WAONGOZA UTALII WACHACHAMAA,WAIVIMBIA TANAPA MALIPO YA DOLA 50 KUINGIA HIFADHINI,WAMWANGUKIA RAIS SAMIA AINGILIE KATI, WATOA SIKU 7,WADAI WAZIRI AMESHINDWA KUWASAIDIA

 Na Joseph Ngilisho ARUSHA 

Waongoza utalii mkoa wa Arusha,wametoa siku saba kwa rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati na kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazowakabili ili kufikia malengo ya serikali ya kufikisha idadi ya watalii elfu 5 ifikapo 2025.


Akiongea  kwenye mkutano wa pamoja uliokutanisha vyama mbalimbali vya waongoza utalii nchini,Mwenyekiti wa mkutano huo,Abdallah Noar,alisema moja ya changamoto  hizo ni pamoja na kutakiwa kulipa leseni na viingilio pindi wanapoingia kwenye hifadhi .

Alisema wao ni sehemu ya watumishi katika sekta ya utalii hivyo hawapaswi kulipia viingilio wanapoingia kwenye ofisi zao ambazo ni hifadhi za Taifa.

Noar alisema  machi 7,Mwaka huu walipokea barua kutoka shirika la Hifadhi za Taifa Tanapa,inayowataka waongoza utalii kote nchini ifikapo Mei 1,mwaka huu mfumo wa kudhibiti waongoza utalii wasio na leseni kuingia hifadhini, utaanza kutumika rasmi.
Alisema barua hiyo inalenga kutekeleza mfumo wa kuthibiti waongoza watalii wasiokuwa na leseni ya biashara (TTBL) .

Sehemu ya barua hiyo inasema kuwa sheria ya Utalii Na.29 ya mwaka 2008 kifungu cha 42(1)kinaelekeza kuwa kila mwongoza utalii anapaswa kusajiliwa kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa katika kifungu cha 42(2).

Mwenyekiti huyo ambaye amemtaja rais Samia kama mwongoza utalii namba moja nchini, wamemwomba kuwasaidia kuondoa changamoto hiyo ambayo wanadai inawaumiza katika shughuli zao.

"Tunapofika kwenye milango ya kuingia kwenye ofisi zetu tunatakiwa tuoneshe kuwa tumelipia leseni kupitia fedha za kigeni na tunashurutishwa kulipa kwa  dola 50 za kimarekani wakati nchi yetu inatumia shilingi, huu ni mzigo mkubwa kwetu tunashindwa kutekeleza"

Mwenyekiti huyo alienda mbali zaidi na kuhoji mbona waheshimiwa wabunge ,Madaktari na walimu hawalipishwi leseni wanapoingia kwenye ofisi zao, iweje wao wawekewe masharti ya kuingia kwenye ofisi zao wakati wote ni wafanyakazi???.

"Changamoto kubwa kabisa ambayo imekuwa kero kwa waongoza utalii ni kulipishwa leseni na viingilio  wakati tunaingia kwenye ofisi zetu za kuizalishia serikali na kukuz utalii ambazo ni hifadhi za taifa,tunaomba rais aingilie kati na kuondoa hilo"

Wadau hao wa utalii kwa pamoja wametoa wiki mbili kwa rais Samia kutatua kero hiyo na baada ya muda huo kwisha bila majibu sahihi wataitana tena ili kupata kauli nyingine ya pamoja watakayokubaliana.

Alisema kuwa sheria hiyo ilipitishwa na bunge mwaka 2008 lakini ilikuwa haifanyi kazi hadi juzi walipoiibua upya, hata hivyo alisisitiza kuwa sheria hiyo haikuwa shirikishi na inamapungufu mengi ukizingatia kuna watu wengi wanafanyakazi kwenye hifadhi za utalii.

Naye mwongoza utalii wa kujitegemea,Levis Lewis alisema vijana zaidi ya asilimia 70 Tanzania wamejiajiri kufanya kazi ya kuongoza utalii na kupitia sera hiyo inapingana na kile kinachofanyika kwa sasa kudaiwa leseni.

Alisema Hadi sasa amefanyakazi ya utalii kwa miaka 35, hakuwahi kuona jambo la aina hiyo la kudaiwa leseni kwani waongoza utalii kipato chao ni kidogo na malipo yanayoainishwa kuyalipia ni mengi  na suala la utalii ni la msimu.

"Sisi sio wafanyabiashara tunalipa leseni ya nini sisi ni waajiriwa kama wafanyakazi wengine tupo hapa kuhudumia watalii ili serikali yetu ipate mapato kwanini tunatozwa malipo ya leseni tena tunatakiwa kulipa kwa dola"alihoji .




Ends....


Post a Comment

0 Comments