MFANYABIASHARA BILIONEA AMSHUKIA VIKALI KAMANDA WA POLISI DAR ES SALAAM,ADAI KUTISHIWA MAISHA AKIMBIA NA PIKIPIKI KUTOKA DAR HADI ARUSHA,AJIPANGA KUKIMBILIA MAHAKAMANI,KAMAMDA MULIRO ADAI ANACHEKESHA

 Na Joseph Ngilisho ARUSHA

Mfanyabiashara maarufu wa Magari Jijini Dar es salaam,Samweli Shami(38) maarufu Bilionea Shami, amedai kutishiwa maisha na watu aliodai ni zvigogo wa polisi jijini humo na kulazimika kuyakimbia makazi  yake kutoka dar akitumia usafiri wa pikipiki na kukimbilia jijini Arusha.


Akiongea na vyombo vya habari jijini Arusha, Bilionea Shami ambaye anamiliki kampuni ya magari ya Ongezeko Trading Co ltd,alisema amelazimika kuishi kama digidigi kwa takribani mwezi mmoja kuwakimbia polisi waliokuwa wakimsaka na kumtishia maisha kwa madai kwamba wametumwa na kigogo mzito wa serikali.

Alidai kupigiwa simu na Kamanda wa polisi kanda maalumu ya dar es salaam, Muliro Jumanne Muliro akimtaka kurejesha kiasi cha sh,milioni 129 alizopokea kama  Malipo ya awali kwenye mkataba wa sh,milioni 958 waliokubaliana kuiuzia malori 9 ya mtumba yenye tela zake ,kampuni ya Afrinexus Logistics  ltd ya mjini Mtwara baada ya kampuni hiyo kuvunja mkataba kinyume na utaratibu.

Shami alisema kampuni yake ya Ongezeko Trading  co Ltd ya jijini dar es salaam, iliingia makubaliano hayo September 12 ,2023 ya kuiuzia malori kampuni  hiyo ya Afrinexus Logistics kwa makubaliano kwamba baada ya siku 21 za kazi malori hayo yangeingia nchini kutoka China. 

Alisema baada ya makubaliano hayo , kampuni ya Afrinexus Logistics ilianza kuingiza  fedha kidogo kidogo kwa awamu  6 kwenye akaunti yake ambapo siku ya kwanza aliingiziwa sh, milioni 27.2,siku inayofuata sh,mil 25.5, sh,milioni 16.15,sh,milioni 29.57,sh,milioni 5.1, na sh,milioni 25.5 na fedha hizo kufikia jumla ya sh, milioni 129 .



"Niliwauliza kwanini  wanaingiza fedha kidogo kidogo , walinijibu ni masuala ya kibiashara, hawawezi kutoa fedha zote kwa mkupuo mmoja  "

"Baada ya malipo hayo ya awali ,kampuni ya Afrinexus Logistics walinipigia simu kuniambia kuwa wameshapata malori ya haraka  hivyo hawatahitaji tena,jambo ambalo ni kinyume na utaratibu "

"Niliwauliza itakuwaje na mimi nilishatoa oda China, waliniambia nisijali tutaongea,basi niliwajulisha huko mchina waliniambia walishafanya oda kwenye meli na itanilazimu wanikate dola 18,000 "

Alisema mapema mwaka huu, Februari 3,alipigiwa simu na Kamanda Muliro akimwambia afike ifisini kwake na baada ya kuitikia wito huo akiwa na mwanasheria wake,Muliro alimwambia ameagizwa na kiongozi mkubwa wa serikali(jina tunalo) arejeshe  kiasi cha sh,milioni 129  huku akimsisitiza kuwa  hatatoka ofisini kwake bila kutoa kiasi hicho cha fedha .

"Nilifika ofisi ya Kamanda Muliro nilimkuta akiwa katika hali ya kupaniki akawa ananifokea sana kuniambia kunatuhuma kutoka kwa mtu mkubwa sana serikalini kuwa wewe ni tapeli umefanya biashara za kitapeli lipa pesa za watu,nilijitahidi kumuuliza iwapo kama ameona mkataba wa mauziano aliniambia hahitaji mkataba lipa pesa za watu" 

"Baada ya mabishano ya muda mrefu sana Kamanda Muliro aliniambia ndugu yangu Samweli wewe ni mdogo wangu usibishane na dola ukishaambiwa mtu ameshika mpini wewe umeshika makali hauta muweza, nakushauri kama mdogo wangu nenda kalipe hizo fedha na kuanzia sasa hutatoka hapa mpaka utuambie utalipaje hizo fedha"

"Nikiwa hapo ofisini walinibana sana na kushikilia gari yangu na baadaye waliniambia nijidhamini nilienda nyumbani na kesho yake nilirejea ofisini kwa kamanda Muliro, waliendelea kunibana nikapiga simu kwa rafiki yangu akanikopesa milioni 20,tulienda benki usiku na askari polisi tukachukua pesa na kuziingiza kwenye akaunti ya Afrinexus Logistics na baadaye walinirejeshea gari yangu kwa masharti nikalipe fedha zote"

Alisema askari hao wakiongozwa na Kamanda Muliro waliendelea kumpigia simu yeye pamoja na mke wake wakimtisha kwamba iwapo asipolipa fedha hizo watamfungulia kesi yoyote na tayari wamekamata lori lake lililokuwa Mkoani Simiyu wakimshinikiza alete pesa na  wametishia kuliuza iwapo ataendele kukaidi  .

"Wameingilia mawasiliano yangu ya simu na akaunti zangu za benki kila pesa inayoingia wanaona na wametishia kuzima WhatsApp yangu niliamua kwenda kulala hotelini ila walinifuatilia na kuja kuzingira hoteli niliyolala "

"Nilifanikiwa kutoroka hotelini kwa kutumia usafiri wa bodaboda hadi mto Wami nilipofanikiwa kupata usafiri mwingine wa kwenda Arusha"

Alisema kwa sasa anajipanga kulifikisha suala hili mahakamani na tayari ameanza mchakato wa kukutana na mwanasheria wake  ili suala hilo likaamuliwe kisheria kuliko utaratibu unaotumiwa na upande wa pili wa kutumia nguvu ya askari polisi .

"Kwa sasa polisi wananitishia maisha wakisema kuwa hao unaosikia wanaokotwa kwenye viroba ni watu kama wewe hivyo nimepata hofu huenda yakanikuta mimi ama familia yangh"

Samweli alimwomba Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati suala hili kwa kuwa yeye ni Mfanyabiashara anayetambulika ili suala hili liamuliwe kisheria .

Kamanda Muliro alipotafutwa kwa njia ya simu alisema alipata malalamiko  (bila kumtaja mlalamikaji)na kuanza uchunguzi wa madai hayo ikiwemo kumwita Shami ofisini kwake .
RPC MULIRO

Alisema  hajatumwa na kigogo yoyote wa serikali kama taarifa zinavyosambaa mitandaoni na mimi siwezi kumhoji mtu kupitia jina la waziri mkuu,ila kuna watu wameleta madi yao ndio maana tunafanya uchunguzi .

"Mimi sijatumwa na Waziri Mkuu nimetumwa na Raia wanaodai kutapeliwa"

"Tumebaini huyo mtu amechukua fedha za watu na anafanyaujanja ujanja kurejesha fedha za watu na anaposema amekimbia na bodaboda hasi Arusha hicho ni kichekesho ameamua kuwachekesha, lalamiko lolote likija polisi tunalifuatilia , tunalichunguza na kulipatia majawabu"

"Sisi tunavyo vitu vya msingi vinavyofanya tumhoji tumegundua kuwepo kwa udanganyifu kwa baadhi ya hati za kibiashara ambavyo vilitufanya tuwasikilize walalamikaji"

Bilionea Shami ambaye kwa sasa yupo jijini Arusha,kukwepa ghasia za polisi Muliro amedai kwamba mawakili wake wapo katika hatua ya kufungua kesi ya madai dhidi ya kampuni ya Afrinexus Logistics ltd kuvunja mkataba bila kufuata sheria hatua ambayo imeipa hasara kampuni yake   .

"Nadai fidia ya gharama za  Meli pamoja na gharama zingine ikiwemo wanasheria wa China kwa ajili ya kusuluhisha kati ya kampuni yake na wauzaji kutoka kampuni ya Shandong zhongyue automobile ya jijini jining  CHINA".


Ends.....



























Post a Comment

0 Comments