MBUNGE EAC AFUNNGUKA WATU KUPIGWA WANAPOKUTWA WANAKULA ZANZIBAR WAKATI WA MFUNGO WA RAMADHANI

 *UFAFANUZI KUHUSU KUPIGWA MTU ZANZIBAR KWA KUKUTIKANA AKIWA ANAKULA MCHANA NDANI YA MWEZI MTUKUFU WA RAMADHANI*

                       

Abdullah Hasnu Makame *PhD*

*1.  UTANGULIZI*

Nikiwa mwana jamii mwenye kufuata imani ya Kiislamu, na kadhalika ninayeishi Zanzibar na ni Mzanzibar kwa kuzaliwa na kwa asili ya wazazi wangu, nimeguswa sana na kadhia ya kusambazwa video inayoonesha vijana wa kiume  wakimtandika mwanaume mwenzao ambaye alikuwa amevaa kofia za uzi wa kufuma wanazopendelea kuvaa watu wanaofuata itikadi ya ' _Rastafari_'

Kwa hakika kitendo kile kiliniumiza sana, nikadhamiria kuweka mawazo yangu kwenye maandishi haya, pengine - huenda yakawasaidia watu mbalimbali kuweza kuelewa changamoto iliyojitokeza katika maudhui ile na hivyo kuchukua hatua stahiki ili kuweza kuepuka taharuki nyingine.

*2.  NGUZO YA KUFUNGA MWEZI MTUKUFU WA RAMADHANI*
Dini ya Kiislamu inasimama kwa kuzingatiwa na kutekelezwa kwa nguzo tano, ambapo nguzo ya nne kati ya hizo tano ni kufunga mwezi mtukufu wa Ramadhani.                        
      
*[2:183] "Enyi Mlioamini, imefaradhishwa kwenu funga kama ilivyofaradhishwa kwa waliokuwa kabla yenu ili [pengine] mpate Ucha Mungu"*

Aya hiyo ya Kitabu Kitakatifu ndio inayotoa msingi wa ibada ya kufunga, ambayo ni dhahiri kwamba waliofaradhishwa kufunga mwezi wa Ramadhani ni Walioamini - yaani ni Waislamu. Ibada ya kufunga mwezi wa Ramadhani anayeshurutika kuitekeleza ni mja aliyeamini ujumbe wa Mtume Muhammad SAW. Aidha, aya inaeleza kwamba Waislamu sio wafuasi wa kwanza wa dini kufaradhishiwa ibada ya funga kwani waliotangulia katika imani kabla yao nao waliwahi kufaradhishiwa ibada ya funga, 'Waliotangulia katika imani' kwa mujibu wa Quran ni wale waliowafuata Manabii na Mitume wa haki kabla ya kuja Mtume Muhammad SAW. Izingatiwe kwamba dini kuu nyingi duniani zinatokana na Mtume Ibrahim AS, ambaye yeye ni Baba wa Mayahudi, Manasara na Waislamu. Lengo la kutekeleza ibada ya saumu ni kutafuta UchaMungu

Waislamu ambao ni wasafiri na wagonjwa hawashurutiki kufunga, kwa sababu dini ya Kiislamu inakusudia kuwepesisha mambo na wala siyo kuyatia mambo yoyote uzito.

                                  
*[Quran 2:184] ”Ibada ya funga imepangiwa siku maalum (Mwezi wa Ramadhani); Lakini ikitokea yeyote kati yenu kuwa ni mgonjwa au yuko safarini,  wamepata udhuru wa kufidia siku walizokosa kufunga"*

Kufuatia maelezo yaliyotolewa hapo, ni dhahiri kuwa ibada ya funga kwa mwezi wa Ramadhani ni sharti kwa Waislamu, lengo lake ni kutafuta ucha Mungu, na waislamu wasafiri au wagonjwa hawashurutiki kufunga, bali watatakiwa kufidia siku ambazo hawakuweza kufunga.

*3.  KITENDO CHA KUPIGWA MTU ZANZIBAR KWA KULA MCHANA NDANI  YA  MWEZI MTUKUFU WA RAMADHANI*

Video ya kushambuliwa kwa kupigwa mtu kisiwani Unguja imesambaa kwa kasi sana katika mitandao ya kijamii *[viral]*, huku ikiambatana na ujumbe wa aina mbalimbali. Wapo ambao wameunga mkono kitendo hicho na wako waliopinga kitendo hicho, kwa kuwa kimeonesha uonevu na hali ya kutokuvumiliana. Wengine walienda hatua ya ziada ya kutoa maelezo ambayo sio rafiki kwa ustawi wa jamii ya kitanzania, wakionesha chuki dhidi ya wenzao na kwamba sasa wamepata sababu ya kudhihirisha chuki zao hizo; ambazo kwa kiasi kikubwa zinachangiwa na hali ya kukosa elimu au kwa lugha nyepesi ujinga.

*3.1 KUMUADHIBU MTU KWA KULA RAMADHANI MCHANA NI KOSA*

Kufuatia maelezo yaliyowasilishwa hapo awali, ibada ya funga NI SHARTI KWA WAISLAMU na hivyo basi siyo sharti kwa wengine wasiokuwa waislamu. AIDHA, sharti hilo haliwagusi WASAFIRI na WAGONJWA. Kwa maana sahihi ni kwamba Waislamu wanaofunga mwezi mtukufu wa Ramadhani hawana haki ya kumshurutisha mtu yoyote kufunga au kutokula mchana hadharani ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Sababu za kisheria, zinazotokana na Quran Takatifu ndiyo zinaelekeza hivyo. Hata kama Waislamu hao watakuwa wanataka kuitangaza dini yao, basi hawapaswi kutumia ubabe, kwani mwongozo wa Quran ni kutokulazimishana kwenye dini. Anayetaka atafuata kwa hiyari yake, na asiyetaka ni hiyari yake kukataa.

*(Quran 2:256)   'Hakuna / hapana kulazimishana katika kufuata dini'*

Mtume Mussa AS alitumwa kwa Mfalme Firauni - ambaye alitakabari na alifikia hatua ya kuwatangazia raia wake wa Misri kuwa yeye ndio Mungu wao; na alitakiwa kutumia kauli/lugha laini, ili ujumbe umfikie mlengwa ipasavyo na huwenda ukimfikia ukamuathiri na kumpa sababu ya kubadilika na kuwa mja mwema kwa kuogopa adhabu za Allah SWT

*(Quran 20:44)                                Zungumzeni naye kwa kauli nzuri, kwa hivyo labda anaweza kuwa msikivu kwa ujumbe wangu au akahofia adhabu zangu*
Ni dhahiri kwamba Ujumbe wa dini unapaswa kufikishwa kwa kauli nzuri, njema hata kwa wale wanaoweza kuwa wanaonekana kuwa kwenye upotovu. Allah SWT hakuamrisha matumizi ya nguvu au ubabe popote katika kufikisha ujumbe wake.

*(Quran 16:125)   "linganieni njia ya Allah SWT kwa kutumia hekima na mawaidha mazuri, na muwe wema katika majadiliano yenu"*
Mwenyezi Mungu SWT ametuamrisha kulingania dini yake kwa kutumia hekima, mawaidha mazuri na tuwe wema/wazuri katika majadiliano yetu. Tusimtukane mtu wala tusimpige au kumuumiza mwengine kwa namna yoyote.

Kwa maelezo yaliyowasilishwa hapo, kwa ushahidi wa Quran; Uislamu haukubaliani kabisa na kitendo walichokifanya hao vijana cha kumpiga huyo mtu kwa kula mchana wa Ramadhani, kwa kumdhalilisha kwa kumchukua video ni dhahiri kwamba hao vijana hawakuwa wenye elimu ya dini ya kiislamu walipochukua hatua kama hiyo. Zaidi ya hapo, lengo kubwa la ibada ya saumu ni kwa anayefunga kupata Ucha Mungu; sasa swali la kuwauliza wale vijana na wenye mawazo yanayofanana na wao, je hicho kitendo walichokifanya kinawafikisha kwenye lengo?

Uislamu umekamilika katika kila idara na sekta, na hata kama ingelikuwa kuna mwongozo katika jamii kwamba watu wasile hadharani mchana ndani ya mwezi wa Ramadhani, basi wa kuadhibu itakuwa Mamlaka iliyotoa huo mwongozo na sio vijana waliokosa elimu na wanadhihirishia ulimwengu mzima kuwa ni wajinga. Kwa kitendo chao hicho hao vijana wamemkosea yule waliyempiga, wamejikosea wenyewe nafsi zao, wameikosea Zanzibar kwa kuitukanisha sana kwa makosa yao na zaidi ya hapo wameukosea Uislamu kwa kuupa sifa ambazo ni kinyume na mafundisho yake. Kwa niaba yao, tunawaomba msamaha wote ambao watakuwa wamekwazika kwa kitendo chao kwa namna moja au nyengine.

*3.2 KITENDO HICHO KILIFANYIKA MWAKA 2017, SIO MWAKA 2024*
Ushahidi wa kimtandao umethibitisha kuwa kitendo hicho kilifanyika mwaka 2017; takriban miaka saba iliyopita. Taarifa tulizo nazo ni kwamba hatua kali zilichukuliwa kuhusiana na kadhia ya kitendo hicho. Tumebaini kwamba kuna watu wenye nia mbaya na ovu na amani na utulivu tunaoendelea nao hapa nchini wameirudisha katika mzunguko video ya tukio hilo huku wakitoa maelezo kuwa limefanyika mwaka huu.

Tunawaomba Watanzania na wapenzi wote wa amani waipuuzilie mbali video hiyo kwa kuwa ni ya zamani na hatua zilishachukuliwa. Aidha, tunawaomba *TCRA* wafuatilie kwa kina chanzo cha hii video kuingia katika mitandao ya kijamii na wajiridhishe dhamira ya aliyeasisi video hiyo kuingia mit andaoni mwaka huu. Aidha, wale wote wanaotumia video hiyo kueneza chuki, wazingatie kuwa hilo ni kosa na ni kinyume na mila ya nchi yetu; na pia tukienda katika Injili ya  *1 Yohana 4:8* '*
*_Yeyote asiyependa hamjui Mungu kwa kuwa Mungu ni Upendo'_*  na *1 Yohana 4:16* *_"Tunatambua kwa kiasi gani Mungu anatupenda sisi, nasi tumeweka imani yetu yote katika upendo wake. Mungu ni Upendo, na wote wanaoishi ndani ya Upendo wanaishi ndani ya Mungu na Mungu anaishi ndani yao'_*

Tuepuke mihemuko ambayo inaweza kukuza chachu ya chuki kwenye jamii ambayo kwa maslahi mapana ya amani endelevu ndani yake inafaa zaidi kudumisha upendo. Jamii yetu kwa sasa inakabiliwa na uadui mkubwa wa mmomonyoko wa maadili ikiwemo suala zima la kukua kwa mahusiano ambayo hayatoweza kuendeleza kizazi chetu kwa miongo kadhaa ijayo; kwa sasa tunapaswa tuungane na tushirikiane kukabiliana na uovu ambao utapata mwanya wa kupenya katika nyufa za mahusiano yetu.

*4.0  TAMATI*

Tuungane kwa pamoja kukemea tabia ovu za kiuchochezi kwenye jamii. Tusikubali kufarakanishwa kwa kutumia video za matukio yaliyopita zenye dhamira ya kugombanisha jamii na kuyumbisha amani na utulivu tulio nao. Kwa kuwa kosa lilitokea, na hatua ilishachukuliwa; sisi tuishi ndani ya Injili ya *Luka 23:34* _Yesu Akasema 'Baba wasamehe, kwa maana hawajui walitendalo'_ - kutokana na maelezo ya kwenye andiko hili, vijana walitenda kosa lakini hawakuwa wenye kulijua walitendalo. Tuishi kwa amani na upendo, siku zote. Tusiruhusu chuki na vurugu nchini kwetu.

*WITO KWA JAMII*

Tuhimizane kufanya juhudi ya kutafuta ELIMU. Matendo yanayokirihisha, kukera na kuudhi hufanywa na watu waliokosa ELIMU. Dini zetu zinahimiza Upendo baina yetu na miongoni mwetu, Zinahimiza kuheshimiana na kuthaminiana. Tusiutukuze ujinga kwa kuruhusu chuki katika Jamii.

*TANBIHI*

Unaruhusiwa kunakili, kunukuu au kusambaza 

Post a Comment

0 Comments