By Ngilisho Tv -HAI
BAADHI ya waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Jimbo la Hai la Dayosisi ya Kaskazini, wakiwamo Wainjilisti wawili, wamejitenga na kisha kuhamia Kanisa la Kilutheri Afrika Mashariki (KKAM) na kusimikwa rasmi kuwa Wachungaji wapya, huku wakitoa sababu za kuhama kwao.
Wainjilisti hao na waumini wengine wanaodaiwa kuwa zaidi ya 100, walipokelewa katika ibada maalum ya Kanisa la KKAM iliyoongozwa na Makamu Mkuu wa Askofu wa Kanisa la Kilutheri Afrika Mashariki, Dk. Philemon Langasi, aliyefuatana na Askofu Philemon Monabani, Juni 20 mwaka huu.
Askofu Dk. Langasi, pia ni Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Arusha ya Kanisa hilo la Kilutheri Afrika Mashariki.
Wainjilisti waliosimikwa rasmi na KKAM, kuwa Wachungaji wao katika eneo hilo, ni Malaki Lais na Michael Laitayo.
Akizungumza na waumini hao waliokusanyika katika eneo la Mlima Shabaha, Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, ambako kulifanyika ibada ya kuwasimika waliokuwa Wainjilisti wa KKKT, kuwa Wachungaji wapya wa KKAM wa eneo hilo, Askofu Langasi alisema:
“Tuna Parishi (Parokia) zaidi ya 40 ambazo tumeshazifungua, tuna Wachugaji sasa hivi 50. Nazungumza kama Makamu wa Askofu Mkuu wa KKAM. Tumeshaifikia takribani mikoa 17.
“Kwa hiyo tumeshafika Songea, Mtwara, Morogoro, Mbeya, Dar es Salaam, Tanga, Simiyu na Manyara, Singida na Arusha. Kwa hiyo ni kanisa ambalo linakua kwa kasi nzuri.
…Kanisa hili ni changa kimuundo, kimsingi na hata linavyosikika katika masikio ya watu, lakini KKAM limekuja kama kanisa la matengenezo.”
Akizungumza baada ya ibada ya kuwaweka wakfu na kutoa itikio la kuwa Mchungaji wa KKAM, Malaki Alais, alisema wao na waumini wanaowaunga mkono, sasa watakuwa wanaabudu Kanisa hilo la Kilutheri Afrika ya Mashariki.
“Baada ya mambo magumu aliyoyapitia katika utumishi wake, nimepata neema ya Mungu, kuungana na kanisa hili katika Parokia ya Semento ya Jimbo la Magharibi la Dayosisi ya Arusha.
“Tunafuraha kubwa, kwa sababu mioyo yetu imekuwa na furaha katika kuungana na kanisa hili. Mimi binafsi lakini na wenzangu waumini, ambao ni wazazi wangu pamoja na majirani katika eneo hili la Semento.
“Tumeungana katika kumtegemea Mungu na kumwamini Mungu, kwa sababu kuna wakati tumejiona kama tumetelekezwa. Tunalo dafrari la wakristo ambao wamekubali kuungana nasi ambao ni zaidi ya 130, ukiweka na watoto, ni zaidi ya wakristo 200,”alisema Mch. Malaki.
Mwisho
0 Comments