Na Joseph Ngilisho ARUSHA
Waziri wa Mali asili na Utalii,Angellah Kairuki amefuta malipo ya leseni kwa dola 50 za kimarekani walizokuwa wakitozwa waongoza utalii nchini,badala yake amesema ada hiyo sasa italipwa kwa fedha za kitanzania ambayo ni sh, 100,000 tu kwa miaka mitatu, kuanzia julai mwaka huu.
Aidha, Kairuki amefuta viingilio kwa waongoza watalii katika mageti ya hifadhi kwa waliolipia leseni zao za usajili.
Kairuki ametoa kauli hiyo ,mjini Arusha akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi kwenye mkutano wa pamoja baina ya Wizara na wadau wa sekta ya utalii ambao ni Chama cha Waongoza Utalii, Wakala wa Usafirishaji Utalii, Vyama vya Wamiliki wa Huduma za Malazi na Vyama vya Wabeba Mizigo kujadili masuala mbalimbali ili kuboresha sekta hiyo.
Marchi 26 Mwaka huu waongoza utalii zaidi ya 1000 walifanya ukutano wao jijini Arusha, kujadili mambo mbalimbali ikiwemo malipo ya leseni kutozwa kwa dola 50 kwa mwaka na kutoa maadhimio ya kumwomba rais Samia Suluhu kushughulikia changamoto hizo ikiwemo kulipishwa viingilio kwenye mageti ya hifadhi,jambo ambalo waziri Kuituki amelitekeleza na kuibua shangwe kwao.
Waziri alisema wadau wa utalii wana mchango mkubwa katika uchumi wa taifa ambapo amefafanua kuwa sekta hiyo inachangia takribani asilimia zaidi ya 25 ya mapato ya fedha za kigeni na kutoa fursa za ajira na kuchochea ukuaji wa sekta nyingine muhimu.
Katika mkutano huo Waziri Kairuki amemtaka Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Utalii (TTB) ambaye ameteuliwa hivi karibuni , Ephraim Mafuru kushirikiana na wadau mbalimbali wa utalii nchini ili kuendelea kuvitangaza vivutio vya utalii duniani.
Ametoa wito kwa waongoza watalii kuwa wazalendo kwa kuwa wao ndiyo mabalozi wa taifa huku akisisitiza kuwa wageni hukaa nao kwa muda mwingi hivyo ni muhimu kutoa taarifa sahihi.
Akiongea katika kikao hicho, Muongoza utalii, Hope Tumaini ambaye amekuwa kwa zaidi ya miaka 15 ameishukuru Serikali kwa kazi kubwa inayoifanya huku akiomba Serikali kutoa mafunzo maalum kwa waongoza watalii hususan wanawake.
Waziri alisema kuanzia mwakani Serikali itatoa mafunzo ya utalii kuanzia kwenye ngazi ya Sekondari ambapo wadau wa utalii pia watahusishwa katika maandalizi ya mitaala ya utalii ili mafunzo hayo yawe na tija.
Katika mkutano huo baadhi ya mambo ambayo yamejadiliwa na kupatiwa ufumbuzi wakati mengine yakiendelea kufanyiwa kazi ni pamoja na kupunguza ada ya leseni ya waongoza Utalii iliyokuwa USD 50 kila mwaka ambapo sasa itakuwa laki moja kila baada ya miaka 3 ada hiyo itaanza Januari 2025.
Pia malipo ya ada ya leseni hiyo ya waongoza watalii ya dola za kimarekani 50 sasa itaanza kulipwa kwa shilingi za kitanzania kuanzia Julai mwaka huu.
Wadau hao wa Sekta ya Utalii wametumia mkutano huo na Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuleta mabadiliko chanya katika kipindi kifupi cha uongozi wake, huku wakisifu kasi ya sasa ya utendaji wa Wizara.
Awali akimkaribisha Waziri Kairuki katika mkutano huo Dkt. Abbasi amesisitiza kuwa katika kipindi hiki Serikali itakuwa karibu na wadau kwenye kila hatua ili kuhakikisha sekta inasonga mbele kwa maslahi ya wadau na taifa kwa ujumla.
Miongoni mwa waongoza utalii jijini Arusha , Davis Lewis aliishukuru sana Serikali kwa kusikia kilio chao na kueleza kuwa amejawa furaha kiasi kwamba imemlazimu kumshukuru mungu kwa kutoa shukrani kanisani kwani jambo hilo limewasimbua na kuwaumiza kwa muda mrefu .
Ends..
0 Comments