwomba naibu katibu mkuu kusaidia kuhimiza wataalamu hao wa afya kuona umuhimu wa kuhudhulia mafunzo hayo muhimu katika mustakabali wa sekta ya afya nchini.

Naye mshiriki wa mafunzo hayo elekezi ya uongozi katika sekta ya Afya ,Dkt Steven Mwandambo mganga Mkuu Halmashauri ya jiji la Tanga,aliishukuru serikali kwa kuendelea kutatua changamoto katika sekta ya afya ikiwemo kuwapatia vitendea kazi yakiwemo magari.


Ends..
















 



 

Post a Comment

0 Comments