Na Joseph Ngilisho ARUSHA
MAELFU ya wakazi wa jiji la Arusha wakiwa na Majonzi vilio na simanzi ,wamejitokeza kuiaga miili ya wanafunzi nane na raia mmoja waliokufa maji , kwenye tukio la gari la Shule ya msingi Ghati Memorial lililotumbukia kwenye korongo lenye maji kasi ya mvua.
Tukio hili limetonesha kidonda cha wazazi na wakazi wa jiji hili kukumbuka ajali ya basi la shule ya msingi Lucky Vicent iliyoua watoto 32 ,walimu wawili na dareva mmoja wilayani Karatu ,June 6,2017.
Watoto hao walikumbwa na mauti April 12,Mwaka huu majira ya saa 12.30 asubuhi baada ya gari la shule hiyo walilokuwa wamepakiwa marehemu hao lenye namba T 496 EFL kuacha njia na kutumbukia kwenye korongo la maji mengi ya mvua katika mtaa wa Engosengiu ,Sinoni katika jiji la Arusha.
Katika maombolezo hayo yaliyofanyika kiwanja cha wazi cha shule ya Msingi Sinon ,serikali imetoa mkono wa pole wa sh,milioni moja kwa kila familia ya mzazi aliyepoteza mtoto na sh,milioni 5 kwa familia ya msamalia mwema ,Brian Tarangie(34)aliyekufa maji akijaribu kuwaokoa wanafunzi hao.
Hata hivyo vilio vilitawala zaidi katika eneo hilo pale miili ya marehemu hao ikiwasili na wakati majina ya marehemu yakisomwa na kufanya eneo zima la maombolezo kuzizima kwa vilio.
Marehemu hao ni Winfrida Emmanuel mwanafunzi wa darasa la Awali,Abialbol Peter darasa la awali,Articia Emanuel darasa la tatu,Shedrack Emanuel darasa la sita,Dylan Jeremiah, Noela Jonas darasa la awali pamoja na msamalia Brian Tarangie.
Mkuu wa wilaya ya Arusha,Felisician Mtahengerwa aliagiza Magari yote ya shule katika kipindi hiki cha Mvua, yachukue wanafunzi kuanzia majira ya saa 1.30 asubuhi badala ya saa 12.
Pia aliwaagiza askari wa usalama barabarani kuhakikisha wanayafanyia ukaguzi wa mara kwa mara magari yote ya shule sanjari na kuyakamata yale yanayokiuka utaratibu kwa kufanya kazi nyakati za mvua kubwa.
Naye Mkurugenzi wa jiji la Arusha mhandisi Juma Hamsin alisema rais Samia Suluhu Hasani ameguswa na msiba wa wanafunzi hao lakini ameguswa zaidi na msamalia mwema Brian Tarangie aliyejitolea kuokoa maisha ya watoto hao na kuamua kuipatia familia yake pole ya sh,milioni 5.
Meya wa jiji la Arusha Maxmilian Iranghe alisema ni wakati wa serikali kufanya usaili wa madereva wanaoendesha magari ya wanafunzi na kuwapatia mafunzo maalumu ili kuepuka ajali zisizo na ulazima.
Ends..
0 Comments