Na Joseph Ngilisho ARUSHA
KAMATI ya sheria, haki na hadhi za wabunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA)imeanza uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili aliyekuwa katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo dkt Peter Mathuki ikiwemo matumizi mabaya ya Madaraka na kusababisha upotevu wa fedha zaidi ya dola milioni 6 za Marekani .
Dkt Mathuki(Raia wa Kenya) ambaye hivi karibuni nchi yake ilimwondoa madarakani kutokana na tuhuma hizo ,atahojiwa na kamati hiyo ili kujibu tuhuma zinazomkabili,zilizoibuliwa na mbunge wa bunge hilo, Kennedy Mukulia kutoka nchi ya Sudan kusini.
Akiongea na vyombo vya habari makao makuu ya jumuiya hiyo jijini Arusha mwenyekiti wa kamati hiyo,Mashaka Ngole,(EALA Tanzania)alisema tuhuma hizo ziliwasilishwa hivi karibuni katika bunge hilo lililoketi nchini Kenya na kupokelewa na spika wa bunge hilo na baadaye kuwasilishwa kwenye kamati hiyo ya bunge.
"Tuhuma zinazomkabili Katibu mkuu ambaye kwa sasa amesimamishwa kazi kupisha uchunguzi ni pamoja na matumizi mabaya ya ofisi yake ,matumizi mabaya ya mali za Jumuiya ya Afrika Mashariki na tayari kablasha la ushahidi wote tunalo maana tuhuma ni nyingi"
Dkt Matuki aliteuliwa kuwa katibu Mkuu wa EAC,Februari 27,2021 wakati wa Mkutano wa kwanza wa wakuu wa nchi uliofanyika kwa njia ya Mtandao na kwamba iwapo tuhuma hizo zitathibitika atakuwa katibu Mkuu wa kwanza wa EAC kuondoshwa madarakani kabla ya muda wake wa miaka mitano wa kuhudumu wadhifa huo .
Taarifa za tuhuma hizo ziliibuliwa nchini Kenya katika kikao cha bunge hilo wakati bunge hilo likijadili matumizi ya dola milioni 6 za Marekani ambazo zinadaiwa kutumika bila kupata kibali cha bunge hilo chini ya dkt Mathuki.
"Tuhuma zinazomkabili katibu mkuu huyo ni matumizi mabaya ya fedha za mfuko wa usalama ,uuzwaji wa mali za Jumuiya kwa bei chee yakiwemo magari bila kufuata sheria ,kuajiri wafanyakazi bila kushirikisha ofisi inayohusika na ajira ,kuhamisha wafanyakazi bila kuzingatia utaratibu ,kuajiri walinzi bila kufuata utaratibu,kufungua akaunti za fedha bila kufuata utaratibu na tuhuma zingine nyingi"
Mwenyekiti huyo alisema kuwa kamati hiyo imekutana Arusha ili kupitia kablasha lililosheheni tuhuma hizo pamoja na kukusanya mashahidi na kuwahoji ili kupata uthibitisho wa tuhuma hizo.
"Leo tumekutana hapa na tayari wajumbe wa kamati wamekabidhiwa kablasha lenye tuhuma ili walipitie na waone kilichomo na baada ya hapo ni kukusanya ushahidi kwa kuwaita mashahidi waliotajwa ili tuwasikie na baadaye tutamwita mtuhumiwa na kumhoji"alisema Ngole.
Dkt Mathuki ambaye kwa sasa ameteuliwa na nchi yake kuwa balozi nchini RUSSIA, nafasi yake ya ukatibu mkuu EAC inashikiliwa na Caroline Mwenda Mueke aliyependekezwa hivi karibuni na serikali yake ya Kenya kumalizia kibarua cha Miaka Miwili iliyosalia.
Hata hivyo uteuzi wake utalazimika kuidhinishwa na wakuu wa nchi katika mkutano mkuu .Nchi ya Kenya itakuwa na makatibu wakuu wawili akitanguliwa na Francis Muthaura aliyehudumu kuanzia mwaka 1996-2001.
Makatibu wakuu EAC waliotangulia walikuwa ni Francis Muthaura (1996-2001)Nuwe Amanya Mushega (2001-2006)Juma Mwapachu(2006-2011),Richard Sezibera(2011-2016)na Liberat Mfumukeko(2016-2021)
Ngole alisema kamati yake ikikamilisha uchunguzi wa tuhuma za dkt Mathuki itawasilisha ripoti yake katika bunge hilo linalotarajiwa kuketi mapema mwezi ujao wa Juni.
Dkt Mathuki ambaye kwa sasa ni Balozi wa Kenya Nchini Russia huenda akashtakiwa iwapo tuhuma zake zitathibitika na hivyo kuweka rekodi ya kwanza kwa kiongozi wa juu wa jumuiya hiyo kushtakiwa kwa makosa ya ubadhilifu wa mali katika sekretarieti ya Jumuiya hiyo na hivyo kuipa doa nchi yake .
Kwa upande wake Mbunge wa EALA, Kennedy Mukulia alishukuru kupokelewa kwa taarifa yake aliyoiibua bungeni nankupewa uzito anaamini haki itatendeka ili kukomesha vitendo vya ufisadi ndani ya sekretarieti ya jumuiya ili jumuiya hiyo isonge mbele.
"Kuhusu ni wapi nimepata taarifa hizo ni habari za kiuchunguzi sisi kama wabunge hatuwezi kukubali kuona nali ya jumuiya hiyo inakuwa mbaya na fedha zikitumika ndivyo sivyo kuna wakati sekretarieti haina fedha hata za mishahara ya wafanyakazi kumbe fedha zinaliwa na wajanja wachache"
Ends...
0 Comments