Na Joseph Ngilisho ARUSHA
Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP),limezindua ofisi yake mkoani Arusha, ikiwa ni kutekeleza mpango wake wa kusaidia vijana katika kilimo cha biashara na ufugaji na kukuza hali zao za kiuchumi.
Aidha serikali pamoja na wadau wengine, wameliomba shirika hilo,kurudisha mpango wa lishe, kwenye shule za pembezoni na jamii za wafugaji, ili kuwanusuru wanafunzi wa maeneo hayo na utapiamlo.
Akiongea katika hafla ya kuzindua ofisi za WFP Mkoani hapa, kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Arusha John Mongela, Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Kanali Wilson Sakulo, alisema wanafajirika kuona shirika hilo la kimataifa kurejea kwa kishindo nchini wanaimani changamoto za lishe mashuleni zitapata ufumbuzi.
Alisema miaka ya nyuma WFP walikuwa wakitoa chakula kwenye shule za pembezoni na jamii za wafugaji na kuongeza ufaulu,uelewa na kupunguza utoro shuleni.
"Lakini hali imekua mbaya zaidi na kuongezeka kwa hali ya utapiamlo kwa watoto chini ya miaka mitano, hasa Wilaya za Longindo na Monduli, baada ya kusitishwa kwa mpango huo na kusababisha hali ya ufaulu na uwezo wa kuzingatia masomo kupungua kwenye shule nyingi za maeneo hayo, ya wafugaji,"alisema.
Alisema hali hiyo inatokana na mabadiliko ya tabia nchi, ambayo yamesabisha ukame na mafuriko ya mara kwa mara, yanayoathiri shughuli za kilimo na mifugo katika maeneo hayo na mengine mkoani humo,ambazo shughuli zake hutegemea chanzo kikubwa cha vipato kwenye kilimo na mifugo.
"Lakini mbali na kusababisha athari katika kilimo na mifugo, pia wanyamapori huathirka na ukame,ambao ndio chanzo cha utalii unaoleta kipato kwa wanaanchi wa mkoa huu na Taifa, nawaomba WFP fikirieni jinsi ya kurudisha mpango endelevu wa lishe shuleni maeneo haya kwa kushirikiana na serikali,wadau na wazazi,"alisema.
Aidha alisema serikali inatambua juhudu za WFP za kushirikiana na serikali na walengwa, katika kutatua changamoto za mabadiliko ya tabia nchi yanayoleta athari ya utapiamlo.
"Lakini tunatambua jitihada zenu za kusaidia wakulima wadogo kupata pembejeo bora na kwa wakati ,kupata masoko ya mazao na kupunguza upotevu wa mazao yao baada ya kuvuna,"alisema
Pia alipongeza WFP kuzindua mpango wa kusaidia wakulima na wafugaji kuelewa njia bora za kutumia taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa, ili kuepuka athari kabla ya kutokea.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Sarah Gordon alisema uwepo wa ofisi yao utasaidia kutekeleza mpango wao wa kusaidia vijana katika kilimo cha biashara na ufugaji na kukuza hali zao za kiuchumi.
"Katika mradi huu ni lazima tuunganishe nguvu zetu, serikali, washirika wa maendeleo wa sekta binafsi, wabunifu na WFP ili kufikia lengo la maendeleo endelevu ambalo ni kumaliza njaa, kuwa na usalama wa chakula,kuboresha lishe na kukuza kilimo endelevu,"alisema.
" Ni muhimu tuwekeze kwa vijana, hasa wanawake. wawezeshwe kwa maarifa, ujuzi na vitendea kazi vitakavyowasaidia kukidhi mahitaji ya soko na kuchangia katika uchumi wa Tanzania.
Mwisho
0 Comments