WAZIRI KAIRUKI AMWAPISHA KAMISHNA KUJI TANAPA,ATOA MAELEKEZO MAZITO TANAPA,MAMIA WAPONGEZA UTEUZI WA KUJI.

Na Joseph Ngilisho ARUSHA.


Waziri wa Maliasili na Utalii ,Angellah Kairuki amemvisha cheo na kumwapisha , Musa Kuji kuwa kamishna wa uhifadhi wa shirika la hifadhi za Taifa (Tanapa)  na kutoa maelekezo Shirika hilo kwa  kulitaka libadilike ili liweze kuchangia ipasavyo  uchumi wa taifa kupitia utalii na kuhifadhi raslimali kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.


Aidha amemtaka kamishna kuji kuliongoza shirika hilo kwa weledi,mshikamano huku akiwa na hofu ya mungu hu akiliepusha na  migogoro isiyo na tija baina ya

 wananchi wanaozunguka hifadhi za taifa.


Kairuki ametoa maelekezo hayo  kwenye hafla  hiyo iliyofanyika katika makao makuu ya TANAPA yaliyopo jijini Arusha .



Alisisitiza kuwa katika kipindi hiki TANAPA inatakiwa kuja na ubunifu wa hali ya juu katika kutangaza vivutio vya utalii na kubaini mazao mapya ya utalii ili sekta ya utalii iweze kufikia lengo la kuwa na wageni milioni 5 na kuliingizia taifa jumla ya dola za kimarekani bilioni sita ifikapo mwaka 2025.


Aidha alimpongeza Rais  Samia Suluhu Hassan kwa maono yake ya kuifungua Tanzania duniani kupitia Filamu ya The Royal Tour na kuwataka watumishi wa wizara kumuunga mkono Rais Samia kukuza sekta hiyo .


Ameitaka TANAPA kukuza na kuimarisha mahusiano na jamii zinazozunguka hifadhi na mbuga za taifa na kujenga  mahusiano na wadau mbalimbali wa hifadhi na utalii ili kuweza kubadilishana mawazo na uzoefu katika uhifadhi na kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii duniani pia uendeshaji wa Shirika kwa ujumla wake.


"Katika kufanya kazi watumishi wanatakiwa kuzingatia kushirikiana na kufanya kazi kama timu mmoja huku wakizingatia taratibu za Serikali ili kuweza kupata matokea tarajiwa kwa haraka"


Kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo waziri Kairuki amesisitiza kutekeleza miradi yote kwa wakati huku akisisitiza kufuata taratibu zote za manunuzi ya umma kwa kuzingatia ubora. Pia kuchukua hatua mapema wakati wowote inapotokea changamoto badala ya kukaa kimya na kuruhusu mitandao kuendelea kupotosha


Waziri alimpongeza Kuji kwa kuteuliwa kushika washifa huo akimweleza kuwa ni kiongozi sahihi mwenye uzoefu wa miaka wa zaidi ya miaka 33 akitumika ndani ya shirika hilo.


"Kuji umeteuliwa kutokana na imani rais aliyokuwa nayo kwako ikiwemo uzoefu wako w miaka 33 ndani ya Tanapa, ombi letu uteuzi wako ukatumike vizuri,ukatumie vipaji vyako na karama yako ukawaunganishe askari na watumishi wote wa Tanapa ,usibague huku ukimtanguliza mungu mbele"


Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas alimtaka Kamishna Kuji  kuwaunganisha watumishi wote katika kipindi chake huku akimsisitiza kumtanguliza Mwenyezi Mungu.


Naye Mwenyekiti wa bodi ya eadhamini Tanapa,Jenerali mstaafu George  Waitara alisema hana shaka na uteuzi wa Kamishna kuji unaobebwa na uzoefu wa miaka 33 ndani ya tanapa tangu ajiunge na shirika hilo Juni 1991.


Jenerali Waitara alisisitiza kuwa Kamishna aendelee kuwa na ukaribu na watu anaowaongoza na kutatua kwa haraka changamoto zao na kwamba iwapo kuna changamoto kubwa asisite kuishirikisha bodi..


"Kiongozi lazima ahakikishe malengo ya shirika yanafikiwa"


Kwa upande wake kamishna wa shirika hilo, Musa Kuji alimshukuru Sana rais Kwa kumteua kuwa kamishna wa uhifadhi Tanapa na kuahidi kuendelea kusimamia rasilimali za Tanapa  na maeneo yote  ya uhifadhi kwa kutumia taaluma vipaji ,busara na  uzoefu huku tukimtangulia mwenyezi mungu mbele.


"Ninaahidi kwamba  nitaendelea kuunga mkono jitihada za serikali kwa kupunguza ama kumaliza kabisa migogoro isiyo ya lazima kati ya shirika na wananchi wanaoishi kando na maeneo ya hifadhi pamoja na kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi kwa wananchi hao kama sehemu ya kujenga ujirani mwema"


Hafla hiyo ilipambwa na kikosi maalum cha wanamuziki kutoka TANAPA ambacho kilitumbuiza wimbo maalum wa kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuigiza Filamu ya The Royal Tour inayohamasisha utalii hapa nchini.







                                         





Ends...






Post a Comment

0 Comments