Na Joseph Ngilisho ARUSHA
Ujenzi wa jengo la utawala katika halmashauri ya jiji la Arusha,imeiweka pabaya Jiji la hilo, kutokana na uwepo wa mapungufu katika hatua ya utoaji wa tenda mara baada ya kubainika kuwepo kwa mianya ya Rushwa.
Jengo hilo la utawala linalomilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Arusha, linatarajia kutekelezwa kwa gharama ya Sh 12 Bilioni.
Hata hivyo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imebaini kukiukwa kwa taratibu za mchakato wa upatikanaji wa Zabuni ya Ujenzi wa Jengo hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Arusha Zawadi Ngailo amesema Mapungufu ya ujenzi wa jengo hilo la Halmashauri ya jiji la Arusha, ilibainika kwenye uwepo wa mianya ya Rushwa kuanzia mchakato wake wa tenda iliyotangazwa njia ya vikwazo (Restrictive tendering) badala ya tenda ya wazi.
Zawadi amesema kuwa baada ya kubaini mapungufu hayo walichukua hatua ya kusimamisha mchakato huo na kuitaka Jiji kutangaza upya kwa njia ya wazi.
Alisema Taasisi yake ilipata taarifa za tukio hilo mwishoni mwa mwaka jana, na kuanza kulichunguza kwa karibu hadi kubaini mapungufu hayo.
“Baada ya kupokea taarifa, tulifanya ufuatiliaji wa zabuni hiyo ambapo pia tulibaini uwepo wa mianya ya Rushwa katika mchakato wa uteuzi wa njia ya manunuzi kama inavyoelekezwa na kanuni, na kwenye uundwaji na utekelezaji wa jukumu la uchambuzi yakinifu” alisema Zawadi.
Kwa upande mwingine Zawadi alisema, katika ufuatiliaji wa fedha za umma zilizotolewa na serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali kwa miezi mitatu kuanzia mwezi January hadi March, mwaka huu pia wamebaini mapungufu katika miradi mingine minne.
Amesema walibaini mapungufu kwenye mfumo wa maji katika vyoo vya shule ya sekondari 'Lake Eyasi' iliyoko Wilaya ya Karatu, unaojengwa kwa thamani ya Sh584.280 milioni lakini pia mapungufu katika ujenzi wa Shule ya Sekondari Kamwaga uliyoko Wilaya ya Longido wenye thamani ya Sh584.0 milioni.
"Katika miradi hii miwili, tuliagiza kamati ya ujenzi wa Shule hizo, zisimamie urekebishwaji wa miundo mbinu hiyo kwa kuzingatia kiwango cha ubora" amesema Zawadi.
Ujenzi wa mtaro wa barabara ya Mtaa wa Naurei iliyoko kata ya Sekei Wilaya ya Arumeru wenye thamani ya Sh 30 milion, nao umebainika kuwa na mapungufu sambamba na ujenzi wa nyumba za walimu 6:1katika shule ya Maweni iliyoko ndani la Jiji la Arusha, unaotekelezwa kwa Sh 70 milioni ambazo Zawadi amesema kuwa wameelekeza zote zifanyiwe marekebisho na maboresho.
"Kwenye ujenzi wa Mtaro wa Naurei, kwanza mradi imecheleweshwa na hakuna vibao vya tahadhari lakini kwa ujenzi wa nyumba moja ya walimu sita Kuna dosari katika malipo ya zaidi ya Sh 2.4 milioni yaliyofanywa na mzabuni na vyote tumebaini na wahusika wamekubali na wanarekebisha" alisema Zawadi.
Alitoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za Rushwa kwenye utekelezaji wa miradi ili kuendelea kulinda rasilimali fedha za umma zisitumike vibaya kwa maslahi ya wachache.
Ends ...
0 Comments