Na Joseph Ngilisho ARUSHA
Wakala wa Barabara Mkoa wa Arusha (Tanroads)imefanikiwa kutekeleza ujenzi wa miundo mbinu ya Barabara yenye urefu wa zaidi ya kilometa 150 ikiwa ni mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitatu tangu Rais Dk.Samia Suluhu Hassan aingie madarakani .
Akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake ,Meneja wa TANROADS mkoani hapa,mhandisi Reginald Massawe alisema Tanroads imetekeleza juhudi kubwa za serikali ikiwemo matengenezo na ukarabati wa barabara na madaraja na kufanya mtandao wa barabara katika mkoa wa Arusha kuwa mkubwa na kuingiliana katika wilaya zote za mkoa huo.
Mhandisi Massawe aliishukuru serikali kutokana na ongezeko kubwa la bajeti ya matengenezo ya barabara na kufanikisha upanuzi mkubwa wa mtandao wa barabara za lami.
"Kuanzia mwaka 2021 hadi 2024, mtandao wa barabara za lami umeongezeka kutoka kilomita 425.78 hadi kilomita 478.78, ikiwa ni ongezeko kubwa la kilomita 53".
Massawe, alibainisha kuwa mafanikio yanayoonekana ni pamoja na ujenzi wa barabara za lami kama vile Wasso-Sale (kilomita 49), T/Packers-Bypass (kilomita 1), na Kijenge - Usariver (kilomita 3).
Zaidi ya hayo, zaidi ya kilomita 152 za barabara kwa sasa zinajengwa kwa kiwango cha lami, ikiwa ni pamoja na miradi kama Mianzini-Ngaramtoni Juu (kilomita 18), Karatu-Kilimapunda (kilomita 51), na Mbaunda-Losinyai (kilomita 28).
Pia Serikali imeanzisha miradi kabambe kama vile ujenzi wa barabara ya Arusha-Kibaya-Kongwa (kilomita 453) na barabara ya Karatu – Mbulu – Haydom – Sibiti River – Lalago – Maswa (kilomita 339). Aidha, mipango inaendelea ya ujenzi wa barabara ya Arusha - Kibaya - Kongwa yenye urefu wa kilomita 453.2.
Pamoja na miundombinu ya barabara, mafanikio makubwa yamepatikana katika ujenzi wa madaraja, ambapo miradi iliyokamilika ikiwamo Daraja la Nduruma na Daraja la Kimosonu mkoani hapa.
Aidha, uwekaji wa taa 991 kwenye barabara mbalimbali zikiwemo Arusha-Namanga, Arusha-Minjingu na Kijenga-Usariver, umeimarisha usalama na mwonekano wa madereva.
Pamoja na jitihada zinazoendelea za kuboresha miundombinu katika mkoa mzima, Mkoa wa Arusha unaelekea katika maendeleo zaidi na ukuaji wa uchumi chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu.
Ends...
0 Comments