Na Joseph Ngilisho-ARUSHA
Mkuu wa wilaya ya Arusha kwa kushirikiana na halmashauri ya jiji la Arusha wameanza kutekeleza kwa vitendo maelekezo ya Katibu wa siasa na uenezi CCM Taifa ,Paulo Makonda kwa kuzindua wiki ya kero inayolenga kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
Makonda alifanya ziara katika jiji la Arusha mapema januari 23 na 24 mwaka huu na kuelekeza kwa viongozi wa umma kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
Akizindua mpango huo katika viwanja vya ofisi yake,mkuu wa wilaya ya Arusha,Felisician Mtahengerwa aliwataka viongozi wa umma kutumia wiki hii kutenga muda na kusikiliza kero za wananchi na kuzipatia ufumbuzi wa kudumu
"Sisi viongozi wa umma kuanzia ngazi ya mtaa tuwape nafasi wananchi ya kuwasikiliza, mwananchi yeyote atakayekuja ofisi ya mkuu wa wilaya awe amesikilizwa ngazi ya chini na uwe na nyaraka zinazoonesha uliwahi kusikilizwa"
Alisema hata mpokea mwananchi yeyote ofisini kwake ambaye hatakuwa na nyaraka inayoonesha kuwa kero yake imepitia katika ngazi ya chini ya ofisi ya DC.
"Kitendo cha wingi wa wananchi kukimbilia ofisi ya mkuu wa wilaya inaonesha jinsi gani ofisi za mtaa kata na Tarafa hazifanyi kazi ipasavyo"
Aidha alizitaka ofisi zote za kata katika jiji hilo kuweka maboksi ya maoni ili wananchi wapate fursa ya kuweka barua zenye kero zao na kuonya kuwachukulia hatua kali viongozi wenye tabia ya kufungua maboksi hayo na kuchambua barua zinazowahusu bila kuzifikisha kunakotakiwa.
Naye Mkurugenzi wa jiji la Arusha,Mhandisi Jumaa Hamsin alisema tangia ujio wa Katibu wa siasa na uenezi ccm,Paulo Makonda wamepokea kero mbalimbali ambazo zimegawanyika katika makundi mbalimbali zikiwepo za uhitaji wa mitaji.
"Kikundi cha vijana walioomba fedha zaidi ya milioni 17 kama mtaji tulishauriana na wenzangu na kukubaliana tuwapatie sh,milioni 8.3 na baada ya kuzigawanya kila mmoja atapata mtaji wa chini sh, laki 2 na sh,laki 3 kwa mtaji wa juu kwa kila mmoja"
Pia alisema wametatua kero ya muda mrefu ya madai ya wazabuni wapatao 68 wanaodai kuanzia mwaka 2003 hadi 2023 yanayofikia sh, bilioni 1.38 na kwamba hadi leo halmashauri hiyo imefanikiwa kulipa kiasi cha sh milioni 560.
"Na kwa ushuhuda tunaye mwenyekiti wa halmashauri ya Monduli Joseph Kadogoo alikuwa akiidai halmashauri milioni 48 baada ya kukatwa kodi ya zuio pamoja na huduma ya biashara tumemlipa "
Alisema hadi juni 31 mwaka huu halmashauri hiyo itakamilisha kuwalipa wazabuni wote waliobaki
Alisema kundi lingine lililobaki ni wazabuni wa TASAF ambao mchakato wa kuwalipa unaendelea .
Katika hatua nyingine Mkurugenzi huyo alimtambulisha bwana Manyama ambaye ni Mkuu wa idara ya maendeleo ya jamii kuwa atakuwa akihusika na malipo ya fedha za maendeleo ,TASAF badala ya Mkurugenzi wa jiji hilo.
Wakati huo huo Mhandisi Hamsin amewatahadhalisha wananchi juu ya uwepo wa vibali feki vya ujenzi ama ukarabati wa majengo vinavyotolewa na ofisi yake ,akidai kwamba vibali batili ni zaidi ya asilimia 85 katika jiji la Arusha na tayari baadhi ya watumishi waliohusika wamechukuliwa hatua za kinidhamu na kuwataka wananchi wasitumie 'control number' kama kibali cha ujenzi ama ukarabati wa jengo.
Aidha alisema watu wamekuwa wakipewa namba za malipo (control umber )na baada ya kulipia wanaendelea na shughuli zao watambue kwamba hicho sio kibali.
"Wananchi control number sio kibali cha ujenzi ,kibali hakitolewi kwa rushwa kinatolewa kulingana na maombi yako lazima uthibitishe umiliki wa eneo husika, kwa hiyo tusichanganye watu wanaomba kibali cha kukarabati nyumba kumbe wanaenda kujenga maduka hatuwezi kuwa na maduka kila mahali"alisema Mhandisi Hamsin
Ends.....
0 Comments