Na Joseph Ngilisho ARUSHA
BENKI ya CRDB imekuwa ikiimarika kila mwaka kwa kuongeza faida na thamani ya hisa zake, ambapo kwa mwaka 2023 baada ya kodi, imeweza kupata faida ya sh. bilioni 428.8 ikilinganishwa na sh. bilioni 351.4 kwa mwaka 2022, sawa ongezeko la asilimia 21.
Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB Dkt. Ally Laay kwenye Mkutano wa Waandishi wa Habari na Benki hiyo jijini Arusha katika kuelekea mkutano mkuu wa 29 wa wanahisa wa crdb unaotarajiwa kufunguliwa kesho(leo)jijini Arusha, ambapo mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa rais wa Zanzibar Dkt Hussein Mwinyi.
Aidha dkt Naal alisema kutokana na mafanikio hayo makubwa bodi ya Wakurugenzi imependekeza gawio la shilingi 50 kwa kila hisa ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 11.11 ikilinganisha na gawio la sh, 45 lililotolewa mwaka 2022.
Alisema iwapo pendekezo hilo litaidhinishwa kupitia mkuu wanahisa wataweza kuvuna gawio la sh,bilioni 130.6 sawa na asilimia 34 ya faida halisi ikiwa ni ngezeko la sh, bilioni 117.5 lililolipwa mwaka 2022.
Alisema Mkutano Mkuu wa CRDB wenye kauli mbiu ''ustawi wa Pamoja", unatarajiwa kufanyika jumamosi Mei 18 mwaka huu ukitangukiwa na semina ya wanahisa katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano Arusha (AICC) jijini Arusha.
Katika mkutano huo wa wanahisa watajadili ajenda mbalimbali zitakazowakilishwa ikiwemo mapendekezo ya gawio la hisa,kupokea taarifa za wakurugenzi na kupokea taarifa ya hesabu ya gawio la fedha 2023 ,kuidhinisha ada ya mkurugenzi,kuteua wakaguzi wa fedha .
"Baadhi ya mambo ambayo yatatakiwa kuidhinishwa yapo katika taarifa ya mwaka ikiwamo taarifa ya Wakurugenzi, na pendekezo la gawio ambapo mwaka huu Bodi ya Wakurugenzi imependekeza ni gawio la sh.50 kwa hisa, ikiwa ni ongezeko la asilimia 21 kulinganisha na gawio la sh. 45 lililotolewa mwaka jana".
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Group Abdulmajid Nsekela, alisema benki hiyo inayomilikiwa kwa mfumo wa hisa, inatambua jukumu muhimu ambalo wanahisa wake wanalo katika kuimarisha utendaji wa benki na kuamua mustakabali wa sasa na baadaye.
Nsekela alisema nguvu ya Benki ya CRDB ipo katika uwezo wa pamoja wa wanahisa wao. Maoni yao yanawawezesha kukabiliana na changamoto, kutumia fursa, na kutoa ukuaji endelevu kila mara. Hilo limewasaidia, kujenga msingi imara na thabiti ambao juu yake wameendelea kushuhudia mafanikio makubwa.
Alisema mkakati wa utendaji kazi wa miaka mitano ulioanza mwaka jana 2023 hadi 2027 unalenga kuleta ufanisi katika benki hiyo ikiwemo kupanua matawi katika nchi mbalimbali na tayari benki hiyo imezifikia nchi za DRC Kongo na Burundi na Mpango wa usoni ni kufungua matawi katika nchi ya Zambia,Uganda,Visiwa vya Comoro
“Bodi yetu ya Wakurugenzi ikiwa chombo cha uwakilishi wa Wanahisa katika kuisimamia vyema benki yetu kwa manufaa ya wanahisa, imekuwa ikifanya kazi nzuri ikiwamo kuhakikisha Mkutano Mkuu unafanyika na wanahisa wanapata haki yao ya msingi ya kufanya maamuzi, na kuwasilisha maoni kwa ajili ya kuboresha utendaji wa benki yao” .
"Mkutano wetu huu wa 29 utakuwa mzuri sana kwa sababu utatafakari mwaka wa kwanza wa mkakati wetu wa miaka mitano ambao umeanza mwaka jana 2023,ila nafarijika sana kuona tumeifikia DRC Kongo kwa kufungua tawi letu baada ya tawi letu Burundi kufanya vizuri sana kwa kuongoza kwa kupata faida kubwa".Alisema Nsekela.
Aidha amewahamasisha wanahisa kuhudhuria Semina na Mkutano Mkuu ikiwa ni haki yao ya kimsingi na kisheria lakini pia ushikiri wao unasaidia kuongeza tija na ufanisi katika uendeshaji wa Benki ya CRDB.
Katika mkutano huo pia Benki hiyo imetumia fursa hiyo kuzindua rasmi taarifa ya mwaka ya Benki pamoja na Ripoti ya ustawi endelevu (Sutainability Report) ambazo zinapatikana kwenye tovuti yao.
Ends...
0 Comments