MAKONDA AWASHUKIA KAMA MWEWE WATENDAJI LONGIDO ,p

Na Joseph Ngilisho LONGIDO

Mkuu wa mkoa wa Arusha Paul Christian Makonda ameonya tabia ya baadhi ya watendaji wa serikali na taasisi zake kutotembelea miradi ya maendeleo suala ambalo limekuwa likisababisha wananchi kuteseka na ukosefu wa huduma mbalimbali za kijamii licha ya serikali kutoa fedha nyingi za kutekeleza miradi hiyo


Makonda ametoa kauli hiyo mapema leo, Mei 23, 2024 wakati alipotembelea Zahanati ya kijiji cha Lemereta pembezoni mwa mji wa Longido na kuelezwa kuhusu changamoto za ukosefu wa umeme wa uhakika na kutopatikana kwa maji kwenye Zahanati hiyo iliyo muhimu kwa wakazi wa kijiji cha Lemereta

Supuk Melita ambaye ni Mwenyekiti wa kijiji cha Lemereta amemueleza Mkuu wa mkoa huyo kwamba licha ya kutoa taarifa kwa mamlaka ya maji vijijini na kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wilaya ya Longido, ni miezi mitatu sasa hawakuwahi kuona maafisa wa mamlaka hizo wakifika na kutatua changamoto walizowasilishiwa na wananchi

Kufuatia hali hiyo, Makonda amemtaka Ramadhan Musiba ambaye ni Meneja wa mamlaka ya maji vijijini wilaya ya Longido kumuandikia barua mteule wake (Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji) ili kueleza kuhusu udanganyifu alioutoa kwa uongozi wa mkoa wa Arusha pamoja na kushindwa kuwa mfuatiliaji mzuri wa miradi ya maji inayotakiwa kusimamiwa na ofisi yake

Katika Hatua nyingine, Makonda amemuagiza Lazaro Lenoi ambaye ni Meneja wa TANESCO wilaya ya Longido kuhakikisha kuwa ndani ya siku tatu Zahanati ya Lemereta inakuwa na umeme wa kutosha ili kuondokana na changamoto ya umeme kushindwa kuendesha vifaa tiba na mashine nyingine zinazotumika kwenye Zahanati hiyo

Amewataka watendaji kuwa na utamaduni wa kwenda kwa wananchi kila wakati na kutatua changamoto zao badala ya kukaa ofisini pekee na matokeo yake kusababisha ubadhirifu, uharibifu na kusuasua kwa miradi mingi ya maendeleo inayosimamiwa na serikali ya awamu ya sita.

Ends..

Post a Comment

0 Comments