Na Joseph Ngilisho..ARUSHA
Mfanyabiashara Jofrey Mollel Mkazi wa Baraa jijini Arusha,amedai kutapeliwa na mfuko wa maendeleo ya jamii, Tasaf jijini Arusha kiasi cha sh, milioni 19 baada ya kuwapatia vifaa vya ujenzi na kugoma kumlipa na hivyo amemwomba mkuu wa mkoa wa Arusha Paulo Makonda kumsaidia ili aweze kupata fedha zake na kuwachukulia hatua wezi wa fedha zake.
Aidha mfanyabiashara huyo amedai yupo katika wakati mgumu wa kuuzwa kwa nyumba yake aliyoiweka reheni kwenye taasisi ya fedha baada ya kuchukua mkopo akitengenea fedha hizo kukomboa nyumba yake.
Akiongea kwa uchungu,Mollel alisema kuwa mwezi wa sita mwaka jana aliingia makubaliano ya kuwapatia vifaa vya ujenzi Tasaf kwa ajili ya kutekeleza mradi wa ujenzi wa uzio katika shule ya msingi Shangarao iliyopo katika kata ya Moivaro jijini Arusha.
Alisema "kabla ya kuanza biashara hiyo alikuja diwani wa kata hiyo ,Philemon Meijo akiwa ameambatana na mratibu wa Tasaf jijini hapa, aliyemtaja kwa jina moja la Mlay ,diwani aliniambia kuwa kuna mradi wa Tasaf unatekelezwa kwa ajili ya ujenzi wa uzio na kuniomba niwe msambazaji wa vifaa vya ujenzi,nilikataa kwa sababu mtaji wangu ni mdogo"
Diwani pamoja na Mratibu wa Tasaf (Mlay)walinibembeleza wakidai kuwa pesa nitalipwa hata kabla ya kutoa mzigo hivyo nisiwe na wasiwasi "walinipeleka kwenye kamati ya ujenzi kunitambulisha na nikaanza mara moja kuwapatia vifaa vya ujenzi.
Alisema baada ya makubaliano hayo aliwapatia mifuko 200 ya simenti yenye thamani ya sh 3,200,000 milioni ,baadaye walichukua nondo 358 za thamani ya sh, milioni 8,392,000 ,Binding ware 5,sh,425,000 ,Misumari kilo 30 sh,120,000 na nondo 250 za thamani ya sh, 3,500,000. Ambapo jumla yake ni sh,milioni 19,037,000.
"Baada ya kumaliza kutoa mzigo nilianza kufuatilia malipo yangu ,alitumwa mwakilishi wa Tasaf kuja kuhakiki hesabu na kupeleka ofisini kwao na baadaye waliniambia niende benki kuthibitisha akaunti yangu kwa mhuri wa benki ,nilisubiria pesa sioni wakaniambia tena lilete risiti ya EFD nikapeleka lakini bado waliendelea kunizungusha"
Alisema aliamua kumfuata diwani wa kata hiyo ambaye alimtambulisha kwake mratibu wa Tasaf , lakini naye alianza kumpiga chenga akawa hapokei hata simu yake ya mkononi.
"Nilimfuata diwani ambaye naye alikuwa akinipiga chenga nilimfuata hadi kwa wazazi wake ambao walinikutanisha naye na kuniahidi kufuatilia malipo yangu lakini pia sijafanikiwa jambo ambalo hata diwani atakuwa alihusika na wizi wa fedha zangu maana hanipi ushirikiano tena"
Alisema septemba mwaka jana aliamua kwenda ofisi ya mkuu wa wilaya ya Arusha kupeleka kilio chake,lakini alikutana na wasaidizi wake na baada ya kuwaelezea walimpigia simu Mlay ambaye aliwaambia wamzuie Mollel asiingie kwa DC.
"Baada ya muda mchache Mlay na wenzake walikuja wakiwa na gari ndogo na kuniomba niingie kwenye gari hilo na mmoja wapo aliyemtaja kwa jina la Mhandisi Enock alimwambia kuwa watamletea fedha hizo tasilim jambo ambalo hawakulitekeleza badala yake waliendelea kunizungusha "
Alisema mapema mwaka huu aliamua kupeleka kilio chake kwa aliyekuwa mkuu wa Mkoa wa Arusha,John Mongela na baada ya kumsikiliza Mongela aliahidi kulifuatilia suala hilo na kuchukua hatua.
Alisema wiki iliyofuata Mongela aliitisha kikao ofisini kwake na kuwaita wahusika wote akiwemo mkurugenzi wa jiji la Arusha,Juma Hamsin, na katika majadiliano hayo alisema Mongela alithibitisha kuwa Mlay na wenzake walihusika kuiba fedha hizo na kutishia kumweka lokapu polisi.
Alisema Mlay aliahidi kurejesha fedha hizo wiki iliyofuata siku ya jumanne na kumtaka Molel na Mlay wakamalizane ofisi ya mkuu wa wilaya lakini hakufanya hivyo.
Mollel alisema wiki ilipofika alienda kwa dc kufuatilia jambo lake lakini hakuambulia chochote ,aliendelea kufuatilia mara kadhaa , lakini baadaye mkuu huyo alimwambia jambo hilo limemshinda na kumwandikia barua ya kurejea tena kwa Mkuu wa mkoa.
"Niliamua kurejea tena kwa RC Mongela ambapo Mkuu huyo alinipokea na kuwaita pande zote pamoja na Mkurugenzi wa jiji la Arusha ,pia mkuu huyo alibaini kwamba Mlay na Genge lake wamekuwa wakichepusha fedha za umma na kuweka kwenye akaunti ya mfanyabiashara mmoja aliyemtaja kwa jina moja la Secy.
Katika kikao hicho mkuu wa mkoa alimpigia simu mfanyabiashara SECY mkazi wa Moshi na kuweka Sauti ya juu,na baada ya kujitambulisha na kumuuliza fedha anazoingiziwa na Mlay alikiri kuingiziwa fedha mara kwa mara na baadaye Mlay na Enock huja kuchukua na kumwachia sehemu ya fedha hizo.
Wakati Mongela akimhoji Cesy kwa njia ya simu, alikiri kuingiziwa kiasi cha sh, milioni 64 kwenye akaunti yake na kabla ya hapo aliingiziwa kiasi cha sh milioni 300 na baadaye Mlay na mhandisi Enock humfuata na kuzitoa fedha hizo na kumwachia kiasi cha fedha hizo.
Hata hivyo Mongela aliahidi kulifanyia uchunguzi zaidi suala hilo ,lakini kabla hajatoa ufumbuzi wa fedha za mfanyabiashara huyo alipata uhamisho wa kikazi.
Mollel amemwomba Rc Makonda kufuatilia udanganyifu ndani ya Tasaf unaofanywa na baadhi ya watumishi wasio waadilifu na kuwachukulia hatua .
Akiongelea sakata hilo Mkurugenzi wa jiji la Arusha, Mhandisi Jumaa Hamsin, alisema mfanyabiashara huyo hakuwa na mkataba na Tasaf .
"Tumemwomba huyo mfanyabiashara alete mkataba wake na Tasaf,ila tunaona hapakuwa na mkataba "alisema Hamsin kwa kifupi.
Naye mkuu wa wilaya ya Arusha, Felisician Mtahengerwa alikiri kufahamu sakata hilo na kueleza kwamba kuna mkangamyiko wa namna jambo hilo lilivyofanyika kwa sababu hapakuwa na nyaraka zinazoonesha makubaliano ya maandishi katika biashara hiyo ila hakuna ubishi Mfanyabiashara huyo aliwapatia vifaa vya ujenzi Tasaf
"Ni kweli Jofrey alifika ofisini kwangu kuhusu madai yake lakini tumeshindwa kulipatia utatuzi kwa sababu hakuna nyaraka za moja kwa moja juu ya biashara hiyo na Tasaf ,suala hilo hakuna asiyejijua hata takukuru wanalijua ila "
Aliongeza kwa kusema, amemwagiza Mkurugenzi wa jiji la Arusha, Mhandisi Hamsini kuunda tume maalumu itakayochunguza jambo hilo na ukweli utajulikana.
Ends..
0 Comments