DC SAKULO AFUNGUA ZOEZI LA KLINIKI YA TIBA MKOBA ZAHANATI YA ENGARASERO:
By Ngilisho Tv-NGORONGORO
Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Kanali Wilson Sakulo amefanya ufunguzi wa zoezi la tiba mkoba katika Zahanati ya Engarasero iliyopo kata ya Engarasero inayoendeshwa na Madaktari Bingwa Kutoka Marekani na Tanzania watakao toa Matibabu bure Kwa Wakazi 4,000 wa Wilaya ya Ngorongoro, mkoani Arusha kwa muda wa siku tano wanaofanya kazi na Shirika la Worldserve International Tanzania.
Shirika la Wordserve International Tanzania lenye makao yake jijini Arusha kwa kushirikiana na wadau wake waitwao Hands of Hope waliopo chini ya huduma ya Joyce Meyer Ministries (Mwinjiisti wa Kimataifa wa Marekani), na Serikali ya Mkoa wa Arusha, wameanza kuendesha kliniki ya matibabu ya bure katika Kituo cha afya cha Engaresero, wilayani Ngorongoro kuanzia tarehe 3 Juni, na kuhitimisha tarehe 7 Juni, 2024.
Mkuu wa Wilaya amesema Wananchi wamejitokeza kwa wingi ili kuweza kunufaika na huduma hiyo ya bure iliyoletwa na Shirika la Worldserve International na ametumia nafasi hiyo kuwashukuru Wananchi hao kwa kujali afya zao, pia amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwajali Watanzania kwa kuruhusu na kuwakaribisha wageni wetu kutoa huduma za kiafya kwa Wananchi wote wa Wilaya ya Ngorongoro na Wilaya za jirani.
Pia, Mhe. Kanali Sakulo ameyashukuru Mashirika ya Wordserve International Tanzania na Hands of Hope kwa kuamua kuleta huduma hii ya kiafya katika Wilaya ya Ngorongoro, kisha ameyaomba mashirika hayo kuleta vifaa vya tiba zaidi kama utra sound, X-ray, na vingine watakapokuja tena nchini.
"Niwashukuru sana kwa kuja na ninajua mnachokifanya ni kuisaidia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, baadala ya Watu wetu kwenda kupata huduma mjini nyie mmetusaidia wanaipata hapa" amesema Kanali Sakulo.
Aidha, Bi. Victoria Kundansai ambaye ni Mratibu wa programu wa Shirika la Wordserve International Tanzania kwa niaba ya Mkurugenzi naye ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuwawezesha msaada huo wa kuwafikia wananchi wa Engaresero bila kuwepo na vikwazo.
0 Comments