By Ngilisho Tv-Kilosa
MAPACHA wenye umri wa miaka miwili, wamedaiwa kubakwa na baba yao, Hamadi Kapera (20) na kuwasababishia maumivu na maambukizi ya magonjwa ya zinaa.
Hata hivyo, mama mzazi wa watoto hao, Watende Mwishehe (32), ameomba mume wake asamehewe katika kesi hiyo waendelee kulea watoto wao.
Tukio hilo, lilitokea Mei 21, mwaka huu wakati Mama wa mapacha hao, alipowaacha watoto na baba yao na kwenda shambani.
Akizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mkoa wa Morogoro, Shaka Hamdu Shaka, alimweleza kuwa anachokiomba ni kufutwa kwa kesi hiyo, awalee watoto wake.
Awali, Watende alieleza kuwa, siku ya tukio alikwenda shambani na alivyorudi akawakuta watoto wanacheza.
“Niliota watoto wanaingiliwa, ila sikujua ni nani…nikiwa shamba nikamweleza mwenzangu basi tukarudi nyumbani, nikawaogesha watoto wangu…ila nikawaona wana uwazi nikawaonyesha wenzangu embu angaliendi mbona wanakiuwazi,”alisema.
Aliongeza kuwa: “Nikajiuliza wameingiliwa ama ni magonjwa, wakanimbia huenda ni magonjwa kama wangekuwa wameingiliwa hawa watoto wa miaka miwili wangechanika wasingeweza kutembea maana tumewakuta wanatembea.”
Watende aliendelea kueleza kuwa, mapacha hao walikuwa wanatoa majimaji yenye harufu katika sehemu zao za siri, ikabidi awapeleke hospitali na kumweleza Daktari awatizame ni magonjwa ama wameingiliwa.
“Daktari aliniambia wameingiliwa, wakaniuliza unamjua aliyewaingilia nikawajibu simjui, baadae polisi akaja wakaanza kufanya uchunguzi wao na baadaye nikachukuliwa maelezo na siku ya Jumanne naambiwa nikatoe taarifa polisi,”alisema.
Alisema polisi walimwambia ataondoka kwa ajili ya upelelezi ili aliyefanya tukio hilo kubainika na kukamatwe.
“Nikaona amekamatwa mwanaume wangu, akapelekwa kituo cha polisi na kesho yake wakakamatwa wapangaji tukahojiwa na kila mmoja alijielezea vizuri na kutoa ushahidi wao,”alisema.
Aliongeza kuwa: “Leo nimekuja kuomba tulimalize hili, isiwe kesi maana mimi sijawahi kujielezea tusije kufungwa wote huko mahakamani, ndio maana naomba nisaidie hili jambo liishe, huyu baba aje kuilea familia yake,”alisema.
Kutokana na maelezo hayo, Shaka alimhoji mama wa mapacha hao kuwa: “Hivi mama ni kweli hauna uchungu na mapenzi na hawa watoto wako hadi unataka mumeo asihusishwe katika hiyo kesi.
“Wewe ndio unayejua uchungu ambao uliupata kama mume wako hajahusika vyombo vya kutoa haki vitaweka bayana, wewe hofu yako ni nini? hili tukio linajulikana kila kona tunataka kuchukua hatua za kisheria mnatufanyia mambo ya kitoto hapana… hapana… siwezi kukubali jambo hili.”
Aliongeza kuwa: “Kama watoto wamekushinda kuwalea, serikali itawachukua hawa na tutawalea vizuri, wamefanyiwa vitendo vya kinyanyasaji, unyama na ukatili watoto wadogo kama hawa halafu unasema tumsamehe hakuna kitu kama hicho, tusipochukua hatua vitendo hivi haviwezi kuisha, wanaume tunaharibu watoto halafu wake zetu mnatukingia kifua eti aje tulee watoto nampenda sana mume wangu eti watoto watapata shida nani kasema hao watoto watapata shida?”alihoji Shaka.
Hivyo, alimhakikishia kuwa, serikali ipo na watoto hawawezi kupata shida na hata usalama wa mama huyo utaangaliwa kwa karibu.
“Kitendo cha kufuta kesi ni jambo ambalo haliwezikani kabisa,”alisema.
Aliongeza kuwa: “Kila kukicha tunamsikia Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, anapiga kelele na kukemea vitendo vya ukatili, udhalilishaji na unyanyasaji wa kijinsia vinaumiza na kudumaza jamii…pia inauma sana.”
Shaka aliendelea kuhoji: “Kwa nini unataka kesi isiendele, naomba nikuelimishe kisheria mama, huna mamlaka ya kuondoa kesi hii mahakamani na Jamhuri itaendelea kutafuta haki ya kisheria ya watoto hawa wasio na hatia, nakuhurumia mama maana unaweza kuingia katika shida kwa kutaka kubeba dhambi za uovu za mtu, badala ya kusimama haki ya watoto waliofanyiwa unyama na ukatili.”
Hivyo, Shaka alilaani vikali tukio la mama huyo juu ya kitendo hicho na kuwa, serikali itaendelea kuchukua hatua kali za kisheria kukomesha vitendo hivyo pamoja na kuwatambua wote ambao wanalea na kufumbia macho matendo hayo.
0 Comments