Ngilisho Tv-Live
Watu wasiojulikana wamemfyatulia risasi zisizopungua nne Mbunge wa Simanjiro Mkoani Manyara, Christopher Ole-Sendeka akiwa ndani ya gari lake safarini na Dereva wake majira ya saa moja leo usiku na kisha kukimbia muda mfupi baada ya Mbunge huyo kuanza kupiga risasi juu kuwatishia.
Akiongea kwa njia ya simu, Sendeka amesema “Ni kweli nimeshambuliwa kwa risasi majira ya saa moja kasoro katika Wilaya ya Kiteto kati ya Kijiji cha Ngabolo na Ndedo, kulikuwa na gari ambayo ilikuwa inanifuatilia kwa nyuma tukawapisha kidogo kama tunataka kuwapisha wapite kulia walipofika usawa wetu wakaanza kumimina risasi kwa Dereva na baada ya hapo wakavuta kwenda mbele halafu wakaanza kuzipiga za usoni na sisi tukakata kona kugeuza na Mimi nikaanza kupigapiga (risasi) za juu pale kuwatishiatishia ndio tukafanikiwa kugeuza na kuondoka”
“Walikua na silaha kubwa na silaha ndogo, hakuna aliyepata madhara tulikuwa Mimi na Dereva wangu ni gari tu ndio wameichakazachakaza wameipigapiga, mpaka sasa kwakuwa tumekuja gizani huku hatujazihesabu lakini zipo risasi moja, mbili, tatu, nne kama nne hivi hatujazihesabu lakini nne au tano hivi zipo waziwazi (matundu ya risasi yanaonekana kwenye gari)”
“Kuhusu kwanini nimeshambuliwa bado sijui bado siwezi kusema jambo kwa wakati huu, sio rahisi pia kujua sura za waliohusika katika kipindi kama hicho” Mbunge Ole-Sendeka ameiambia
Wakati huo huo,jeshi la Polisi kutoka Makao Makuu Dodoma limesema kikosi maalumu cha polisi wametumwa kwenda kusaidiana na wenzao kwa uchunguzi mkoani Manyara.
Msemaji wa Jeshi la Polisi Makao Makuu ya Polisi
Dodoma, Tanzania, DCP David A. Misime amesema Polisi wanafuatilia tukio hilo kwa karibu sana na uchunguzi ulishaanza mara tu baada ya kupokea taarifa.
“Timu ya Wataalamu wa uchunguzi wa matukio na matumizi ya risasi kutoka Makao Makuu ya Polisi Dodoma imetumwa kwenda kushirikiana na Timu ya Mkoa wa Manyara kuchunguza tukio hilo ili kubaini waliohusika ni akina nani na madhumuni au kusudio lao lilikuwa ni nini na baada ya uchunguzi wa Wataalamu taarifa kamili itatolewa”
0 Comments