Na Joseph Ngilisho ARUSHA
Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya (DCEA) kanda ya Kaskazini, imewataka wadau wa sekta ya usafirishaji wa abiria mkoani hapa, kufanya utambuzi wa mizigo inayosafirishwa na abiria kupitia vyombo vyao vya moto ili kuepusha vyombo hivyo kutumika kusafirisha dawa za kulevya .
Hayo yameelezwa na maafisa ustawi wa jamii kutoka mamlaka hiyo kanda ya kaskazini katika kikao cha wadau wa usafiri kilichoandaliwa na Mamlaka ya udhibiti usafiri Ardhini LATRA,kilicholenga kutoa elimu juu ya kanuni mpya za usafirishaji.
Sara Ndaba afisa ustawi wa jamii kanda ya Kaskazini DCEA,alisema mkakati wa kwanza uliopo mbele yao ni kupunguza uzalishaji na usambazaji wa dawa za kulevya ,kupitia elimu wanayoitoa ukizingatia kwamba vyombo vya usafiri vinatumika sana katika kusafirisha dawa za kulevya ikiwemo Mirungi na bangi .
"Wadau wa usafiri mkoa wa Arusha ni muhimu tuwapatie elimu juu ya madhara ya dawa za kulevya na wao ndio wanavyombo vya usafiri ambavyo vinaweza kutumika kusafirisha dawa za kulevya "
Naye Shaban Miraji afisa elimu jamii kutoka mamlaka hiyo, alisema wadau wa usafirishaji ni muhimu sana kupata elimu hiyo kwani wanahusika kwa kiasi kikubwa kusafirisha mizigo na baadhi yao kusambaza dawa za kulevya.
"Ili dawa za kulevya ziweze kutapakaa nchini lazima vyombo vya usafiri vitumike kusambaza kwa mfano mihadarati aina ya mirungi inapitishwa sana katika mpaka wa Namanga kupitia mabasi ama pikipiki "
"Sisi kama mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya baada ya kubaini hilo tumefika hapa kutoa elimu ili wadau wa usafiri watambue namna ambavyo vyombo vyao vinatumika kusafirisha dawa za kilevya iwe kwa kujua ama kwa kutojua"
Alisema sheria za mamlaka hiyo ni kali sana iwapo utabainika chombo chako kuhusika katika biashara hiyo haramu adhabu yake ni kifungo cha miaka 30 na chombo chake kinataifishwa na kuwa mali ya serikali.
Mmoja ya washiriki wa semina hiyo, Okelo Kostentine , mwenyekiti wa waendesha pikipiki wilaya Arusha alisema sekta ya usafirishaji hasa bodaboda inachangamoto nyingi ikiwemo kusafirisha dawa za kulevya bila kujua.
"Sisi kama viongozi tunajua wapo baadhi wa waendesha pikipiki wanahusika kusafirisha dawa za kulevya ila tukibaini kuna mwanachana anajihusisha na biashara hiyo tunachukua hatua"
Alisema kupitia semina hiyo wataenda kusimamia hilo ili kuwaelimisha wanachama wao namna pekee ya kuepuka usafirishaji wa mihadarati na hatari ilipo mbele yao iwapo watabainika kuhusika.
Ends..
0 Comments