Na Joseph Ngilisho ARUSHA
BENKI ya CRDB nchini Burundi imeeleza namna ilivyofanikiwa kuteka soko la kifedha nchini humo kwa kurahisisha shughuli za kibiashara kwa wafanyabiashara waliopo nchini humo na wenzao waliopo nchini Tanzania na nchi jirani ya DRC Congo.
Akiongea na vyombo vya habari
katika Mkutano Mkuu wa 29 wa benki hiyo uliofanyika jijini Arusha, Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo ya CRDB Burundi, Fredrick Siwale alisema tangia kuanzishwa kwa kampuni Tanzu ya CRDB nchini humo mwaka 2012 imefanikiwa kuwa na wateja zaidi ya 45,000, matawi manne na mawakala 1500 wanaotoa huduma za kibenki nchini humo.
Alisema benki hiyo kwa sasa ipo katika hatua nzuri ya kupanua wigo wa huduma zake kwa kuongeza Matawi mengine mawili katika miji ya Makamba na Gitega ili kuweza kuwapatia huduma za kibenki wananchi waliopo maeneo ya mpakani.
"Tumekuwa tukitoa huduma mbalimbali za kibenki kwa njia ya kimtandao kwa wananchi wa mjini na vijijini na tunatarajia mwaka huu kupanua huduma zetu za kibenki kwa kuongeza matawi mengine mawili, tunawashukuru sana wananchi pamoja na serikali ya Burundi kwa kutuunga mkono yakiwemo makampuni Makubwa "alisema Mkurugenzi na Kuongeza
"Benki yetu imeingia nchini Burundi mwaka 2012 ina matawi manne kwa sasa yanayotoa huduma pamoja na mawakala zaidi ya 1500 wanaohakikisha wananchi na wafanyabiashara wanahudumiwa kwa wakati na mapato ya Serikali kukusanywa kwa utaratibu rahisi nchini humo"
Akiongelea mpango wa nchi za jumuiya ya Afrika mashariki kuwa na Sarafu moja. Alisema mpango huo iwapo utafanyika utasaidia katika shughuli za kibiashara katika kununua,kuuza na kusafirisha na hivyo soko la pamoja la jumuiya hiyo litakuwa na manufaa makubwa kwa benki yao.
Akiongelea Siri ya mafanikio ya benki hiyo ,Siwale alisema ni utofauti uliopo kati ya benki yao na mabenki mengine,ambapo CRDB imekuwa ikitoa huduma bora ya kidigitali kwa wateja kwa muda wa masaa 24 ambayo imesaidia kuondoa msongamano.
Aidha alisema sera ya CRDB ni pamoja na kuunga mkono sekta ya kilimo ambapo wananchi wengi nchini humo wamewekeza kwenye kilimo na sisi tunasapoti sekta hiyo kwa asilimia 85 na benki hiyo imekuwa ikiwapatia mkopo .
"Tumekwenda katika sekta zote zinazochochea uchumi nchini Burundi katika kilimo na tunasapoti asilimia 85 ya ajira na sekta ya usafirishaji kwa asilimia 40"
Awali Mkurugenzi mtendaji wa CRDB Group,Abdulmajid Nsekela alieleza mafanikio wanayoyapata katika benki Tanzu ya nchini Burundi na kusema kwamba benki hiyo nchini humo imeongoza kwa kupata faida kubwa.
"Benki yetu ya crdb imekuwa na ukuaji endelevu na katika kampuni Tanzu ya Burundi imekuwa na mafanikio makubwa ya kupata faida kubwa itakayopelekea wanahisa kupata gawio kubwa"
Ends...
0 Comments