Na Joseph Ngilisho -MONDULI
Shule ya Sekondari ya Mchepuo wa Kiingereza ya Tumaini Senior iliyopo Makuyuni wilaya ya Monduli Mkoani Arusha, imebuni mbinu mpya ya kutoa zawadi zikiwemo fedha tasilimu kwa wanafunzi na walimu wanaofanya vizuri kimasomo ikiwa ni njia mojawapo ya kuongeza morari na ushindani kwa walimu na wanafunzi kufanya vizuri kimasomo.
Hayo yamebainishwa na mkurugenzi wa shule hiyo ya Tumaini Senior ,Modesty Bayo katika hafla ya kuzawadia wahitimu 45 wa kidato cha nne baada ya kuonesha uwezo mkubwa wa ufaulu kwa kupata alama za juu na kuifanya shule hiyo kushika nafasi ya 56 kitaifa kati ya shule 5343,huku wanafunzi wawili tu wakipata Division II na wengine wote Div 1.
Alisema utaratibu huo umesaidia kuongeza Morari kwa wanafunzi kufanya vizuri na walimu kujituma na hivyo kuifanya shule hiyo kushika nafasi za juu ikiwemo nafasi ya 5 kimkoa kati ya shule 246 za mkoa wa Arusha.
"Siri ya mafanikio hayo ni pamoja na kuwajengea mazingira mazuri ya kujifunzia na kufundishia ,kufikia malengo ya mikakati tuliojiwekea pamoja na kuwapatia motisha ambayo imekuwa desturi yetu kupongezana na hii imetusaidia sana kuleta mageuzi ya elimu kwa wanafunzi wetu"
Bayo alisema mafunzo yanayotolewa hapa ni pamoja na masomo ya sayansi kwa vitendo, masomo ya ziada ,kufanya tafiti mbalimbali na kuandaa mada zinazomsaidia mwanafunzi kuwa na uelewa mpana.
Naye mkuu wa shule hiyo, Sifael Msengi alisema katika awamu nne za wahitimu wa kidato cha ,hawakuwa wamefanya vizuri sana ila awamu hii ya tano ambapo wahitimu 45 wamevunja rekodi kwa kufanya vizuri zaidi kwa ufaulu baada yakupata alama za juu na hivyo kutimiza malengo ya shule hiyo .
Alisema malengo ya shule hiyo ni kuhakikisha wanaondoa alama ya division III na kubaki na ufaulu wa division I na division II zikiwa cheche sana jambo ambalo amedai wamelifikia.
"Kwa kufikia malengo hayo tumeona ipo haja kuwapatia motisha wahitimu wetu na walimu wao ili waambukize na wenzao kufanya vizuri na tangu shule yetu imeanza tumekuwa tukishika nafasi za juu ,hii ni pamoja na mshikamano tulio nao hapa shuleni" .
Naye mwalimu wa taaluma wa shule hiyo Masalu Mhekela ,alisema siri ya mafanikio ni kuwa na timu imara ya walimu bora waliojipanga kutoa elimu bora kwa wanafunzi.
Alisema miongoni mwa mikakati ya shule ni kuhakikisha walimu wanatimiza vema majukumu yao waliopangiwa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kila mwanafunzi anafanya vizuri somo la mwalimu wake.
Pamoja na mambo mengine shule hiyo imekuwa ikifundisha kwa vitendo elimu ya ufugaji,kilimo na ujasiliamali.Hatua ambayo imesaidia sana kwa wanafunzi kuwajengea mazingira mazuri ya kujitegemea.
"Hapa Shuleni tunamiradi ya Ng'ombe wa Maziwa,bwawa la Samaki,Nguruwe,Kuku,Sungura pamoja na kuendesha kilimo cha mbogamboga kwa ajili ya kujifunza faida zake na imetusaidia sana kuwa na elimu ya ujasiriamali"alisema Samweli Benedicti anayesima kidato cha sita
Mussa Maringo ni mmoja ya wahitimu wa kidato cha nne waliofanya vizuri, alisema shule hiyo imemsaidia sana kufanya vizuri kutokana na mazingira mazuri ya kujifunzia ikiwemo vifaa vya kujifunzia.
Aliwapongez walimu wao ambao muda wote wamekuwa wakijitoa kuwafundisha bila kujali muda wao wa kazi na wakati mwingine hadi usiku hali iliyowasaidia wao kuyapenda masomo yao na kufanya vizuri.
Ends....
0 Comments