MBUNGE MPINA KITANZINI SPIKA AMKALIA KOONI , BUNGE KUMSULUBU KAMBA YAWEKWA SHINGONI

By Ngilisho Tv -DODOMA 


Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson ameiagiza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kumhoji Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina kufuatia kitendo cha Mbunge huyo kuzungumza na vyombo vya habari kuhusu ushahidi aliouwasilisha kwa Spika juu ya madai aliyoyatoa bungeni kuwa Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alilidanganya Bunge.


Spika ametoa maelekezo ya leo bungeni jijini Dodoma akieleza kuwa kitendo cha Mpinga, ambaye ni Mbunge mzoefu anayezifahamu kanuni za Bunge, kuwasilisha ushahidi wake na kisha kwenda kuzungumza na vyombo vya habari kuhusu nyaraka za ushahidi huo, ni kitendo cha utovu wa nidhamu kwa Bunge na Spika, kudharau mamlaka ya Spika na kuingilia mwenendo wa Bunge na kushusha hadhi na heshima ya Bunge.


“Kitendo cha Mheshimiwa Mpina kinakwenda kinyume na kifungu cha 29(d)(e) na kifungu cha 34(1)(g) vya Sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge Sura 296,” ameeleza Spika wa Bunge akiongeza kuwa “baada ya kutafakari mazingira ambayo suala hili lilijitokeza na alichokifanya mheshimiwa Mpina tarehe 14 Juni 2024 ni maoni yangu kuwa Mheshimiwa Mpina amemkosea Spika na amelikosea Bunge.”


Amesema “hii ni kwa sababu amepoka fursa ya Spika na Bunge kutumia mamlaka iliyopewa kikanuni kufanyia kazi ushahidi alioutoa bila kuendeshwa na mashinikizo kutoka kwa umma ambao unaendelea kujadili ushahidi huo na kutoa hukumu.”


Kutokana na hayo, spika ameiagiza kamati ikutane kuanzia leo kwa ajili ya kumsikiliza Mpina na itoe maoni ya nini kifanywe na Bunge.


Pia, ameiagiza kamati kupitia ushahidi uliowasilishwa kuhusu madai ya Waziri Bashe kudanganya Bunge, ili kuona kama unathibitisha madai kuwa amesema uongo bungeni na ieleze nini kifanywe na Bunge, ambapo ametaka iwasilishe taarifa kwake Juni 28 mwaka huu.


Juni 4 mwaka huu Spika Dkt. Tulia alimpa Mpina siku 10 (hadi Juni 14 mwaka huu) kuthibitisha madai yake kuwa Waziri Bashe amelidanganya Bunge, baada ya waziri huyo kusema kuwa nchi ina upungufu wa sukari tani 410,000, huku yeye akisema kuwa upungufu uliopo ni tani 120,000 tu, hivyo akaeleza kushangazwa na kitendo cha wizara kuagiza kiwango kinachozidi upungufu uliopo.


Alipohojiwa na Spika kama kwa maelezo hayo anamaanisha kuwa waziri anadanganya, Mpina alikiri kuwa waziri amedanganya na yupo nje ya sheria, hali iliyopelekea Spika kumtaka kuwasilisha ushahidi kama ambavyo kanuni za Bunge zinavyotaka Mbunge kuwasilisha ushahidi anaposema kuwa mbunge anayezungumza au aliyemaliza kuzungumza ameongea uongo bungeni.


Juni 14 mwaka huu Mpina aliwasilisha ushahidi wake, lakini baada ya hapo akazungumza na vyombo vya habari, jambo ambalo Spika ameeleza ni ukiukwaji wa kanuni za Bunge ambazo zinazuia kuchapisha kwa umma taarifa zilizoandaliwa mahsusi kwa ajili ya kuwasilishwa bungeni pasipo kupata kibali cha Bunge na kabla ya taarifa hizo kuwekwa mezani.

Post a Comment

0 Comments