Na Joseph Ngilisho ARUSHA
Changamoto ya upatikanaji wa umeme hapa nchini huenda ikapata ufumbuzi wa kudumu baada ya wadau wa sekta ya nishati ya umeme kukutana jijini Arusha kujadili njia mbadala za upatikanaji wa nishati hiyo katika nchi zao.
Hayo yamebainishwa na kamishna wa nishati jadidifu kutoka wizara ya nishati ,mhandisi Innocent Luoga katika mkutano wa 5 wa kimataifa wa shirika la nishati (TECS),uliowakutanisha wataalamu wa nishati kutoka nchi 10 za ukanda wa Afrika ikiwemo Malawi, Ethiopia , Uganda na Tanzania lengo likiwa ni kujadili changamoto zinazoikabili sekta ya nishati pamoja na kujadili mipango ya kuongeza uwekezaji wa umeme kwa njia mbalimbali katika maeneo ya Tanzania ambayo itasaidia kuondoa upungufu wa umeme .
Aidha alisema katika mkutano huo azimio kubwa linaloenda kufanyika ni kutumia vyanzo mbadala vya upatikanaji wa umeme ikiwemo matumizi ya upepo, joto ardhi, nishati ya jua, maji na gesi.
"Katika kutatua changamoto ya umeme sisi Tanzania tayari tuna miradi mikubwa ya kuunganisha umeme nchi jirani na sasa tunaunganisha umeme Tanzania na Kenya ambapo utatokea Singida, Arusha, unapitia namanga mpaka Isinya nchini Kenya" Alisema.
Alisema kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kupambana na suala la mdororo wa kiuchumi unaosababishwa na kukatika katika kwa umeme mara kwa mara jambo linalopelekea wawekezaji kushindwa kufikia malengo yao.
Kwa upande wake mtendaji Mkuu wa shirika la umeme Tanzania TANESCO hapa nchini ,Gissima Nyamo-Hanga amesema amekuja katika mkutano huo kimkakati na kuangalia mashirikiano ya wadau mbalimbali wa nishati na kuleta mawazo ya kuboresha upatikanaji wa umeme wa uhakika.
Aliongeza kuwa katika kipindi cha hivi karibuni wamejipanga kama shirika kuanza kuzalisha umeme kwa kutumia umeme wa joto ardhi.
Akizungumzia hali ya upatikanai ya umeme wa uhakika hapa nchini,alisema wapo mbioni kukamilisha na watanzania watapata umeme wa uhakika hivyo aliwataka kuwa walinzi wa miundombinu ya TANESCO .
Alisema kwa Sasa Hali ya umeme bado ni changamoto ndiyo maana wamekubaliana na Nchi za Afrika kushirikiana katika matumizi ya nishati jadidifu kuongeza uwezo wakua na nishati ya uhakika .
Ends....
0 Comments